Mfuko wa Pesheni ya Mashirika ya Umma (PPF) imefanikiwa katika suala ka kujikinga, kuzuia maambukizi ya VVU sehemu ya kazi.

Mpaka sasa hakuna mfanyakazi aliyejitokeza kuwa mwathirika, hatua hiyo imetokana na Menejimenti ya PPF kutoa elimu kwa wafanyakazi wake.

Hayo yalizungumzwa na Mkurugenzi wa PPF, William Erio, wakati alipowakaribisha wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi.

Amesema PPF imetenga  bajeti inayokwenda sanjari na mikakati mathubuti ya kuzuia maambukizi na kujikinga, ili kujenga PPF yenye wafanyakazi wenye afya bora katika kuwahudumia wanachama na Taifa kwa ujumla.

“PPF tunaamini kuwa na wafanyakazi ambao hawana maambukizi, ni hatua na msingi ya awali ya kupata matokeo makubwa sasa.

Pia katika bajeti, PPF imetenga fungu ambalo hulielekeza kwa jamii kwa masuala ya Ukimwi. Hili hutolewa pale ambapo PPF inaombwa kufanya hivyo,” amesema Erio.

Erio amesema PPF imekuwa ikiwasomesha watoto wa wanachama waliofariki kuanzia shule za chekechea hadi sekondari kidato cha nne na kuanzia mwakani hadi kidato cha sita.

Amesema kwa kuwa kwa kuwa taarifa za sababu za vifo vya wanachama ni siri, PPF haina takwimu sahihi ya wazazi waliofariki kwa ugonjwa huo, Lakini kati ya Januari na Juni 2013, mfuko umesomesha  watoto 1,151 katika shule mbalimbali za msingi na sekondari kwa gharama ya Sh milioni 651.

Huduma na mafunzo kwa waathirika

Amesema PPF imekuwa ikitenga katika bajeti yake fungu kwa ajili ya huduma kwa waathirika na wanafamilia wa mfanyakazi aliyeathirika. Jambo hilo ni endelevu na kila mwaka PPF itaendelea kutenga bajeti husika.

Hata hivyo, hadi sasa hakuna mfanyakazi aliyejitokeza kuhitaji huduma, matunzo au matibabu ya kwake au ya mwanafamilia wake.

Masuala ya VVU na Ukimwi PPF,  jamii

Erio amesema Kamati ya Ukimwi imekuwa na mipango mbalimbali ya kusaidia jamii. Kamati inaelimisha jamii kuhusu masuala ya VVU na Ukimwi.


Katika Mkutano wake wa kila mwaka wa wadau na wanachama wa PPF, kumekuwa na mada ya masuala ya Ukimwi na jambo hili ni endelevu. Pia inatoa misaada mbalimbali ya kifedha kwa ajili ya shughuli zinazohusu Ukimwi kwa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na taasisi zisizo za kiserikali kama vile Benjamin Mkapa HIV/AIDS Foundation.

Matibabu

Amesema katika Sera ya Ukimwi ya Mfuko wa PPF kuna kifungu kinachoainisha kuhusu kutunza siri. Hatua hiyo inawafanya wafanyakazi walioathirika na wako tayari kupata matibabu na huduma, wanatakiwa kutoa taarifa ya afya zao kwa siri ili waelekezwe utaratibu wa matibabu na huduma zinazotolewa na mwajiri.

“Ili kulinda usiri wa taarifa husika, taarifa hutolewa kwa Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala tu ambaye yeye ndiye mwenye jukumu la kumwelekeza mfanyakazi taratibu zote za huduma na matibabu.

Amesema PPF ina mkataba na mojawapo ya mashirika ya Bima ya Afya (AAR) na kipengele cha matibabu ya waathirika kimepewa kipaumbele.

Utekelezaji wa programu

Amesema kuwa katika kutekeleza programu ya Ukimwi, PPF katika mwaka huu ilitenga kiasi cha Sh milioni 100 katika bajeti yake kwa ajili ya utekelezaji wa sera na programu ya Ukimwi kwenye Mfuko.

Kati ya fedha hizo, Sh milioni 25 ni kwa ajili ya kusaidia juhudi za Serikali na asasi mbalimbali kupambana na ugonjwa huu katika jamii (community outreach).

Erio anasema programu ya Ukimwi ya PPF imejikita katika maeneo makuu matatu, ambayo ni kujikinga na kuzuia maambukizi mapya ya VVU.

Matibabu kwa waathirika wa Ukimwi na Matunzo na Huduma kwa waathirika wa Ukimwi.

Amesema katika kuzuia maambukizi ya VVU, waelimishaji rika wamekuwa na vipindi vya dakika 45 mara moja kwa mwezi vya kuelimishana na kujadiliana na kikundi cha wafanyakazi wenzao wapatao 18-20 kuhusu masuala ya Ukimwi sehemu ya kazi.  PPF ina jumla ya wafanyakazi 311 ambao wapo katika vikundi 17.

