Mtakumbuka kuwa Agosti 10, mwaka huu, siku ya Idd Pili, iliisha vibaya kwa Katibu wa Jumuia na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Ponda Issa Ponda. Siku hiyo katika simu yangu uliingia ujumbe mmoja kutoka kwa watu zaidi 25. Ujumbe huo ulisomeka hivi ‘Sheikh Issa

Ponda amepigwa risasi Morogoro, wataarifu waumini wengine kumuombea na kukemea mashambulizi ya silaha dhidi yake’.

Siku hiyo Sheikh Ponda inasemekana alishambuliwa kwa risasi mara baada ya kutoka kwenye mkutano ambao alihutubia kama mgeni mwalikwa.

 

Kamanda wa Polisi mkoani humo, Faustine Shilogile, alikaririwa na vyombo vya habari akisema kuwa Polisi hawahusiki na tukio la kupigwa risasi kwa Sheikh Ponda. Hata  hivyo, alikiri kuwa polisi wake walifyatua risasi kuwatawanya wafuasi wa Sheikh Ponda waliokuwa wameanza kuleta fujo.

 

Hii kimantiki maana yake ni nini? Maana yake ni kuwa Shilogile anachora mstari wa kuwaondoa Polisi kwenye tuhuma hizo. Anamaanisha kuwa Polisi hawahusiki kabisa na kumjeruhi Sheikh Ponda.

 

Lakini maana nyingine ni kuwa anayetaka kulituhumu Jeshi la Polisi linalolinda usalama wa raia na kudumisha amani, ni sawa na kulipakazia na kulipunguzia imani kwa wananchi ambao wengi bado imani iko juu kwa jeshi hilo kama mchongoma na mawingu yaletayo mvua, hivyo asiaminiwe mtu mwingine yeyote akiwamo Shehe Ponda mwenyewe aliyekuwapo kwenye tukio na hata anayesema kuwa polisi ndiyo wamempiga risasi.

 

Mantiki yangu inahitimisha hivi, ‘Kama unawaamini polisi basi Shilogile yuko sahihi na hivyo humuamini Sheikh Ponda. Kama humuamini Sheikh Ponda basi Ponda anadanganya na endelea kusimika imani yako kwa Jeshi lako tukufu la Polisi.

 

Kwangu mimi naona ni sahihi kabisa jeshi hili kuunda tume ya kujichunguza maana halihusiki na yaliyotokea Morogoro dhidi ya Sheikh Ponda. Wao polisi walifyatua risasi kutawanya wafuasi wa Ponda na hawakumpiga Ponda risasi kama wengi wanavyowasema.

 

Hapa usianze kujiuliza nani walikuwa na risasi siku walipomfuata Ponda maana utakuwa unalituhumu Jeshi la Polisi bila ushahidi, eti tu kwa kuwa wao ndiyo wenye bunduki zenye risasi na eti labda walijisahau na kumfyatulia Sheikh Ponda kwa bahati mbaya.

 

Ingeundwa tume inayowahusisha polisi na kujichunguza wao wenyewe, eti kwanini wawafyatulie risasi wafuasi wa Ponda, hapo ingekuwa sawa kabisa na wala kusingekuwa na nongwa wala kuhoji.

 

Wengi wanajiuliza, kama polisi wanasema hawajamfyatulia risasi Sheikh Ponda ni nani basi atakuwa amemfyatulia risasi? Au kama polisi wanasema hawajamfyatulia risasi  yale majeraha kwenye bega lake ni ya nini na yametokana na nini?

 

Kumbuka kuwa polisi wamesema hawajamfyatulia risasi Ponda bali wamefyatua risasi hewani kutawanya wafuasi wa wake. Ukiamua kuwaza  na kuumiza kichwa  kiasi kwamba unatakiwa kutumia dawa ya kutuliza maumivu kama Panadol, basi unaweza kusema huenda majeraha ya Ponda yakawa yametokana na ajali ya bodaboda.

 

Usafiri huo ndiyo sasa unaoongoza kuumiza watu na kuwaacha na majeraha makubwa kwenye miili yao. Isipokuwa kama unataka kutuliza akili yako na kupata majibu ya nani alimfyatulia risasi Sheikh Ponda, wala huhitaji kumtafuta mwalimu mwenye shahada za chuo kikuu ili akupe majibu, na wala huhitaji kuwa na elimu ya kurusha roketi angani!

 

Jibu ni rahisi sana! Samahani nakuingiza kidogo kwenye siasa maana ndiyo mmeng’enyo wa jibu unakoanzia. Nauliza hivi, kwani kule Arusha bomu lilipolipuka katika mkutano wa chama fulani cha siasa kilipokuwa kinahitimisha kampeni zake tuliambiwaje?

 

Kama utakuwa umesahau nakukumbusha wala sikwambii nipe mji, maana hiki si kitendawili cha tega ni kutege. Baada ya mlipuko wa bomu kule Arusha, tuliambiwa kuwa kile chama kilijilipua na kumuua kiongozi wake na mmoja wa vijana watatu akiwamo ndugu yangu.

 

Amiri Mtoi, tuliyemzika kule kijijini kwetu Mkuzi, Lushoto, eti ili kutafuta huruma za wananchi ili wakichague kwa kura za kishindo kwenye uchaguzi ambao baadaye uliahirishwa na ulipoitishwa tena ni kweli wananchi wa kata zote nne wakakipa chama kile kura za huruma na kikaibuka washindi.

