Na David John, JamhuriMedia, Dar

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Dkt.Ally Possi amefungua warsha ya siku tano kwa watendaji na wataalamu wanaofanya kazi na Shirika la Uwakala wa Meli nchini (TASAC) katika ukumbi wa kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam, lengo likiwa kuwajengea uwezo na kubadilisha uzoefu.

Akifungua warsha hiyo juzi Dkt Possi amesema warsha hiyo ni muhimu kwa wataalamu hao kwani pamoja na mambo mengine mafunzo watakayoyapata yataendelea kuwaimarisha, kuwajengea uwezo lakini pia watabadilishana uzoefu.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Kaimu Mkenge akizungumza na waandishi wa habari.

Amesema mafunzo hayo ni muhimu hususani kwa watalamu wote ambao wanafanya kazi na TASAC kwa kutambua uwepo wa majanga na ajali ambazo zinajitokeza hususani kwenye anga na majini na kwamba Serikali imekuwa ikiwekeza kwa kiasi kikubwa kwenye sekta hizo.

“Mafunzo haya ni muhimu sana sana kwa kutambua kwamba maeneo yetu ya sekta ya anga na majini yanakuwa salama hivyo kongamano hili au mafunzo haya ni muhimu sana kwani watalaamu wetu watapa ujuzi wa kisasa na lazima tutambue kuwa nchi na bara letu linakabiliwa na changamoto gani na katika siku hizi tano wahakikishe wanakuja na suluhisho ,”amesema Dkt.Possi.

Ameongeza kwamba anafahamu nchi zetu zinakosa vifaa vya kisasa lakini pia mambo ya kibajeti, hivyo watalamu wakae wafundishane na waje na mapendekezo ambayo Serikali wataendelea kuyachukua na kimsingi Serikali wanamikataba ya kimashirikiano ya kimataifa ambayo pia kuna masuala ya utafutaji na uhifadhi kupitia sekta hizi za anga na majini.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Dkt. Ally Possi akifungua warsha ya siku tano ya wataalamu wa sekta ya anga na majini iliyoandaliwa na TASAC kwa ufadhili wa Shirika la Kimataifa la IMO

Amesema lazima wataalamu wapate ujuzi wa kutosha kwani hata zinapojitokeza changamoto waweze kushirikiana na wenzao lakini pia nchi isipokuwa na vyombo au utaratibu wa uokoaji na utafutaji katika sekta ya anga na majini basi itakuwa na changamoto na kuhatarisha utafutaji wa sekta nyingine.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli ( TASAC), Kaimu Abdul Mkeyenge amesema kuwa lengo kubwa la mafunzo hayo yatakayotolewa na wakufunzi wa kimataifa kutoka Shirika la Bahari Dunia (IMO), kwenye shughuli za utafutaji na uokoaji katika majanga au ajali ambazo zinajitokeza maeneo ya majini .

Amesema kimsingi nchi wanachama wa IMO) wanapaswa kutekeleza mkataba ulioingiwa mwaka 1979 ambao unahusiana na masuala ya utafutaji na uokoaji kwa ajali zinazotokea majini, hivyo basi Tanzania kama nchi wanachama hawanabudi kutekeleza kwani walishauridhia na ulianza kufanya kazi tangu mwaka 1985.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Kaimu Mkenge

Mkeyenge amesema wao wamekuwa ni wanachama kwa muda mrefu lakini pia kuna vitu ambavyo vilikuwa bado vinakwenda kwa kasi ambayo haikuwa inaridhisha, hivyo wameona huu ni wakati mahususi kutokana na maeneo yao ya naji kuwa makubwa wenye kilometa 1500 kutoka ukanda wa bahari ya Hindi.

Pia kwene maeneo ya Maziwa,Mito na Mabwawa makubwa nchini , hivyo bila kutekeleza matakwa ya mkataba huo wanaweza wakawa wanapata shida hasa panapojitokeza majanga kama hayo .

Pamoja na mambo mengine alisema cha kwanza wanachoweza kukifanya ni kuwawezesha wadau wote ambao wanahusika na masuala ya utafuataji na uokoaji maeneo ya bahari na ndio maana kuna vyombo vya ulinzi vinavyohusika na usalama vipo.”Kwa hiyo mafunzo hayo yatakwenda kuwawezesha watu hao kuwa wazuri katika maeneo yao.

Ameongeza mafunzo mbalimbali huwa yanafanyikia japo kutoka katika Shirika la bahari Duniani ni kwa ufinyu sana kwasababu ni tabu pia kuwapata lakini inategemea na nguvu ya uhamasishaji kama nchi, hivyo sasa wameamua kutoka na kwenda kuomba fursa ili zije nchini hata kama mafunzo hayo yakiwa yanafanyikia kama ya kikanda.

“Lakini tunahitaji yafanyike hapa nchini ili uelewa uwepo kwa umma wote au wadau katika maeneo hayo, pia mafunzo kama hayo wanategemea yatafanyika tena Juni mwaka huu.”