PPF pia imekuwa na utaratibu wa kumwalika mtaalamu wa masuala ya Ukimwi kila mwaka mara mmoja, ili kutoa elimu kwa wafanyakazi wote. Waelimishaji rika wamekuwa wakipatiwa mafunzo na wataalamu wa masuala ya Ukimwi mara moja kwa mwaka pia.

“Hii ni katika kutekeleza programu ya kujikinga na kuzuia maambukizi mapya ya Ukimwi PPF. PPF imekuwa na utaratibu wa usambazaji wa kondomu kwa wafanyakazi wake kila mwezi na kazi hii haiishii kwa wafanyakazi tu bali kwa jamii pia.

“Kondomu huwekwa kwenye vyoo vya ofisi zote ambavyo hutumika pia na wanachama, wadau na wageni wanaofika katika ofisi za PPF.

“PPF imekuwa ikiendesha kampeni kwa wafanyakazi kuhusu kuhamasisha upimaji wa hiari ili mfanyakazi ajue hali yake ya kiafya na kwa walioathirika kupata ushauri ili waishi kwa matumaini.

“Aprili mwaka huu, PPF ilizindua kampeni ambayo ilipewa kaulimbiu ya ‘Maambukizi sifuri kwa wafanyakazi wa PPF’ (getting to zero),” amesema.

Amesema waelimishaji rika na menejimenti walijitokeza katika upimaji wa hiari katika kampeni hiyo.

 

Wakati wa mafunzo wafanyakazi wote walipata fursa ya kupima kwa hiari ikiwa ni mwendelezo wa kampeni hiyo.

Kampeni husika ilikuwa na madhumuni ya mwajiri kupata tathmini ya maambukizi ya Ukimwi ili kujiandaa na mipango na bajeti madhubuti ya kukabiliana na ugonjwa husika na huduma na matibabu kwa waathirika.

Katika mpango wa kujikinga na kuzuia maambukizi, wafanyakazi wapya wamekuwa wakielimishwa kuhusu sera, programu na shughuli za Ukimwi katika PPF mara tu wanapoajiriwa.

Mpango mkakati kukabiliana na VVU, Ukimwi

Katika kutekeleza Sera ya Ukimwi, PPF ina mpango mkakati wa masuala ya Ukimwi na uongozi wa PPF umeunda Kamati ya Ukimwi ambayo Mwenyekiti wake ni Mkurugenzi Mkuu wa PPF.

Wahusika katika kamati hiyo ni  wajumbe wanne kutoka Menejimenti ya PFF ambao ni Mkurugenzi wa Rasilimali Watu (ambaye pia ndiyo Katibu wa Kamati), Mkurugenzi wa Fedha, Mkurugenzi wa Uendeshaji na Mkurugenzi wa Masuala ya Sheria.

Mameneja watatu kutoka Kurugenzi ya Rasilimali Watu na Utawala (mmoja ikiwa ni Mratibu), na Meneja wa Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu (Uhusiano na Masoko) na Mwenyekiti na Katibu wa Chama cha Wafanyakazi (TUICO), Tawi la PPF.

Majukumu ya Kamati

Erio amesema Kamati ya Ukimwi ya PPF ina majukumu ya kutunga rasimu ya sera na kusambaza kwa ajili ya maoni na kurekebisha kwa ajili ya kupitishwa na Bodi ya Wadhamini kwa utekelezaji.

Amesema mara kwa mara na pale inapohitajika, Kamati hupitia sera kwa minajili ya kuifanyia marekebisho ili iendane na vipengele muhimu vinavyohusu masuala ya Ukimwi mahala pa kazi.

Amsema jukumu jinguine la Kamati ni kushauri juu ya utekelezji na usimamizi wa sera ili kupunguza unyanyapaa na ubaguzi katika sehemu ya kazi.

“Pia Kamati huandaa mpango wa utekelezaji wa programu ambao unahusisha uandaaji mafunzo ya elimu rika, kuratibu na kusimamia elimu rika katika PPF na kuandaa semina ya uhamasishaji kwa wafanyakazi na familia zao.

“Kujifunza sheria ya Taifa na utekelezaji wake kwa wafanyakazi wa PPF, yaani sheria maalum juu ya VVU na Ukimwi na sheria ya kupambana na ubaguzi,” amesema Erio.

Amesema pia Kamati hutathmini athari za VVU katika PPF na mahitaji ya wafanyakazi walioathirika na Ukimwi kwa kufanya tafiti za msingi na kuhakikisha kuwa siri husika zinatunzwa.

Kuhakikisha huduma muhimu za afya na habari zinazohusu afya za wafanyakazi zinapatikana kwa wote sehemu ya kazi.

Kusimamia, kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa programu za VVU na Ukimwi na kupitia ripoti za waelimishaji rika.