 

Kama hivyo ndivyo basi tukubaliane kuwa hata Ponda pia amejipiga mwenyewe risasi begani, ili kutafuta huruma za wafuasi wake na taasisi anayohudumu ya Shura ya Maimamu nchini.

 

Si unajua kuwa Ponda alishakaa sana jela na alipotoka akagundua kuwa watu hawakumuonea huruma wakati yuko ndani? Ameamua kutafuta huruma kwa kujipiga rasasi  sasa siyo?

 

Ingekuwa tukio hilo limetokea Arusha tungesema labda kwa kuwa kuna kata moja ambayo iko wazi, hivyo huenda wale jamaa wamempiga Ponda ili baadaye uchaguzi ukifanyika wapate tena kura za huruma na kushinda kwa kishindo kama walivyopata kura za huruma kwenye zile kata nne.

 

Lakini kwa kuwa imetokea baada ya mhadhara wa Sikukuu ya Idd Pili, basi huenda baadaye tukasikia hawa hawa waliosema kuwa hawajampiga Sheikh Ponda risasi bali.

 

walifyatua risasi kuwatawanya wafuasi wake, wakisema kuwa Intelijensia imegundua kuwa Sheikh Ponda amejipiga risasi kutafuta huruma za waumini na wafuasi wake, kwa kuwa amekasirika kwa nini Mwezi Mtukufu wa Ramadhani umekwisha mapema.

 

Au Intelijensia imegundua kuwa Sheikh Ponda amejipiga risasi ili kutafuta kuungwa mkono na waumini wake wamchague katika Uchaguzi Mkuu wa Bakwata utakapoitishwa. Mimi nimejifunza kitu kimoja hata wewe pia msomaji wangu unaweza kujifunza kupitia kwangu.

 

Kumekuwa na tabia ya kutuhumu upande wa pili pale kunapokuwa na tatizo lililosababisha madhara upande huo, bila hata kufanya uchunguzi wa kina na wa makini wenye majibu ya uhakika. Kumbuka chama kimoja cha siasa kilipoandamana kule Arusha  Januari 5, 2011 na watu watu kuuawa kwa risasi na wengine zaidi 28 kujeruhiwa.

 

Tume ya haki za binadamu na utawala bora zimewatuhumu wale waliosema kuwa kutokana na sababu za kiintelijensia hakutakuwa na maandamano maana fujo itatokea.  Hawa hawa wamelaumiwa na Tume ya Serikali kwa kukiuka haki za raia na kusababisha mauaji.

 

Kumbuka pia ule mgomo wa madaktari ambao baadaye tulisikia kutekwa na kuteswa kwa kiongozi wake, badala ya kutafuta majibu ya kina na sahihi wakakimbilia kusema kuwa madaktari wanatumiwa na chama pinzani na hivyo hata mgomo wao unaendeshwa na kuratibiwa na viongozi wa chama cha upinzani.  Wakaapa kuwatafuta na kuwawajibisha – hadi leo bila shaka wanawatafuta.

 

Siku hazikuganda baada ya mgomo wa madaktari, walimu nao wakagoma, hayakutafutwa majibu ya kina na makini, zikatoka kauli nyepesi tena. Eti walimu nao wanatumiwa na chama cha upinzani, madai ya walimu na malalamiko yao bado yanaendelea hakuna majawabu mujarabu yaliyotuliza na kuzipa amani nyoyo za walimu.

 

Kule Nyololo mkoani Iringa, alikouawa Mwandishi wa Habari wa Kituo cha Televisheni cha Ten, Daud Mwangosi, tuliambiwa kuwa ni kitu kilichorushwa kama bomu, kama ilivyotokea kwa kitu chenye ncha kali kule Morogoro alipouawa Ally Zona. Ripoti ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ikaja tena na majibu ya kuwalaumu

polisi kwa kusababisha mauaji, tena ikapendekeza aliyekuwa Kamanda wa Polisi mkoani Iringa achukuliwe hatua za kiuwajibikaji.

 

Sijui kama imefanyika lakini amepandishwa cheo na kuletwa Makao Makuu ya Jeshi hilo. Maana yake ni nini? Kuna haja ya kuondokana na huu utaratibu butu wa kutoa majibu mepesi katika masuala mazito, yanayohusu uhai wa raia wetu na hatima za vizazi vyao na hivyo tuanze utaratibu mpya wa kuanza kupata  majibu ya kina na yenye kukidhi haja na hoja kwenye matatizo yanayolikabili Taifa na mtu mmoja mmoja.

 

Hili la Ponda lingeweza kusababisha machafuko kutoka kwa wafuasi wake. Hakuwa na haja ya kumvizia kama kuku ili kumkamata au kumtungua kwa manati, na wala hakukuwa na haja ya kutumia nguvu kubwa ambayo imeleta madhara kama ilivyotokea, na pia hakukuwa na haja ya kukimbilia kusema kuwa Ponda hakupigwa risasi kabla uchunguzi haujabaini hivyo.

 

Uchunguzi wa kina kwanza ungefanyika halafu ndiyo majibu yenye kina kisichoacha mashaka ndiyo yafuate. Hili halihitaji mwekezaji wa Kichina kuja kuingia mikataba na sisi.

 

Tunaweza kuanzia hapa tulipoendelea kujikwaa tujali maisha ya raia wetu kama jinsi wabia wetu wa maendeleo wanavyojali maisha ya raia wao.

 

Wakatabahu.