Jeshi la Polisi limemtimua kazi askari wake, Manga Msalaba Kumbi, mwenye namba F. 5421, kwa kile kinachodaiwa ni mwenendo mbaya kazini. Askari huyo alikuwa anafanya kazi mkoani Mwanza.

Uchunguzi wa Gazeti la JAMHURI umebaini kwamba askari huyo alikumbwa na masahibu hayo baada ya kukamata mihadarati inayohusishwa na ‘wakubwa’ ndani ya Jeshi la Polisi.

Akizungumza na Gazeti la JAMHURI, askari huyo amesema tuhuma ambazo zimemwondoa kazini hazina ukweli, huku wakubwa wanaoufahamu ukweli wakigoma kuusema.

Amesema umekuwapo mpango wa kumfukuza kazi, mpango ambao ulianza kuratibiwa tangu siku ambayo alihusika kumkamata mtuhumiwa wa mihadarati, yeye na askari mwenzake.

“Nilianza kutafutiwa namna ya kufukuzwa kazi tangu siku niliyomkamata mtuhumiwa wa mihadarati na kumfikisha kituoni…inaonekana tukio hilo liliwakwaza wakubwa.

“…siku moja askari mwenzangu aliniomba nimsaidie kumfikisha kituoni mtu aliyekuwa akijihusisha na uuzaji wa mihadarati, tulipomfikisha mimi nilikwenda nyumbani kupumzika. Kesho yake nilipokwenda kazini nilishangaa kukamatwa na kuwekwa rumande, kwa maelezo kwamba natuhumiwa kupokea rushwa,” amesema Kumbi.

Amesema baada ya kutolewa rumande alipata barua ya kufukuzwa kazi pasipo kusikilizwa utetezi wake wala kujua kuhusu ushahidi wowote unaoonyesha amehusika katika tuhuma hizo.

Kabla ya tukio la kufukuzwa kazi, kachero huyo amekumbana na misukosuko kadhaa, ikiwa ni pamoja na kuhamishwa vituo vya kazi mara mbili bila kulipwa stahili zake, ilhali mshahara wake ukiwa umezuiwa baada ya uongozi wa juu wa Jeshi la Polisi kuwaandikia Hazina ili kusitisha.

Kumbi mwenye namba F. 5421, kutokana na mambo hayo dhidi yake alilazimika kufungua kesi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza, kesi namba 6 ya mwaka 2017, ambayo katika hukumu iliamuliwa alipwe stahili zake zote, hukumu ambayo hata hivyo Jeshi la Polisi kwa muda sasa halijaitekeleza, licha ya kuwapo kwa makubaliano ya ziada nje ya mahakama kuhusu malipo ya askari huyo.

Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, DCP Ahmed Msangi, ameliambia Gazeti la JAMHURI kuwa mchakato wa kukamilisha suala hilo unaendelea na kwamba, baada ya uchambuzi Jeshi la Polisi lilibaini kasoro kadhaa dhidi ya askari huyo na hatua stahiki za utatuzi zinachukuliwa.

Kwa mujibu wa hati ya hukumu, Jeshi la Polisi linatakiwa kumlipa jumla ya shilingi milioni 26.8 askari wake huyo F. 5421 DC na kwamba, fedha hizo ni jumla ya malimbikizo ya mshahara na gharama za uhamisho pindi alipohamishwa kutoka Kituo cha Polisi Kirumba jijini Mwanza kwenda Kituo cha Polisi Nansio, wilayani Ukerewe.

Chimbuko la sakata hilo

Askari huyo aliajiriwa na Jeshi la Polisi Tanzania mwaka 2003 na kupangiwa kazi Mwanza katika Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Mkoa (RCO).

