Aprili 9, mwaka huu Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alitangaza kwamba kuanzia Juni mosi mwaka huu itakuwa ni marufuku kutengeneza, kuingiza, kuuza na kutumia mifuko ya plastiki kwa ajili ya kubebea bidhaa za aina yoyote na matumizi yake yatakoma ifikapo Mei 31.
Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo bungeni jijini Dodoma kwenye Mkutano wa 15 wakati akihitimisha hoja ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2019/2020.
Tangu kutangazwa kwa kampeni hiyo mahususi ambayo imelenga kuhifadhi na kutunza mazingira, vyombo vya habari vimekuwa msitari wa mbele kuwaelimisha wananchi pamoja na kueleza fursa za wajasiriamali kutengeneza mifuko ambayo itakuwa rafiki kwa mazingira huku ikiziba ombwe la mifuko ya plastiki.
Sisi Gazeti la JAMHURI tunachukua fursa hii kuipongeza serikali pamoja na wadau wote muhimu ambao wamehakikisha kwamba zoezi hilo linafanyika kwa ufasaha huku wananchi wakielimishwa na si kuwavizia kuwalima faini endapo watakiuka katazo la serikali.
Wahenga walisema mazoea yana tabu. Ni kweli kwamba wananchi walikwisha kuzoea kutumia mifuko ya plastiki, kuwaondoa katika utaratibu huo si jambo dogo, lakini hadi leo ni Juni 4, tumeshuhudia kwenye maduka ya kisasa (super markets), wananchi wakinunua mifuko ambayo ni rafiki wa mazingira.
Jambo jingine ambalo kwa hakika ni la kujivunia ni namna ambavyo serikali ilitoa fursa kwa viwanda kubadilisha teknolojia, wauzaji kuondoa mzigo uliopo huku Ofisi ya Waziri wa Nchi, Makamu wa Rais, Mazingira na Muungano ikitumia kanuni chini ya Sheria ya Mazingira kulifanya katazo hilo kuwa na nguvu ya kisheria.
Katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki nchini limekuja baada ya kuleta madhara makubwa, ikiwemo vifo vya mifugo kwa kula plastiki, kuziba kwa mifereji, uchafuzi wa mazingira na kushindikana kwa kuozesha taka kwenye vituo vya kukusanya taka.
Operesheni hii ya kuondoa mifuko ya plastiki imekuwa moja ya operesheni zilizofanikiwa, kutokana na uungwana wa watekelezaji kuwashirikisha wadau wote, hasa vyombo vya habari ambavyo vimekuwa na programu ya kueleza madhara ya mifuko ya plastiki na umuhimu wa kuondakana nayo.
Tunawapongeza wote walioshiriki katika operesheni hii ambayo imezingatia utu, huku ikilenga kuwasaidia watengenezaji na wasambazaji wa mifuko kuondoa shehena waliyonayo katika maghala yao.