Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

MENEJA Kanda ya Pwani kutoka Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA), Vicky Mollel amesema kuwa mamlaka hiyo ilitarajia ushindi kutokana na nguvu kubwa waliyoiweka katika kuhamasisha Umma.

Ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Eliakim Maswi, mara baada ya kupokea tuzo ya Mshindi wa kwanza katika kipengele cha Mamlaka za Udhibiti kwenye maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (DITF), maarufu Saba Saba.

Amesema kuwa wamepata mafanikio hayo kwa kuwa wameweza kuhudumia wateja zaidi ya 700 ambapo lengo lilikuwa ni kuhudumia wateja 500.

“Pia tuhakikisha banda letu linakuwa zuri la kuvutia wateja kupata huduma, kwahiyo tunaweza kutembelewa na watu 700 zaidi ya lengo tulilojiwekea la watu 500,” amesema na kuongeza:

“Hata hivyo tunashukuru kwa mafanikio haya makubwa ambayo tumeyapata katika maonesho haya kama PPRA tulijipanga kutoa elimu kwa ajili ya matumizi ya Mfumo wa NeST kutokana na Sheria mpya ya manunuzi ya Umma,” amesema.

Mollel amefafanua kuwa siri ya mafanikio ya PPRA ni kufanya kazi kwa pamoja kama timu na kuweza kujituma.

Aidha amewataka wananchi wanaposikia maonesho wawe wanatembelea kwa kuwa kuna vitu vizuri vinaandaliwa kwa ajili ya wateja wao.

Meneja huyo ameeleza kuwa baada ya kupata tuzo hiyo watakuwa na msukumo makubwa wa kutoa huduma kwa wateja wao ikiwa ni pamoja na kujipanga kwa lengo la kuwafikia wateja zaidi hao.

Amesema wanatamani maonesho yajayo ya 49 waweze kuwahudumia wateja zaidi ya 2000.