Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA), imewasihi wadau wa Ununuzi wa Umma Mikoa ya Kanda ya Ziwa kushiriki mafunzo ya matumizi ya moduli ya kuwasilisha na kushughulikia rufaa na malalamiko kwa njia ya kielektroniki katika Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST) Februari 4 – 6, 2025 jijini Mwanza.

Rai hiyo imetolewa na Katibu Mtendaji wa PPAA,James Sando wakati akizungumza na waandishi wa habari katika maonesho ya Wiki ya Sheria yanayoendelea katika viwanja vya Nyerere Square Jijini Dodoma na kuongeza kuwa mafunzo hayo yatakayoambatana na tamko rasmi la kuanza kwa matumizi ya moduli hiyo.

Sando amesema Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imekamilisha moduli ya kuwasilisha na kushughulikia rufaa na malalamiko kwa njia ya kielektroniki (Complaint and Appeal Management Module) katika Mfumo wa NeST.

“Mafunzo ya matumizi ya moduli kwa Kanda ya Ziwa yanawalenga wazabuni na watendaji wa taasisi nunuzi wa mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Kagera, Musoma, Geita na Simiyu. Mafunzo yatafanyika kuanzia tarehe 4 – 6 Februari, 2025 Jijini Mwanza katika Ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) uliopo Capripoint,” amesema Sando.

Katibu Mtendaji wa PPAA, Bw. James Sando akizungumza na waandishi wa Habari (hawapo pichani) katika maonesho ya Wiki ya Sheria yanayoendelea katika viwanja vya Nyerere Square Jijini Dodoma.

Ameongeza kuwa mafunzo kuhusu matumizi ya moduli ya kuwasilisha na kushughulikia rufaa na malalamiko kwa njia ya kielektroniki katika Mfumo NeST yataendelea kwa kanda nyingine za kaskazini, kati, nyanda za juu kusini pamoja kusini.

“Natoa wito kwa wadau wa kanda nyingine ambazo hazijapatiwa mafunzo kujiandaa kwani watafikiwa na kupatiwa mafunzo kuhusu matumizi ya Moduli hivi karibuni, ” amesema.

Awali malalamiko na rufaa zilikuwa zinawasilishwa na mzabuni kufika katika Ofisi za PPAA Jijini Dodoma.

Aidha, kutokana na mabadiliko ya Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2023 kuweka sharti la lazima la kufanya ununuzi wa umma kieletroniki, PPAA kwa kushirikiana na PPRA imejenga moduli itakayotumika kuwasilisha malalamiko na rufaa kieletroniki bila kuwa na ulazima wa kufika katika ofisi za PPAA.

Mei 28 – 29, 2024 Mafunzo ya matumizi ya moduli ya uwasilishaji wa malalamiko/rufaa kwa njia ya kieletroniki yaliandaliwa na PPAA kwa mikoa ya Dar es Salaam, Tanga Morogoro na Pwani.