Mabadiliko ya ulimwengu wa leo yamemfanya Mpita Njia (MN) naye aishi kulingana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.
Ni kwa sababu hiyo, naye amejikuta analazimika kujua namna ya kuingia kwenye mitando na ‘kuchati’ japo kasi yake si kama ya wenye ulimwengu wa sasa, yaani vijana.
Mpita Njia ingawa ana umri mkubwa, amejitahidi kuwa memba kwenye makundi mengi ya whatsapp na mengine mengi.
Kinachomfurahisha ni kuona yamekuwapo mapinduzi makubwa sana kwenye utoaji na upatikanaji wa huduma kupitia mitandao ya simu.
Kwa mfano, MN sasa halazimiki kwenda kupanga foleni kwenye ATM au ndani ya benki kupata vijisenti vyake vya pensheni. Mambo yote anayamalizia kiganjani.
Malipo ya huduma za maji na nyingine nyingi anazipata kupitia kiganjani.
Lakini kuna watu Mpita Njia anawashangaa kweli kweli. Sijui ni uzee, kiburi au dharau – wamepuuza kabisa mabadiliko.
Hawa si wengine, bali ni Shirika la Posta. Wiki iliyopita MN alifika kwenye ofisi kuliko na sanduku lake la barua. Ofisi hizo hazitaji, lakini ziko wilayani Kinondoni.
Mpita Njia alifika hapo kwa lengo la kulipa ada ya mwaka ya sanduku hilo la barua. Akapokewa na bi mkubwa mmoja. Baada ya kumweleza shida yake, akajibiwa kwamba huduma ya kompyuta kwenye tawi hilo imepata mushkeli. Akamshauri MN aende ofisi yoyote ya Posta ahudumiwe!
Jibu hili likamfanya MN awe mnyonge. Kwa shingo upande akarudisha fedha mfukoni na kuondoka.
Kwa kituko hicho, akajiuliza ni kwa namna gani hadi mwaka huu 2019 Posta haijawa na ubunifu wa kuwawezesha wateja wake kufanya malipo kwa njia ya mtandao? Akajiuliza, kama mamlaka za majisafi na majitaka, mashirika ya ndege na wengine wote wameweza, hawa wanashindwa nini?
Mpita Njia akajiuliza, hili nalo linahitaji wapewe amri kutoka Magogoni au Chamwino? Yaani hawana ubunifu hadi wasukumwe? Mpita Njia anawashauri wahusika wabadilike. Huduma za malipo ya masanduku ya barua zitolewe kwa njia ya mtandao, vinginevyo MN ataamini kuwa kwa ukongwe wa Posta watumishi nao wamechoka.