Kama kuna wakati viongozi na wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wamefaidi usingizi wa pono, itakuwa ni wakati huu.

Kila kukicha tunasoma habari za kiongozi mmoja au mwingine akihama kutoka chama cha upinzani na kujiunga CCM. Wengi wao ni madiwani, lakini tumeshuhudia hata mbunge mmoja kuhama wakati zikiwepo tetesi kuwa wapo wengine watakaoendelea kuhamia CCM.

Inabidi kuangalia sehemu ya historia ya siasa nchini Tanzania baada ya kuanzishwa mfumo wa vyama vingi kubaini nini inaweza kuwa sababu ya mfumuko huu wa wanachama na viongozi wa upinzani kuhamia CCM.

Itikadi za vyama vyote vya siasa, kinadharia, zinatofautiana kama miongozo kwa kiasi fulani. Ni tofauti ambazo zipo kwenye maandiko. Lakini siyo miongozo ambayo inazingatiwa katika uamuzi wa wengi wa wapigakura nyakati za uchaguzi. Na kwa uhakika, siyo miongozo kwa wanachama na viongozi wanaolala makao makuu ya chama kimoja cha siasa leo, na kuamkia kwenye makao makuu ya chama kingine kesho.

Suala kubwa la kimtazamo linalogawanya CCM na vyama vingine ni Muungano, pamoja na msululu wa masuala yanayotokana na tofauti za pande mbili ndani ya Muungano. Zaidi ya hapo, kama uzoefu wa kuongoza Serikali isingekuwa muhimu, siamini kuwa Serikali ambayo ingeongozwa na CUF, CHADEMA, au ACT-Wazalendo ingekuwa tofauti sana kiutekelezaji na Serikali ya CCM.

UKAWA ni suala tofauti, na ndiyo chanzo cha matatizo yanayoikumba kambi ya upinzani kwa sasa. UKAWA hauunganishwi na falsafa yoyote ya msingi zaidi ya kuiondosha CCM madarakani.

CCM walipochukua uamuzi wa kumwondoa Edward Lowassa kwenye orodha ya wagombea urais wake kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2015, baadhi ya viongozi waandamizi wa vyama vya upinzani wakaamua kuwa turufu waliyokuwa wanaisubiri kwa muda mrefu kumaliza ubishi wa kisiasa alikuwa nayo Lowassa na haraka haraka wakampitisha kuwa mgombea wao.

Tamaa ya kuingia Ikulu ikawa ndiyo kipaumbele. Tamaa hiyo ikaunda UKAWA na UKAWA ikadhoofisha misimamo yoyote ya kiitikadi na kimkakati iliyowaongoza wapinzani kabla ya hapo.

Hatua ambayo waliamini ingewaimarisha – ingawa inawezekana iliwaimarisha kipindi kile cha kampeni – mwishowe ndiyo imekuwa iliyowadhoofisha na inayoendelea kuwatafuna hadi sasa kwa matokeo haya ya hama hama kuelekea CCM.

Upinzani wamepata mapigo mawili kwa kumpokea Lowassa. Pigo la kwanza, ambalo nimelitaja kwenye moja ya makala zangu zilizopita ni kwa Watanzania kukosa sauti ya kuaminika ya kukemea ufisadi kutoka kambi ya upinzani.

Iwapo kuna ushawishi wowote wa kisiasa uliyojengeka ndani ya kambi hiyo kabla ya kumpokea Lowassa, basi ushawishi huo uliporomoka sana, na hasa kwa wale wanaoamini kuwa msimamo wa chama cha siasa kupinga ufisadi ni kiapo kwa jamii ambacho hakina mbadala.

Kama tunaafikiana kuwa wanachama na viongozi wa upinzani wanaorudi CCM ni vigeugeu, basi tukubali pia kuwa somo hilo wamejifunza kutokana na mafunzo stadi yaliyotolewa na UKAWA walipomsimamisha Lowassa kuwa mgombea wa urais. Hawa wanaohamia CCM wangeonekana kama wanafunzi wa kutunukiwa zawadi kwa kulielewa somo vyema.

Kwa hali ya kawaida mtuhumiwa wa ufisadi, kama alivyotuhumiwa Lowassa kwa miaka nenda rudi na upande wa upinzani zaidi hata na wana CCM wenzake, hapaswi kupewa nafasi ya kugombea urais halafu ashinde, na tuliyomtuhumu tutumaini kwa dhati kuwa atakuwa msimamizi mzuri wa ajenda yoyote ya kupambana na ufisadi.

Pigo la pili ni matokeo ya kushindwa uchaguzi wa urais. Upinzani walikuwa na silaha nzito za kisiasa kutumia kwenye uchaguzi mkuu dhidi ya wagombea wengi wa CCM, ikiwa ni pamoja na Lowassa kama angeteuliwa na CCM, lakini wakajikuta na silaha nyepesi dhidi ya mgombea aliyeibuka, John Pombe Magufuli.

Aidha, inaelekea pia kuwa upinzani hawakutafakari vyema maana ya athari za kushindwa kwenye uchaguzi kwa mgombea wao, athari ambazo naamini tunaziona sasa.

Naamini wengi wa wale wanaorudi CCM ni ambao waliamini Lowassa angeshinda. Kwenye mazingira ya siasa yanayokosa misingi thabiti ya kiitikadi, kushindwa kwa Lowassa ni mwisho wa ligi kwa wale wenye misimamo miepesi.

Mchezaji yeyote mwenye nia ya kujiendeleza anatafuta kujiandikisha na washindi, au timu inayoelekea kupata ushindi msimu ujao. Haombi usajili kwenye timu inayoshuka daraja. Kama ni mchezaji wetu anayehama si ajabu tutasikitika. Kwenye chama cha siasa kama ni mwanasiasa wetu kinara anahama tuna haki ya kuumizwa na kitendo hicho, hasa pale kinapoongozwa na uamuzi ambao hauonekani kuwa na msimamo wowote unaoweza kutetewa.

Lakini muhimu pia kutafakari hatua kama hizi kuwa ni hatari kwa ufanisi wa mfumo wote wa demokrasia ya vyama vingi. Taifa linajengaje kada ya viongozi ambao kwao kuhama chama ni suala linaloambatana kuhama mwelekeo wa upepo? Inawezekana sana viongozi wa aina hii kushika nafasi za juu kabisa za uongozi na kusambaratisha kabisa maslahi ya Taifa.

Kwa faida ya jamii na yao wenyewe, inawezekana kabisa kujenga hoja kupiga marufuku ya maisha viongozi wa aina hii kushiriki shughuli za siasa.

Lakini pamoja na hitilafu yao, hawa tusiwashangae sana. Tushangae zaidi viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani wanaoshangaa matukio haya. Wao ndiyo walikuwa waasisi wa kuyumbisha misimamo. Walikuwa walimu wazuri waliofundisha kuwa misimamo siyo muhimu, muhimu ni ushindi. Na kwa uhakika wamepata wanafunzi wa mfano.

Pombe hii wameipika wao. Watu wameinywa na imewakolea mpaka wamehamisha uanachama kwingine. Baadhi yetu tunashangaa mpika pombe kulalamika kukimbiwa na wateja wake mwenyewe.