Ni jambo la kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa hatua iliyofikiwa na Tumaini Media kuanzisha matangazo katika Jiji na Mkoa wa Dodoma. Kupitia Tumaini Media tunapata huduma nyingi za kiroho, kimwili na kijamii, ikiwa ni pamoja na uinjilishaji, kuelimisha umma kuhusu masuala mbalimbali ya kimwili ikiwemo maadili yetu ili tuishi vizuri kwa upendo, furaha na amani. Kwa uwezo na nguvu ya Roho Mtakatifu: kupitia mapaji (mfano, hekima, elimu na nguvu tulizonazo) pia matunda yake ndani mwetu (amani, furaha, upendo, wema, kuvumiliana na kiasi) tunasonga mbele vizuri.

Kama sikosei, Tumaini Media ni chombo cha Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam chini ya Askofu Mkuu Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo na wasaidizi wake: Askofu Mkuu Mwandamizi, Mhashamu Yuda Thadeus Ruwa’ichi na Askofu Msaidizi, Mhashamu Eusebius Nzigilwa.

Sasa Tumaini Media imetua jijini Dodoma, moja ya majimbo 34 ya Kanisa Katoliki nchini. Wakazi wa Dodoma na mikoa jirani wameanza kufurahia maudhui na huduma zake. Haya ni mafanikio mazuri kwa Tumaini Media, hivyo nichukue fursa hii kuupongeza uongozi wa Tumaini Media chini ya Mkurugenzi Padri Paul Haule na menejimenti nzima bila kuwasahau watumishi wote –HONGERENI SANA na Mwenyezi Mungu awamiminie baraka tele ili mzidi kufanya vizuri zaidi.

Vilevile, nitoe shukrani na pongezi za pekee kwa wadau wote wa Tumaini Media ambao kupitia michango yao ya hali na mali kumewezesha Tumaini Media kusikika Dodoma na maeneo ya jirani kupitia masafa ya 98.1.

Pamoja na kuanza kusikika Dodoma, hakuna mahali pa watumishi wa Tumaini Media kutayarisha na kurusha vipindi hewani vizuri, mathalani ofisi, studio na vitendeakazi, ikiwemo samani za ofisi.

Kupitia ujumbe uliotolewa mwanzoni mwa Juni 2019 kama sehemu ya maadhimisho ya “Moyo Mtakatifu wa Yesu: Msimamizi wa Tumaini Media”; Mkurugenzi wa Tumaini Media alieleza kuwa zinatakiwa Sh milioni 15 kuanzisha ofisi, studio na kupata vifaa muhimu. Kupitia ujumbe huo wadau wanaombwa kuchangia ipasavyo.  Nawapongeza wadau wote kwa moyo huo wa kujitoa ambao ni dalili njema nikiamini kuwa kutoa ni moyo wala si utajiri.

Kwa mahitaji ya ofisi, studio na vitendea kazi kadhaa kiasi kinachohitajika, kwa mtazamo wangu na kwa hali halisi ya maisha ya sasa, naona hakitatosha kukidhi mahitaji hayo. Pengine nikubali kuwa vi vema kuanza kidogo kidogo na kuongeza baadaye. Hata hivyo, nitoe rai kuwa sasa ni wakati muafaka (opportune time) kwa Tumaini Media kufikiria kupanuka kwa lengo la kutoa huduma hizo nchi nzima.

Naiangalia Dodoma kama fursa ya kufanya vizuri zaidi na kwa kiwango cha hali ya juu. Sasa Jiji la Dodoma ni makao makuu ya nchi yetu; kwa mantiki hiyo, Dodoma iwe pia sehemu muhimu ya Tumaini Media kuihudumia Tanzania nzima. Kimsingi, Tumaini Media ina maudhui ya kitaifa kupitia vipindi vyake; kwa hali hiyo huduma zake zinatolewa bila ubaguzi na kutojali imani au itikadi.

Mathalani, vipindi: Hapa na Pale; Jirani Tusalimiane; Afya Zetu na Mikocheni Hospital, Usalama Barabarani; Madikodiko: Jirani; Kutoka Viwanjani, Niko Macho, (Nyimbo/Miziki zilipendwa); miziki mbalimbali, Utamaduni Wetu na Kutetea Uhai (Prolife).

