Na Abel Paul wa Jeshi la Polisi,JamhuriMedia,Tunduru
Jeshi la Polisi kupitia kikosi cha kupambana na kuzuia wizi wa mifugo nchini kinawashikilia watuhumiwa 15 waliohusika katika tukio la mauaji ya wafugaji katika kijiji cha Mbatamila Wilaya ya Tunduru Mkoa wa Ruvuma.
Hayo ya yamesemwa leo Septemba 24,2022, na Kamanda wa Polisi Kikosi cha Kuzuia wizi wa mifugo na migogoro ya wakulima na wafugaji nchini Kamishina Msaidizi wa Polisi ACP, Simon Pasua,wakati alipofika Kijiji cha Mbatamila Wilaya Tunduru Mkoa wa Ruvuma.
Amebainisha kuwa jeshi hilo linawashikilia watuhumiwa 15 kwa kosa la mauaji ya vijana wanne wa familia moja katika Kijiji cha Mbatamila na kuwataka wote waliofanya mauaji kujisalimisha Polisi.
Aidha amewataka wakulima na wafugaji kutojichukulia sheria mkononi na badala yake wafuate misingi ya sheria na taratibu katika kutatua changamoto zilizopo.
Sambamba na hilo amewapa pole wananchi waliopoteza ndugu zao ambapo Kamanda Pasua amesema jeshi hilo linaendelea kuwatafuta watuhumiwa wote walio baki ili wafikishwe katika vyombo sheria kujibu tuhuma zinazowakabili.
Pia Kamanda Pasua amesema kuwa jeshi hilo limefanikiwa kukamata mifugo 159 iliyokuwa imeibiwa katika Kijiji cha Mbatamila Wilaya ya Tunduru mkoa wa Ruvuma ambapo amesema jeshi hilo linaendelea kushirikiana na wafugaji na wakulima katika kupambana na uhalifu.
Kwa upande wake Katibu wa Chama cha Wafugaji nchini Prisca Kaponda amesema chama kitaendelea kutoa elimu kwa wafugaji juu ya matumizi bora ya ardhi ili kumaliza migogoro ya wakuliama na wafugaji hapa nchini.
Nao baadhi ya wahanga wa tukio hilo wamelishukuru Jeshi la Polisi kwa jitihada walizochukua za kuwakamata watuhumiwa wa matukio ya mauaji na kukamata mifugo iliyokuwa imeibiwa katika Kijiji cha Mbatamila Wilaya ya Tunduru Mkoa wa Ruvuma na kuliomba Jeshi hilo kuweka nguvu kubwa ili kupata mifugo ambayo haijapatikana.