Tunaomba kukupongeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Maimuna Tarishi, na baadhi ya wadau kwa kufungua baadhi ya fahamu za Watanzania wazalendo na wanyonge, na huo ndiyo uongozi bora kwa  viongozi wapenda maendeleo ya nchi yao.

Kwa heshima yako kama Mtendaji Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, tunaomba upokee salamu za Watanzania wote wapenda maendeleo waliojitokeza na wanaondelea kujitokeza katika kampeni ya Jitokeze.

Rejea uamsho wako kwa wadau wote wa maliasili na utalii Tanzania  nzima, kama ulivyosema  “Okoa maisha ya tembo kwa kukabiliana na ujangili”

Maimuna tunakuomba kama mabalozi wa maliasili na uhifadhi wa kujitolea kama tulivyokwisha kuzungumza nawe ofisini kwako  Dar es Salaam, mapema Julai na Septemba 8, 2014.

Pokea salamu zetu za kuunga mkono Serikali yetu katika kupambana na janga la ujangili kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii na wadau mbalimbali kama Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Shirikisho la Watoa Huduma kwa Watalii (TATO), AWF, Baraza la Habari Tanzania (MCT), dini zote, TAWIRI, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), vyombo vya ulinzi na usalama, CITES, vyombo vya habari hususani Gazeti JAMHURI kwa kampeni yako ya kuokoa maisha ya wanyamapori kutoka taasisi ya Rafiki Wildlife Foundation.

Kama ulivyoihamasisha jamii ya Kitanzania kwa mujibu wa Sheria ya Wanyamapori Na. 5 ya 2009, sura 283, juu ya ukatili dhidi ya tembo, faru, ndege na kadhalika.

Nasi kama mabalozi wa kujitolea wa kiume na wa kike wa wizara yako, tumehamasika kupitia moja ya kampeni zako kwa kusoma jarida la Kakakuona kama tulivyotaja hapo juu na kwa kushiriki katika jitihada za wadau wengine kama vile TATO mwaka 2013.

Wakati wa uongozi wa aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis  Kagasheki, na aliye waziri mwenye dhamana kwa sasa, Lazaro Nyalandu.

Na hata sasa tunaendelea na kampeni ya Jitokeze, ambayo imekuwa ya mafanikio sana, wadau wengi wamejitokeza zaidi kuiunga mkono Serikali kuhakikisha tunatokomeza kero ya ujangili kwa njia mbalimbali na hata kiibada, hasa wadau wakitoa maoni kuwa elimu ya uhifadhi na wanyamapori ipewe fursa ndani ya jamii ili kusababishwe mwamko wa uhifadhi na kuisaidia Wizara ya Maliasili na Utalii kupata wadau wa ndani yaani mabalozi.

Kwa sasa Rafiki Wildlife Foundation baada ya kuongea na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, na kubahatika pia kuongea na Mkurugenzi mteule wa wanyamapori, Herman Keraryo, tumekusudia kuyafikia maeneo ya baadhi ya mikoa mitatu ambayo ni Arusha, Manyara na Kilimajaro ili kutoa elimu ya uhifadhi na wanyamapori  kukabiliana na janga la ujangili kifursa, hasa jamii na umma kwa ujumla kutambua umuhimu wa uhifadhi na jinsi ya kukabaliana na changamaoto za uelewa mdogo wa jinsi ya kupambana na uharibifu wa mazingira ya wanyamapori wetu.

Tunawaomba wadau mbalimbali kujitokeza pia kutuunga mkono kwa namna yoyote ili kufanikisha shughuli hii kwa haraka, sanjari na hili tuna malengo mengi ambayo tutaendelea kuyazungumzia tupatapo nafasi. Kilio cha wanyamapori wa Tanzania ni janga la Taifa na ukosefu wa maadili.

Kwanini ni janga la Taifa la Tanzania? Ni kwa sababu nyuma ya viumbe hivi adimu vimebeba mambo muhimu ndani ya jamii na hata nje ya jamii, viumbe hivi vimekuwa sababu ya ajira, uwekezaji, uchumi na kwa maendeleo endelevu.

Mfano, jiji letu la Arusha karibu robo tatu ya wakazi wananufaika moja kwa moja na uwepo na matunda ya utalii japo baadhi hawajalitambua hili na baadhi wanapendeza kwa ajili ya viumbe hivi vizuri, wengine wameoa Wazungu na kuolewa na Wazungu, kwa maana nyingi kwa heshima ya wanyamapori tumepata mashemeji na mawifi wa Kizungu.

Kwa sura hii kwanini tusiendelee kujivunia wanyamapori wetu na fahari yetu? Maimuna Tarishi kama ulivyothibitisha kauli yako katika ufunguzi wa mkutano wa wadau uliofanyika katika Manispaa ya Morogoro Juni 10-13, 2013.