Mwaka 2012 alihamishiwa Ofisi za Polisi Wilaya ya Ilemela, kituo chake cha kazi kikiwa Polisi Kirumba, lakini Julai mwaka uliofuata (2013) akiwa anaendelea na majukumu yake ya kawaida, alisomewa simu ya uhamisho akitakiwa kwenda Polisi Ukerewe, simu hiyo ilikuwa yenye namba za kumbukumbu MZR/AD.21/Vol.V/90.

Uhamisho huo uliwahusu pia wenzake wengine sita, na kwamba, akiongozwa na nguzo ya utii, alifanya taratibu zote ili kuhamia wilayani Ukerewe, lakini katika hali ya utata hakulipwa stahili zake kwa wakati.

Kutokana na kutolipwa stahili zake za uhamisho kwa wakati, aliendelea kufanya kazi Kituo cha Kirumba, mkoani Mwanza akisubiri malipo hayo.

Takriban miezi mitatu ikiwa imepita, alilipwa fedha za ‘kufunga mizigo’ Sh 387,500, na aliendelea kusubiri malipo mengine ili ahamie kituo kipya cha kazi, huku Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza ikiahidi kushughulikia suala hilo ndani ya muda mfupi.

Licha ya ahadi hiyo, askari huyo hakulipwa na kinyume chake, Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa (Mwanza) iliandika barua kwenda Makao Makuu ya Polisi Dar es Salaam kusitisha mshahara wake na stahili nyingine.

Pamoja na yote hayo, Kumbi, alikwenda kuripoti kituo kipya cha kazi na kupangiwa majukumu mengine akiahidiwa kuwa atalipwa stahili zake pamoja na mishahara yake yote, ahadi ambayo hata hivyo haitimizwa hadi leo.

Akiwa Ukerewe, alipata tena uhamisho kwenda Wilaya ya Magu, safari hii pia hali ikiwa kama ilivyokuwa mwanzo, uhamisho bila malipo yoyote.

Baada ya kuona hali imekuwa tete, kachero huyo alimwandikia barua Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP),  kupitia Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mwanza kutaka kujua hatima ya sakata hilo.

Katika kutaka kujua IGP amejibu nini kuhusu barua aliyomwandikia, askari huyo aliandika kwenda kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Agosti 25, 2015 kuuliza kuhusu majibu ya IGP, lakini pia hakujibiwa chochote.

Baada ya kukabiliana na ugumu wa maisha uliotokana na kunyimwa mshahara, aliomba msaada kutoka Ofisi ya Mkuu wa Polisi Mwanza kupitia kwa Ofisa Mnadhimu (Staff Officer 1), na ofisa huyo aliagiza akopeshwe shilingi 300,000 za Tanzania, na alipowasilisha taarifa (memo) hiyo ya kukopeshwa kwa mhusika aliyetakiwa kutoa mkopo, hakupewa ushirikiano kutokana na kile kinachoelezwa kuwa ‘maelekezo kutoka juu’, hivyo kushindwa kupata msaada huo.

Kilichoendelea

Gazeti hili limeona barua ya mawakili wa askari huyo kwenda kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza ya Januari 8, 2016, ikionya: “Endapo suala hili halitapatiwa ufumbuzi kadiri ifaavyo, maelekezo tuliyonayo kutoka kwa wateja wetu ni kutochagua jambo jingine lolote, bali kufungua shauri mahakamani ili haki itendeke kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizopo.”

Mawakili hao kutoka Kampuni ya uwakili ya Rwelu Attorneys walifungua kesi Mahakama Kuu, kesi namba 6 ya mwaka 2017 na kupata ushindi, mahakama ikielekeza kuwa askari huyo alipwe Sh milioni 17.3 za malimbikizo ya mshahara wake kuanzia Aprili 2014 hadi Oktoba 2016 sawa na miezi 31.

Mbali na kiwango hicho, anatakiwa pia kulipwa jumla ya Sh milioni 7.53 za uhamisho kutoka Kituo cha Polisi Kirumba (Mwanza) kwenda Nansio, Ukerewe, pamoja na jumla ya Sh 2.04 za usumbufu.