Vilevile, vingine vinavyotarajiwa: Kilimo na Ufugaji na vipindi vya kiroho -Watanzania wengi wanaelimishwa, kuburudishwa, kutoa maoni yao na kusalimiana bila ubaguzi. Hivyo, kupitia Tumaini Media, Kanisa linawezesha jamii kuimarisha umoja wa kitaifa kwa kuhudumia watu wenye imani na itikadi tofauti kama ndugu na kundi moja linaloelewana. Vievile, watumishi wa Tumaini Media wanajitahidi sana kutimiza majukumu yao kwa weledi kwa faida ya taifa letu.

Matumaini yetu ni kuiona Tumaini Media ikichukua sura ya kitaifa badala ya ile ya Jimbo Kuu la Dar es Salaam pekee. Kwa msingi huo, viongozi wakuu na menejimenti waione na waifanye Tumaini Media kama chombo cha kitaifa kwa faida ya wengi.

Hadi sasa kuna majimbo 34 ambayo yanaunganishwa kupitia Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Makao Makuu Kurasini, jijini Dar es Salaam. Kama sikosei baadhi ya majimbo yana vyombo vyake vya habari kama radio na magazeti.

Hata hivyo, itapendeza sana iwapo kitakuwapo chombo chenye maudhui ya kitaifa pengine chini ya Baraza hilo. Kwa mtazamo huo tunapoendelea kuhamasishana kuchangia upanuzi wa Tumaini Media, ni vema lengo likawa zaidi ya kuwa na ofisi na studio ndogo hapo Dodoma. Mtazamo uwe mpana zaidi na kuiona Tumaini Media ikiwa na maudhui ya kitaifa zaidi, kwa mantiki kuwa Dodoma iwe kitovu cha kueneza huduma za Tumaini Media nchi nzima.

Zinapoanzishwa ofisi na studio jijini Dodoma iwe hivyo kwa sasa, lakini tukiwa na mtazamo mpana kwa lengo la kupanua baadaye (think big for the bright future-aiming higher). Serikali imeandaa viwanja vya taasisi mbalimbali, ni vizuri kulitazama hilo ili kupatikane ofa ya kiwanja Dodoma kwa matumizi ya Tumaini Media kuliko kujibanza ndani ya eneo la parokia.

Vilevile, kuandaliwe michoro inayoonyesha matumizi ya eneo kwa mtazamo kuwa Tumaini Media ipo na itadumu miaka mingi na kwa faida ya vizazi na vizazi. Niwaombe wadau na wenye mapenzi mema wachangie kwa maendeleo ya sasa na baadaye.

Masuala mengine, tuwaombe watalaamu waliopo wasaidie mahitaji ya michoro kwa majengo na kupitia Chama cha Wanataaluma wa Kikristo (Christian Professionals of Tanzania-CPT) tuiwezeshe Tumaini Media kusonga mbele. Wataalamu wakitumika vizuri na kwa moyo mkuu watatoa mchango mkubwa kuiendeleza Tumaini Media kwa manufaa ya wengi nchini.

Shilingi milioni 15 kugharamia ofisi, samani, studio na vitendea kazi ziwe ni kianzio, naamini zitahitajika fedha zaidi. Naomba wadau wahamasishwe ili wachangie zaidi (aiming higher). Kwa mtazamo huo naamini Kanisa Katoliki kuwa na chombo madhubuti kwa nchi ni jambo jema sana kuliko kila jimbo kwenda kivyake.

Bora kuwekeza nguvu pamoja na matokeo yatakuwa na manufaa kwa wengi zaidi: kumbuka umoja ni nguvu –Tumaini Media sasa imeingia Dodoma, muhimu ni kuisaidia ikue zaidi kupitia michango ya wadau. Tusiangalie nani katoa fedha nyingi, lakini wakipata wachangiaji wengi hata kama wanachotoa ni kidogo mafanikio yatakuwa makubwa.

Mathalani, kukipatikana watu milioni moja na kila mtu akatoa Sh 200 tu, zitapatikana Sh milioni 200. Kiasi kama hicho kinaweza kuiwezesha tumaini kusonga mbele. Vilevile, uchangiaji uwe endelevu, si kwa kupindi cha muda mfupi tu, bali milango iwe wazi wakati wote.

Dk. Felician Kilahama ni Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri, Misitu Afrika; na msomaji mahiri wa JAMHURI, mwenye makazi yake Dar es Salaam. Anapatikana kwa namba 0783007400.