Wakati uongozi wa Pori la Maswa mkoani Simiyu, ukituhumiwa kupokea rushwa kutoka kwa wafugaji na kuwaruhusu waingize mifugo ndani ya pori hilo, watuhumiwa wawili wamekamatwa na kuachiwa katika mazingira ya kutatanisha.

Uchunguzi uliifanywa na JAMHURI umebaini kuwa waliokamatwa na kuachiwa ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwasinasi, Mayunga Isanzu aliyeingiza ng’ombe 430 katika pori hilo; ma mfugaji mwingine, Kasisi Madekela, ambaye ng’ombe wake 170 walikamatwa kwa kosa kama la Isanzu.

Kwa muda sasa, kumekuwa juhudi za makusudi za wamiliki wa mifugo mingi ambao wengi wao ni viongozi, wanasiasa na wafanyabiashara wakubwa; kutaka waruhusiwe kuchungia mifugo katika Mapori ya Akiba, Mapori Tengefu, Hifadhi za Taifa na maeneo mengi yanayohifadhiwa kisheria.

Wiki iliyopita, Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, aliuthibitishia ulimwengu wa wahifadhi kuwa Serikali haina mpango wa kulitenga Pori Tengefu la Maswa kwa ajili ya kutumiwa na wafugaji.

Kauli ya Profesa Magembe, ilikuja baada ya swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Gimbi Masaba (Chadema), aliyetaka Serikali ilitenge pori hilo kwa ajili ya wafugaji. Pori la Akiba la Maswa, linapakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwa upande wa Kusini na muhimu mno katika ikolojia ya hifadhi hiyo. Pori hilo limepunguzwa kwa nyakati tofauti-mara tano-ili kuwawezesha wafugaji kupata eneo la malisho.

Uchunguzi umebaini kuwa wanasiasa, wafanyabiashara na viongozi wengine wenye ukwasi hununua ng’ombe dhaifu na kisha kutumia malisho katika maeneo ya hifadhi ili kuwanenepesha kabla ya kuwapeleka minadani kuwauza. Hatua hiyo imesababisha kuwapo kwa shinikizo kubwa la kutaka maeneo ya hifadhi yamegwe.

Hivi karibuni JAMHURI liliandika habari ya kuwapo baadhi ya wahifadhi katika Pori la Akiba la Maswa kupokea fedha kutoka kwa wafugaji na kuruhusu mifugo kungia.

Baadhi ya wafugaji wamelalamika kukamatwa na askari wa wanyamapori ilhali wakiwa wameshawapa fedha ili wawaruhusu kuingiza na kulisha mifugo ndani ya pori hilo.

Matukio hayo ya wahifadhi kuhongwa na wafugaji yanatajwa kuwa ya kawaida, na hivyo kuliweka pori na mengine nchini katika hatari ya kutoweka.

Hivi karibuni wafugaji wanane walikamatwa, lakini watatu wakaachiwa huru baada ya kuwasuta askari kuwa iweje wawakamate wakati wamewalipa.

Kutokana na madai ya askari kuhongwa, askari wanyamapori, wa Kituo cha Nyasosi (jina tunalo) alimkata panga askari mwingine wa kampuni binafsi aliyetajwa kwa jina la Mbogoma.

Chanzo chetu cha habari kilisema alimkata panga Mbogoma akimtuhumu kuchunua mgao wa fedha zilizotolewa na wafugaji kwa kiongozi wa askari wa wanyamapori.

“Kweli fedha hizo zilitolewa, akapewa (jina tunalo) halafu akaondoka. Yule askari wanyamapori wa Kituo cha Nyasosi alifika na kumvamia Mbogoma akimtaka ampe pesa zilizoachwa na (anamtaja ofisa wanyamapori) baada ya kuchukua kutoka kwa wafugaji.

“Hili suala lilifikishwa polisi na mipango ilikuwa ikifanywa ili kesi hiyo ifutwe.”

Vyanzo vya habari vimesema baadhi ya viongozi wa Pori la Akiba Maswa ndio wanaowatuma askari wao kukusanya fedha kutoka kwa wafugaji na kuwaruhusu kuingiza mifugo porini.

Imeelezwa kuwa viongozi wa Maswa wanapopokea fedha hizo, nao hutuma sehemu ya fedha hizo kwa baadhi ya viongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii walio makao makuu jijini Dar es Salaam. Majina yao tunaendelea kuyahifadhi kwa kuwa hatujazungumza nao.

Miongoni mwa wanaotajwa kuwa kwenye mgao huo wale waliowahi kufanya kazi Maswa na kwa hiyo wanaujua vema ‘mchezo’ wa uchotaji fedha kutoka kwa wafugaji.

“Mifugo ni mingi sana. Ng’ombe walio ndani ya Maswa wanaweza kufika hata 30,000. Pori linakufa kwa sababu ya rushwa. Wakubwa wanaotakiwa wasimamie hili pori wao kila siku ni safari tu za Mwanza, Bariadi na Shinyanga. Hawana habari na uhifadhi.

“Kwa sasa kuna maelfu ya mifugo Maswa. Askari wa Pori wanapokea pesa wanaachia wafugaji wafanye wanavyotaka, hali ni mbaya kweli kweli,” kimesema chanzo chetu.

Mkuu wa Doria, Shirima na Meneja wa Pori la Maswa, Ayoo, hawakupatikana kuzungumzia tuhuma hizo za kutolinda vilivyo pori hilo.

Hata hivyo, Kaimu Mkurugenzi wa Mapori katika Wizara ya Maliasili na Utalii, Kanyata, ameulizwa na JAMHURI juu ya tuhuma za kuwapo mtandao wa rushwa kwa askari wa Pori la Maswa hadi kwa maofisa makao makuu wizarani naye, akajibu kuwa hana taarifa hizo.

“Kwanza mimi si msemaji wa wizara, nadhani ingekuwa vizuri ukawasiliana na mzungumzaji ili akujibu,” alisema.

Pori la Akiba la Maswa ni sehemu ndogo kati ya sehemu kubwa mno ya maeneo ya hifadhi nchini iliyovamiwa na wafugaji na wakulima. Licha ya Serikali ya Awamu ya Tano kuahidi kulinda rasilimali hiyo, bado haijaonesha ‘makeke’ katika kupambana na wafugaji wavamizi, majangili, wachoma mkaa na waharibifu wengine wa mapori hayo.