Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma.
Serikali imepanga kufanya maboresho ya sheria ya ununuzi wa umma kukidhi mahitaji ya soko, kuondoa urasimu na kuongeza uwajibikaji kwa wanaojihusisha katika ununuzi wa umma.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA) Eliakim Maswi ameeleza hayo leo July 17,2023 Jijini Dodoma, wakati akizungumza na wandishi wa habari kuhusu majukumu ya taasisi hiyo na mwelekeo wa utekelezaji wa bajeti ya mwaka huu wa fedha.
Amesema Serikali haitakuwa na msamaha kwa mtumishi wa umma atakayekwenda kinyume cha utaratibu wa manunuzi ya umma na kwamba katika mwaka huu wa fedha imepanga kupunguza siku za mchakato wa ununuzi kwa lengo la kuongeza ufanisi katika kutekeleza miradi.
“Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, amedhamiria kubadilisha utendaji wetu kama mamlaka na anataka tutoke tulipo kwa kutumia njia mbalimbali ikiwemo matumizi ya mifumo ya kielektroniki kuleta tija na ufanisi unaostahil,” ameeleza.
Maswi amesema katika mwaka huu wa fedha serikali imetenga sh. bilioni 40.4 kwa PPRA kuendesha shughuli mbalimbali za kiutendaji na kwamba katika fedha hizo sh. bilioni 20 zitatumika kwa uwekezaji, ukaguzi wa taasisi na kuwajengea uwezo watumishi.
Pia, Maswi amesema serikali imefanya maamuzi ya kuanzisha mfumo mpya wa manunuzi wa kielekroniki National e-Procurement System of Tanzania (NeST) kudhibiti rushwa, mchakato wa zabuni kuchelewa na kuongeza uwazi wa zabuni.
Amebainisha kuwa lengo la kuanzisha mfumo huo ni kuongeza uwazi katika ununuzi wa umma, usimamizi mzuri wa fedha za umma, kudhibiti vitendo vya rushwa, ufuatiliaji kukidhi sheria, uwajibikaji na udhibiti wa manunuzi.
“Taasisi zinazosimiwa na Msajili wa Hazina na Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa, zinapaswa kuanza kutumia mfumo mpya kwa shughuli za ununuzi wa umma kuanzia mwaka huu wa fedha.
Aliongeza kuwa: “Ifikapo Oktoba Mosi mwaka huu taasisi nunuzi zote za serikali hazitaweza kutuma mialiko ya zabuni katika mfumo wa zamani wa TANePS na badala yake zitapaswa kutumia mfumo wa NeST.”amesema.