Kwa nukuu ya Jarida la Wanyamapori la Kakakuona namba 23 la Aprili-Juni 2013: Tafakari hii iwe sehemu ya mkakati na changamoto tena masikioni mwako na Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na wadau wote waliohudhuria kikao hicho muhimu.

Ulisema na nitanukuu maneno machache. “Lakini mtu anaweza kujiuliza ni nani mhusika mkuu wa ujangili huu? Ni vigumu kulijibu swali hili lakini jangili ni Mtanzania mwenyewe kwa sababu baadhi hujikuta wakitumiwa na watu kutoka nje, na wao bila kujali umuhimu wa rasilimali hii muhimu kwa nchi yetu, huweza kujihusisha na ujangili kwa namna moja au nyingine. Hii inawezekana kwa mtu kujihusisha moja kwa moja kwa yeye kuwaua tembo, au kwa kumficha jangili, au kwa kutoa taarifa za kuwasaidia majangili ili wafanikishe kufanya uhalifu wa kuwaua tembo” mwisho wa kunukuu.

Je, Maimuna Tarishi watu hawa si mfano wa wale wenye kutumia Leseni ya Rais, na huu siyo ukosefu wa maadili ndani wizara, jamii na umma kwa ujumla?                                                                                 Kwa kuwa mmekusudia kujitokeza, naomba mtukubali ili tusije kombea “fito”, tunatamani nia yetu iwe moja kupambana na janga la ujangili. Lakini mkubali kupokea changamoto, maoni mema, japo na mabaya yaweza kutokea hii itawapa kujipima ni kwa jinsi gani mtajua kuwa sasa mna wadau weledi kuliko kubaki kwenye “ziro”.

Mainuma Tarishi, wosia wako huko Morogoro kwa wadau wa uhifadhi na wanyamapori ni “UNABII”, tatizo kubwa kwa  jamii ya Kitanzania, wakubwa kwa wadogo, hatuna elimu wala mwamko wa uelewa wa kutosha kuhusu umuhimu wa wanyamapori na uhifadhi kimazingira.

Kwa sura hii tunaomba kusema hivi kwa Serikali yetu sikivu kuwa elimu ya uhifadhi na wanyamapori ni “NURU” ipewe nafasi kubwa ndani ya jamii na umma kwa ujumla ili kukabiliana na umaskini wa uelewa mdogo kuhusu wanyamapori.

Ukitaka kujua kuwa nchi hii ina “WADAU”, gusa habari ya vyama vya siasa, utaona na jinsi gani watu walivyo tayari kuandamana, au gusa suala la mishahara ya wafanyakazi utaona jinsi gani watu walivyo tayari hata kugoma kwenda kazini na zaidi wapigania haki za binadamu wanavyojitokeza, ni kwa sababu wameelimishwa na wanazijua sera husika na wanacho cha kuhoji na kujihoji.

Lakini suala la uhifadhi wa wanyamapori kukosa “maono” ndani ya jamii na umma linachangia viongozi waadilifu kuvuruga rasilimali zetu, maana wanajua kilicho nyuma ya jamii ni “ziro,” wanajua hakuna wapigania haki za wanyamapori na waliopo wachache ni wale wa “matumbo.”

Kwa jamii na umma kutokujua chochote na ndiyo maana hata hujaona maandamano zaidi ya  wajanja  fulani kwa maslahi ya matumbo yao, ni kweli wajinga ndiyo waliowao. Ila kwa sasa hakuna mjinga tena. Tanzania tunadai haki yetu HONGERA GAZETI JAMHURI, leo na hata milele tuna sababu ya kuhoji kuhusu wanyamapori wetu kwa baadhi ya viongozi wasio waandilifu, isiwe ni kazi ya ‘BUNGE TU’. Leo  wizarani baadhi yao wanapaona kama kituo cha polisi, sina maana kuwa ni watuhumiwa hapana.

Maana wengine kwa uzembe na kutokuisimamia sheria ya uhifadhi na wanyamapori wetu ni sawa na majangili kwa sura ya ustaarabu fulani hivi, baadhi yao wamepata majibu hatuna sababu ya kuwataja majina, hiyo ni kazi ya Ofisi ya Rais Utumishi chini ya komandoo Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue.

Naomba tuwape taarifa majangili porini ni vizuri msalimishe silaha maana dini zote macho ni kwa wanyamapori na Mungu Muumba amekusudia kufanya jambo, tuna imani tembo ataongea. Hakika hatutalala wala kuchoka, maana tuna sababu ya kukemea roho ya ujangili na ni haki yetu kufanya hivyo ikiwa watu wanaomba kwa ajili ya Katiba ya nchi, tuna sababu pia ya kuomba kwa ajili ya wanyamapori wetu.