Kwa mujibu wa amri ya mahakama, Jeshi la Polisi lilitakiwa kulipa fedha hizo ndani ya siku 30 baada ya hukumu hiyo. Hukumu ilitolewa na Jaji Gerson Mdemu, Oktoba 9, 2018 lakini hadi JAMHURI linaandika habari hii hukumu hiyo haijatekelezwa.

Licha ya kukiri utayari wa kufanya malipo hayo baada ya maelewano mahususi chini ya hati ya makubaliano (deed of settlement) ya Agosti 31, 2018 kati ya askari huyo F. 5421 D/C Manga Msalaba Kumbi, Ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Inspekta Jenerali wa Polisi na Mwanasheria Mkuu, askari huyo bado hajalipwa stahili zake.

Chanzo cha kuchelewa kwa malipo ya askari huyo hakijajulikana na jeshi lenyewe halijatoa sababu za msingi mbele ya mahakama wala kumpa taarifa mhusika kwa nini halitekelezi agizo hilo la mahakama.

Hata hivyo, katika barua iliyoonwa na JAMHURI kwenda Ofisi ya Inspekta Jenerali wa Polisi Novemba 22, 2016 yenye namba ya kumbukumbu PHQ/PF/F.5421/33, kupitia kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, askari huyo alifukuzwa kazi kwa fedheha.

Askari huyo ambaye kwa sasa ni raia, amedai kuwa chanzo cha kufukuzwa kazi si tuhuma za kuhusika katika rushwa ya shilingi 500,000 kama inavyodaiwa, bali ni mizengwe aliyofanyiwa na wakubwa wake kazini.

“Sikuwa peke yangu niliyepata simu ya uhamisho. Mimi na wenzangu hatukulipwa stahili zetu kwa wakati. Ilinilazimu niendelee kufanya kazi katika Kituo cha Kirumba nikingojea stahili zangu kabla ya kuhamia kituo kipya,” amesema na kuongeza: “Hata baada ya kuhamia kituo hicho kipya sikulipwa, lakini walinihamisha tena kutoka Ukerewe kwenda Magu pasipo kuwa na mshahara, posho wala malipo ya stahili nyingine.”

Ameeleza kuwa, kutokana na hali hiyo alilazimika kulishitaki Jeshi la Polisi mahakamani na kushinda kesi ili alipwe stahili zake zote.

Katika kuhakikisha kachero huyo anatendewa haki kwa mujibu wa hukumu ya mahakama na maridhiano kati ya pande zinazohusika kwenye kesi hiyo, Naibu Msajili wa Mahakama, O.H. Kingwele, Januari Mosi, mwaka huu, aliagiza uamuzi wa Mahakama Kuu utekelezwe kwa kumlipa askari huyo shilingi 21,382,380.

Agizo hilo lilielekezwa kwa Katibu Mkuu wa Hazina, ambayo ndiyo ofisi iliyositisha mshahara wake kutokana na taarifa kutoka Jeshi la Polisi.

Kwa upande wake, DCP Msangi, amesema utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa kuhusu suala hilo utafanyika kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa kati ya pande zote, yaani upande wa askari huyo na upande wa mamlaka za Jeshi la Polisi na serikali kwa ujumla.

“Tulibaini kuwapo kwa kasoro fulani na ndiyo maana tuliomba suala hili tulitafutie ufumbuzi nje ya mahakama, na kuna makubaliano ya nje ya mahakama. Utekelezaji wa namna ya kuhitimisha suala hili unafanyika … unajua fedha ya serikali ni lazima itoke kwa utaratibu wake.

“Tutalimaliza na kimsingi, hakuna mvutano au mvurugano kati ya askari huyu na Jeshi la Polisi, kila hatua inakwenda vizuri bila mikwaruzano katika kuhitimisha suala hili,” amesema DCP Msangi alipozungumza na Gazeti la JAMHURI.