Mfuko wa Pensheni za Mashirika ya Umma (PPF) umetangaza kuongeza fao la elimu kuanzia kidato cha nne hadi cha sita, ikiwa ni sehemu ya kusherehekea miaka 35 ya mfuko huo.

Katika mazungumzo na wanahabari Dar es Salaam hivi karibuni, Meneja Uhusiano na Masoko wa PPF, Lulu Mengele, amesema maelezo zaidi kuhusu fao hilo yatatolewa hivi karibuni katika mkutano wa wanachama na wadau wa PPF utakaofanyika Oktoba, mwaka huu.

 

Amesema mtaji wa mfuko huo umekua kutoka Sh milioni 50 mwaka 1978 (ulipoanzishwa kama Shirika la Bima kabla ya kuanza kujitegemea kama PPF mwaka 1992) hadi thamani Sh trilioni 1.3, mwaka huu.

 

Mengele amesema katika kipindi chote hicho PPF umeweza kulipa mafao kwa wastaafu zaidi ya 25,607 ambapo unalipa Sh zaidi ya bilioni 3.7 kwa mwezi kama pensheni pekee, achilia mbali mafao mengine.

 

“Katika kusherehekea miaka 35 ya mafanikio ya PPF, tulipanga kuwa na Wiki ya Huduma kwa Wateja kuanzia Julai mosi hadi 5, mwaka huu. Tunawaomba wateja wafike kwa wingi ili wapate maelezo zaidi kuhusu huduma na shughuli zitolewazo na PPF,” amesema Mengele.

 

Ameongeza kuwa wakurugenzi wa PPF watahudhuria maadhimisho hayo kwa kuhudumia wateja katika ofisi za Mkoa wa Dar es Salaam Kanda ya Ilala, Temeke, Kinondoni na Makao Mkuu.

 

“Shughuli hiyo itaenda sambamba na maonesho ya Sabasaba, ambapo Mfuko utashiriki na tunawakaribisha sana kutembelea banda la PPF katika viwanja vya Sabasaba,” amesema.

 

Michango ya wafanyakazi inatakiwa kuwasilishwa PPF na waajiri ndani ya siku 30 kila mwezi. Kucheleweshwa au kutowasilisha michango ya wanachama ni kosa la jinai. Mwajiri anayetenda kosa hilo anastahili kutozwa asilimia tano kwa kila michango iliyocheleweshwa kwa kila mwezi kwa kipindi ambapo michango husika imecheleweshwa.

 

Mafao ya elimu hutolewa kwa watoto wa mwanachama anayefariki akiwa katika ajira na tayari amekwishachangia miaka 3 au zaidi. Huduma hiyo hutolewa kugharimia sehemu au gharama zote zinazohitajika katika elimu ya mtoto wa mwanachama aliyefariki. Gharama hizo ni kuanzia elimu ya chekechea hadi kidato cha nne.

 

Mafao ya kiinua mgogo hutolewa kwa mwanachama anayeondoka katika ajira akiwa na kipindi cha kuchangia ambacho ni chini ya miezi 120. Sababu za kuondoka katika ajira ni kupunguzwa kazini, kustaafishwa kwa manufaa ya umma au kuondolewa na mamlaka iliyokuweka katika ajira.

 

Kila mwanachama wa PPF hupatiwa kadi ya uanachama mara baada ya kujaza fomu ya kujiunga na kuiwakilisha PPF. Wanachama wanaweza kupata taarifa za michango yao, madai na pensheni kupitia tovuti na simu yake ya kiganjani kupitia namba 15553.

 

Kwa upande mwingine, PPF hutoa mikopo kwa wanachama wake kupitia Vyama vya Kuweka na Kukopa Fedha (SACCOS) kwa masharti nafuu.

 

Pia PPF imejenga nyumba 580 za makazi katika eneo la Kiseke, Mwanza kwa ajili ya kuwauzia na kuwakopesha wanachama na wasio wanachama nyumba za bei nafuu.