Mfuko wa Pensheni wa Mashirika ya Umma (PPF) umewatoa wasiwasi wafanyakazi wa mashirika ya umma waliochangia tangu mwaka 1978, kwa michango isiyoonekana kwenye mtandao wa mfuko huo.
Mkurugenzi Mkuu wa PPF, William Erio (pichani chini), ameiambia JAMHURI mwishoni mwa wiki kuwa wafanyakazi wa mashirika ya umma wakiingia kwenye mtandao wa mfuko huo wanaona michango yao kuanzia mwaka 1994 na kuendelea ila hilo lisiwatie hofu.
“Tulipoanzisha mfumo huu, tulibaini kwamba kwanza michango ya zamani ilikuwa midogo midogo. Ilikuwa watu wanachangia Sh 1,000 au 1,700, hivyo ni gharama kuiingiza kwenye mfumo takwimu za kuanzia mwaka 1978 hadi sasa,” Erio ailiambia JAMHURI.
“Lakini pili, kwa mfumo wa ukokotoaji wa hesabu wa sasa, hesabu muhimu ni miaka mitano ya mwisho ya utumishi, ambapo hesabu za mfanyakazi atalipwa nini zinakokotolewa kwa kutegemea mshahara aliokuwa anapata mtumishi kila mwezi katika miaka mitano ya mwisho wa utumishi wake,” amesema.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa michango ya nyuma inayoendelea kuhifadhiwa katika majalada ya zamani, nayo itahesabiwa katika siku ya kumlipa mtu mafao yake kwa nia ya kutambua alianza kuchangia lini na amechangia kiasi gani.
“Kama kuna mtu anataka kuona hesabu zake kwa uhalisia amechangia nini tangu mwaka alioajiriwa, basi awasiliane na sisi tutamtengenezea hesabu zake tangu siku ya kwanza alipochangia, lakini muhimu nasisitiza ni ile mishahara ya miaka mitano ya mwisho ndiyo msingi wa kukokotoa hesabu za mafao yake, na tarehe aliyoajiriwa kwa maana ya kujua amechangia miezi mingapi,” alisema Erio.
Kauli ya Erio itakuwa imewaondolea hofu wafanyakazi wa mfuko wa PPF walioanza kudhani kuwa watakosa sehemu ya mafao yao yasiyoonekana kwenye mtandao wakati uhalisia ni kwamba mafao hayo yamehifadhiwa katika majalada kama ilivyokuwa zamani, kuepusha gharama kubwa ya kuhamisha kumbukumbu kutoka kwenye vitabu kwenda kwenye mtandao.