Neno la Mungu linasema Zaburi 36:6b “Ee Bwana unaokoa wanadamu na wanyama”. Neno la Mungu ni zaidi ya hiyo “helikopita”. Neno la Mungu ni msaada litawasaidia wahifadhi waadilifu na askari pori waadilifu huko porini na hili ni uthibitisho kuwa Mungu anachukia ujangili. Naomba ukasome na Rum 8:19-22.

 

Hongera Ikulu na Ofisi ya Rais Utumishi

 

Lakini tutakuwa hatuna shukurani kama hatutatoa pongezi kubwa za mabadiliko makubwa yaliyofanywa na Ikulu juu ya wizara hii nyeti. Maana msomi huyu na mwanafalsafa safi, jina lake Mtume Paulo kwa uwezo wa Roho Mtakatifu alisema, “Kila mtu na aitii mamlaka inayotawala, kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu, nazo mamlaka zilizopo zimewekwa na Mungu. Kwa hivyo, yeye anayeasi dhidi ya mamlaka inayotawala anaasi dhidi ya kile kilichowekwa na Mungu, nao wale wafanyao hivyo watajiletea hukumu juu yao wenyewe.

Kwa kuwa watawala hawatishi watu wale wanaotenda mema bali wale wanaotenda mabaya. Je, wataka usimwogope mwenye mamlaka? Basi tenda lile lililo jema naye atakusifu.

Ndiyo maana nikasema hongera Ofisi ya Rais Utumishi kwa maana mwenye mamlaka ni mtumishi wa Mungu kwa ajili ya mema. Lakini kama ukitenda mabaya, basi ogopa, kwa kuwa huchukui upanga bila sababu. “Yeye ni mtumishi wa Mungu, mjumbe wa Mungu wa kutekeleza adhabu juu ya watenda mabaya”. Rum 13:1-4.

Hongera Ofisi ya Rais Utumishi na Ikulu yote hongera na hongera Rais wetu, Dkt Jakaya Mrisho Kikwete, hata Biblia yangu ina sababu za kusema kumbe Ikulu ilikuwa “ikisoma ramani”, ama kweli leo tunakumbuka ule msemo wa Baba wa Taifa, aliousema kuwa Ikulu ya Tanzania ni mahali patakatifu na majibu yatokanayo na Ikulu ni lazima yawe matakatifu, nafikiri wote mmeona hayo majibu.

Hongera Gazeti JAMHURI, sasa wahifadhi nanyi hili mmeliona kaeni kwenye madawati huenda macho Ofisi ya Rais Utumishi yakahamia hifadhini, maana ukiona mwezako ananyolewa nywele, basi huenda bwana kinyozi anakusubiri wewe au jicho la kinyozi linakuelekea wewe, hodi hodi TANAPA, NCAA NA NDUGU VITALU, maana huku pia tuna wasiwasi sana.

Karibu Mkurugenzi mpya wa Wanyamapori Tanzania, Herman Keraryo.

Ofisi ya Rais Utumishi, huu ndiyo uamuzi ambao Watanzania wanauhitaji kuuona kwa sura ya nje, ambayo ndani ya mioyo unaweza kuponya majeraha ya Watanzania wanyonge tunaofanyiwa ufisadi kwa kuhujumiwa maliasili zetu hadharani.

Uamuzi huu uliofanywa na Ikulu ni wenye tija na maslahi mbele ya jamii na umma kwa ujumla. Ama kweli Mungu huwainua wanyonge kutoka chini na kuwapandisha juu na huwashusha wenye kiburi chini ili washike adabu.

Hongera mliopata promosheni huko Wizara ya Maliasli na Utalii tukiwa tunawatakia kazi njema na nzuri. Ni vizuri kuwapongeza hata kama baadhi ya wadau njaa watanuna, ila mbingu za Mbingu kwa ajili yenu zimetabasamu, karibu Mkurugenzi mpya wa Idara ya Wanyamapori au kwa kimombo Director of Wildlife Tanzania, Herman Keraryo.

Watanzania tunakuamini, tena baadhi ya sifa zako njema tunazijua kuwa hata mapema hivi karibu umekuwa mstari wa mbele kumshauri vyema rafiki yetu Nyalandu, alipotaka kuongeza vita huko porini kwa kuajiri askari wa Kimarekani.

Kwa ushauri wako mzuri japo ulienda kinyume na matakwa yake tarajiwa ya kutokuona umuhimu wa kuajiri Wamarekani, “wakati vijana wa Kitanzania wanasota mtaani bila ajira kutafuta kazi tena wana uwezo mzuri, na wengine wamemaliza kozi za kivita huko Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), na wanafaa kabisa kuwa askari wa wanyamapori, licha ya kuwa walikuwa wameandaliwa kuwa askari wa kivita si bora waende huko.