Katika kutelekeza mpango mkakati, Kamati ya Ukimwi iliteua waelemishaji rika 34 kutoka ngazi mbalimbali za wafanyakazi (kuanzia ngazi ya uongozi wa kati (middle management) mpaka wafanyakazi wa ngazi ya chini kutoka ofisi za kanda na makao makuu ili kuendesha na kutekeleza programu ya VVU na Ukimwi

Sera na mpango mkakati kukabiliana na Ukimwi PPF

Amesema Sera ya Mfuko wa PPF ina sehemu kuu sita ikizungumzia madhumuni ya sera, sera yenyewe, utekelezaji wa sera, muundo wa Kamati ya Ukimwi ya Mfuko.

Amesema kazi za kamati hiyo na nia ya dhati ya Mfuko ni kutekeleza Sera hiyo. Mfuko utaelimisha wafanyakazi na familia zao juu ya kujikinga, kupata huduma za matibabu na ushauri na nasihi juu ya ugonjwa huo kwa kupitia vipeperushi, vijarida na semina.

Wafanyakazi watakaoathirika na maambukizi hayo wataendelea kufanya kazi mpaka pale ambapo afya zao hazitawaruhusu kuendelea kufanya kazi husika, na pia kutolewa kuhamishiwa sehemu nyingine.

Amesema wanatoa elimu kwa wafanyakazi juu ya masuala ya utoaji damu na kuongezwa damu salama. Kutunza siri za taarifa za mfanyakazi mwathirika. Stahili ya mfanyakazi kupandishwa cheo na kupata mafunzo kutoathiriwa na hali yake kiafya na kutoa kondomu katika maeneo ya kazi.

Amesema kupima Ukimwi kuwa ni suala la hiari. Pia wamepiga marufuku mfanyakazi kunyanyapaliwa kwa sababu ya kuwa na ugonjwa huo.


Mbali na kuwa na sera husika, PPF ina mpango mkakati kuzuia, kujikinga, matunzo, huduma na matibabu ya kupunguza makali ya Ukimwi kwa walioathirika katika sehemu ya kazi.

 

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Masuala ya UKIMWI  Lediana Mng’ong’o liapongeza PPF kwa hatu ilizochukua kukabiliana na maambukizi ya ungojwa huo

 

Aliutaka mfuko kutobweteka na mafaniko waliyoyapata bali waongeze bidii katika kutoa elimu katika mitaa na maeneo wanayotoka wafanyakazi wake.


Nendeni na huko mitaani kwa majirani ndugu wanoawazunguka huko majumbani kweni msiishie hapa tu ili mkatoe elimu hii kwa kufanya hivyo mtakuwa mmelisaidia taifa,” amesema Mng’ong’o.

 

Amesema mfuko huo ni mfano wa kuigwa na mifuko mingeni ambayo haina utaratibu wakutoa elimu ya Ukimwi kwa wafanyakazi wake.


Amempongeza Mkurugenzi wa Mfuko huo kwa kukubalia kuwa mwenyekiti wa kamati inashughulikia masuala ya Ukimwi kwani ni nadra kuona wakurugenzi wanakubali kushika nafasi hiyo.

PPF ulianzishwa kwa Sheria namba 14 ya mwaka 1978 (ambayo sasa inafahamika kama Sheria ya Mfuko wa Pensheni wa PPF Sura na 372 ya sheria za nchi), kwa madhumuni ya kutoa mafao ya pensheni na mafao mengine yanayoendana na hayo kwa wafanyakazi wote walio katika sekta rasmi na zisizo rasmi.

Mfuko wa Pensheni wa PPF unaelewa fika ya kwamba Virusi vya Ukimwi na Ukimwi ni janga la kitaifa na kimataifa.

 

Hivyo katika kukabiliana na ugonjwa huo hatari, PPF ina sera ya kujikinga na kukabiliana na Ukimwi, ambayo ilipitishwa na Bodi ya Wadhamini wa Mfuko mwaka 2006 na kufanyiwa marekebisho mwaka 2011.

Sera hiyo ilifanyiwa marekebisho ili iende sanjari na Kanuni ya Utendaji wa ILO juu ya masuala Virusi vya Ukimwi (ILO Code ya Practice on HIV/AIDS and the World of work) ya mwaka 2001 ambayo inaelekeza ushirikiano kati ya waajiri, wafanyakazi na wadau.

Katika kuhakikisha sehemu za kazi zina sera na programu sahihi zinazoshughulikia masuala ya kinga, matunzo, huduma na matibabu kwa waathirika wa Ukimwi sehemu ya kazi, na sera ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi ya mwaka 2001.

Mfuko wa Pensheni wa PPF uliipitisha sera husika baada ya kuona umuhimu wa kulinda afya za wafanyakazi na katiba kuhakikisha hivyo sera hii inasimamiwa na uongozi wa juu wa PPF.