Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limefanikiwa kukamata kundi la wahalifu wanane wanaotuhumiwa kula njama kwa pamoja na baadae kufanya tukio la kumteka mfanyabiashara, Deogratius Tarimo.

Novemba 11, 2024 eneo la Kiluvya Ubungo, Dar es Salaam lilitokea tukio la kutekwa kwa Tarimo, mfanyabiashara na mkazi wa Kibaha Mkoa wa Pwani.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Disemba 4, 2024 jijini Dar es Salaam, Kamanda Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema wahumiwa hao wamekamatwa kwa nyakati tofauti Dar es salaam, Songea Ruvuma na eneo la Mbingu Mlimba Morogoro.

“Pia lilipatikana gari aina ya Toyota Raum ambayo ilitumiwa wakati wa tukio hilo huku ikitumia namba isiyo halisi T 237 EGE na baada ufuatiliaji namba halisi ya gari hiyo ni T237 ECF,” amesema.

Amewataja watuhumiwa hao kuwa ni
Bato Tweve (32) Bondia na Mkazi wa Kimara Bunyokwa na Songwe Mbozi, Yusuph Abdallah (32) Mkazi wa Mbingu – Mlimba Morogoro, Fredrick Juma, (31), Mkazi wa Kibamba na Nelson Elimusa @ msela, Dereva Tax, (24), Mkazi wa Mbezi Luguluni.

Wengine ni Benk Mwakalebela@tall (40), Mkazi wa Mbezi Makabe na Kyela Ipinda
Rusungo Mbeya, Thomas Mwakagile @ baba Mage (45) Mkazi wa Kinyerezi Bonyokwa na Kyela Ngonga Ndiali Mbeya, Anitha Temba, (27) Mkazi wa Mbezi Mwisho na Isack Mwaifani, @ boxer , Mkazi wa Kimara Tembo Salanga na Bujonde Isanga Kyela Mbeya.

“Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam linaendelea na kazi ya kuzuia vitendo vya kihalifu lakini pia kuwakamata na kutokuwa na huruma kwa watuhumiwa wote
wanaojihusisha na matukio ya kihalifu ikiwa ni pamoja na kuwashughulikia kwa mujibu wa sheria kwa kuwapeleka kwenye mamlaka zingine za haki.

“Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi wote kuendelea kutoa taarifa za kweli ili Jeshi lichukuwe hatua za kisheria kwa watu wanaopanga kufanya matukio ya kihalifu ili washughulikiwe mapema kabla ya matukio,” amesema.