Maana sasa wananchi tumejitambua tumetangaza mpango mkakati wa amani kwa makazi ya watu Tanzania nzima, ukitaka kujua hali hii muulize RPC wetu Mkoa wa Arusha, Kamanda SACP Liberatus Sabasi, akisaidiana na kamanda Operesheni, ACP Balele, na kurunzi nzima ya makachero hakuna cha mabomu wala tindikali, wala mauaji ya albino, shida iko kwa wanyamapori wetu huko maporini tukaze msuli.

Kwa wazo hilo, hekima hiyo na busara hizo na uamuzi huo Herman Keraryo Mungu amekuchagua na kwa maombi ya Watanzania wengi kuwa Mkurugenzi wa Wanyamapori Tanzania, wewe ni NUHU NA SAFINA [Mwanzo 7:1-3].

Tumekuamini kwa maana hiyo “kura ya ndiyo” pokea kwa sababu tumekusudia kumwona Mungu akisimamisha viongozi wenye “haki” watakaosimamia rasilimali zetu kwa maslahi ya Watanzania wote wakubwa kwa wadogo, tunakuombea moyo wa utulivu uliosheheni hekima na maarifa.

Mdo 13:22 “Na alipokwisha kumwondoa huyo, “S” alimwinua Daudi awe mfalme wao ambaye alimshuhudia, akisema, Nimemwona Daudi, mwana wa Yese; yaani [Herman mwana wa Keraryo], mtu anayeupendeza moyo wangu, atakayefanya mapenzi yangu yote”. Wizara ya Maliasili na Utalii nimeongeza.

Jiamini kuwa unaweza maana sasa tembo na wenzake huko maporini ni tabasamu tupu, tuko nyuma yako, tuseme nini Bwana akiwa upande wetu (Rum  8:31-39) kwa maombi huku tukiendelea na kampeni ya kuelimishana, kwa pamoja inawezekana Tanzania  kutokomeza roho za ujangili, karibu kwa wanyonge usiishie kwenye hoteli za kifahari. Mnyonge mnyongeni lakini haki yake apewe, ni kauli aliyoipenda Balozi Kagasheki aliyewahi kuwa waziri wa wizara hii.

Tunakukumbuka Balozi Kagasheki, japo mambo ndiyo hivyo tena, kwa leo tunaomba kuitumia kauli yako hii yenye “mashiko” kuwatakia kazi njema wazalendo na wapiganaji na vipenzi vya Watanzania na wadau wa wanyonge na wapenda amani, maprofesa wawili huko waendako Mweka, Kilimajaro na SUA Morogoro uhamishoni, Mungu awe juu yenu Prof. Alexander Songorwa na Prof. Kidegesho, tunawaahidi kuwa tutaukumbuka mchango wenu daima, na kuhodhi maono yenu kwa jamii na umma kwa ujumla, ndiyo maana tukamnukuu bosi wenu wa zamani aliyesema mnyonge mnyongeni lakini haki yake apewe, tunawapenda, tunawaombea dua kwa Mola.

Kazi zenu ni dhahiri hata “Ikulu” ilitambua mchango wenu na ndiyo maana ilitegua ule uamuzi, ila ni mambo madogo tu “USIASA”. Msiwanyime kura mwaka 2015, maana ninyi ni wazalendo na watu wa Mungu wenye misingi ya msamaha ndani ya mioyo yenu, najua watapita majimboni kwenu, japo baadhi si wajibu wenu kunadi sera zao, ila tutawauliza maswali maana wanajisahau wakati mwingine ni kama ile methali isemayo “usimcheke mamba kama bado hujavuka mto,” wanasahau kuwa bado kuna mto wa 2015, na tayari wanajifanya kumcheka mdau mamba.

Msihofu kuwa nje kidogo ya wizara hii si kitu sana, bado ninyi ni watumishi shujaa wa umma na jamii yumkini mwaka wa mabadiliko mnaweza kurudi pale pale, tunauombea uchaguzi 2015 na “KITI” cha Ikulu kiutambue tena mchango wenu msiache kumpa ushirikiano Herman Keraryo na wizara kwa ujumla, tembeeni ule msemo wa kimbingu unaosema usishindwe na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema.

Msisahau kusameheana ili Mungu wa mbinguni naye awasamehe ninyi katika yote.

Ee Mungu ibariki Tanzania, wakumbuke na wanyamapori wetu Tanzania na Afrika kwa ujumla. Ni sisi mabalozi wa kujitolea kuelimisha jamii na umma kujua umuhimu wa uhifadhi na wanyamapori kifursa, ili kukabiliana na changamoto za janga la ujagili Tanzania, chini ya taasisi ya Rafiki Wildlife Foundation ya jijini Arusha.

Kuwa rafiki, sema ndiyo kuwalinda wanyamapori wa Tanzania na Afrika kwa ujumla.