Juma lililopita tumesikia taarifa za kutisha kwamba wabunge wametembelea Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) iliyopo Makutupora, Dodoma na kuridhishwa na matokeo ya utafiti wa mbegu za GMO, mbegu zinazoundwa kwenye maabara.
Zilifuatiwa na habari kwamba serikali imesimamisha mara moja utafiti wote unaofanywa na TARI na kuagiza kuteketezwa kwa mazao yote yaliyokuwa yakitumika kwa sababu TARI ilitangaza matokeo ya utafiti kabla ya matokeo hayo kuthibitishwa na serikali.
Ni wale ambao tunaamini kuwa usalama wa matumizi wa mbegu na mazao ya GMO bado haujathibitishwa pasipo shaka tulioshtushwa na kauli ya wabunge. Baadhi ya watafiti hawajafurahia uamuzi wa serikali, na sababu inaeleweka. Utafiti ni ujira.
Wanaounga mkono matumizi ya GMO wanaungwa mkono na nguvu ya ushawishi ya kampuni zinazonufaika na bidhaa za GMO. Utafiti wa Graham Brookes na Peter Barfoot unabainisha kuwa mwaka 2012 faida ya biashara hii ulimwenguni ilifikia dola bilioni 18.8 za Marekani, faida ambayo wakulima na kampuni waligawana nusu kwa nusu. Dola bilioni 9.4 kwa kampuni ambazo tunafahamu si nyingi ni pesa nyingi sana.
Kampuni ya Monsanto, kinara wa biashara hii, na ambayo sasa imenunuliwa na kampuni ya Bayer, iliuza bidhaa za dola bilioni 2.7 za Marekani mwaka 2017. Kulinganishwa thamani hiyo na bajeti ya serikali ya Burundi kwa mwaka huo huo yenye thamani ya dola bilioni 7.9 za Marekani kunatoa mwanga wa nguvu ya kampuni hii.
Ungedhani inatosha na hazihitaji msaada wowote. Lakini uzoefu unaonesha kuwa hizi kampuni hutumia kila mbinu kushawishi kubadilishwa sera, sheria, na taratibu ili kulinda maslahi yao ya biashara.
Ndiyo sababu tunaposikia wabunge kusifia matokeo ya tafiti za GMO tunakumbuka matukio ya kampuni kama hizi kutumia mbinu za kila aina kujitengenezea mazingira muafaka ya kuendeleza biashara zao wakati tukiuliza pia ni nani analinda maslahi ya wakulima ambao wanaweza kuathiriwa na matumizi ya GMO.
Nchini Marekani imethibitishwa kuwa wafanyakazi wa zamani wa Monsanto huajiriwa serikalini kusimamia idara ambazo jukumu lake kubwa ni kudhibiti bidhaa na biashara zile zile walizozalisha chini ya Monsanto. Ni ile hadithi ya zamani ambayo hata watoto wa chekechea wanaielewa bila ufafanuzi mkubwa: maajabu ya fisi kuteuliwa kuwa mlinzi wa ghala ya mifupa.
Hawa wameshika nafasi kama washauri, majaji, na watendaji wakuu ambao wameajiriwa kwenye Wizara ya Sheria, Shirika la Chakula na Dawa, na Shirika la Kulinda Mazingira. Hawajatoka kwenye sekta binafsi kwa kukosa ajira; wanahamia serikalini ili kuhakikisha kuwa uamuzi wote mkubwa unalinda maslahi ya mwajiri wao wa zamani.
Hatuwezi kusema kwa uhakika kuwa mbinu zile za Marekani zinatumika pia Tanzania, lakini tunafahamu kuwa fisi hauachi mfupa bila kuupigania. Atapambana hata na simba. Thamani ya biashara hii ni kubwa na haitakuwa ajabu kutarajia kuwa tamko la serikali la kusitisha utafiti wa TARI halitaachwa kushika mizizi.
Upo msukumo mkubwa sana wa kuharakisha kuenezwa kwa matumizi ya bidhaa za GMO kwa madai kuwa bidhaa hizi zitamaliza mara moja tatizo la wadudu waharibifu, zitaongeza uzalishaji, na kuongeza kipato kwa wakulima.
Hayo madai yanapingwa na tafiti zinazoonesha matokeo tofauti. Lakini hata kama tukikubali kuwa haya madai ya faida za GMO ni ya kweli bado tunakabiliwa na athari kubwa ya kukubali kugeuza shughuli ya uzalishaji wa chakula kusimamiwa na mashirika ambayo nia yao kuu ni kuzalisha faida.
Moja ya mbinu ya kujihakikishia faida isiyotetereka ni kuendeleza mikakati ya kuzalisha mbegu ambazo haziwezi kutumika zaidi ya msimu mmoja na zinazolazimisha wakulima kununua mbegu mpya kila msimu. Sambamba na hilo ni kushawishi kutungwa sheria zinazodhibiti au kuzuia matumizi ya mbegu asilia.
Tangu enzi na enzi wakulima wamezoea kutenga mbegu kutokana na mavuno yaliyopita na kuzitumia kwa msimu unaofuata, suala ambalo linaminya ukubwa wa soko na kuminya faida inayosakwa na kampuni hizi.
Kama lipo jambo ambalo linaashiria kugeuka kwa upepo dhidi ya nguvu ya hizi kampuni ni taarifa kuwa kampuni ya Bayer inakabiliwa na kesi zaidi ya 9,000 ambazo zimejitokeza baada ya mahakama ya nchini Marekani kutoa hukumu dhidi ya Monsanto na kumpa ushindi Dewayne Johnson kwa kuugua saratani baada ya kutumia kwa muda mrefu dawa ya kuua wadudu waharibifu, Roundup, iliyotengenezwa na Monsanto na ambayo hutumika sambamba na mimea au mbegu za GMO ambazo zimetengenezwa mahsusi zitumike na Roundup.
Mahakama imeamua kuwa Roundup imesababisha saratani na kuwa Monsanto waliiuza dawa hiyo wakifahamu kuwa inasababisha saratani. Lakini, kama ilivyo faida inapokuwa kipaumbele, afya na maisha ya watu yanakuwa siyo muhimu sana. Madaktari wa Johnson wanatabiri atafariki dunia ifikapo mwaka 2020.
Tamko la serikali ya Tanzania halisimamishi mikakati ya waungaji mkono wa GMO. Linatoa mwanya tu kwao kupanga mikakati mipya ya kutafutwa mbinu mpya ya kufanikisha malengo yao.
Somo ambalo tunalipata kutoka hukumu ya Marekani ni kuwa madhara ya afya yanayohusiana na baadhi ya bidhaa hizi hayajitokezi mara moja ila yanaweza kuchukua muda mrefu kubainika. Ni mtazamo wa muda mrefu tu ambao utaweza kulinda maslahi ya wengi.