Vyombo vya habari vimeandika na kutangaza juu ya matumizi ya nguvu yanayofanywa na polisi na vyombo vingine vya usalama nchini. Wadau mbalimbali wamejitokeza kulaani kifo cha mwandishi Daudi Mwangosi ambacho tunadiriki kusema wazi kwamba kimesababishwa na bomu lililofyatuliwa na mmoja wa polisi.
Kama kweli Polisi ni wasikivu, bila shaka kwa tukio hili la aibu na fedheha lililotokea hivi karibuni katika Kijiji cha Nyololo, Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa, litakuwa funzo kwa wengine. Tunamlilia Mwangosi kwa sababu inawezekana habari zake zimetangazwa mno. Inawezekana kama angelikuwa mtu wa kawaida, kama yule ambaye polisi walimuua mkoani Morogoro, asingeweza kupata kuandikwa na kutangazwa kwa kiwango tulichokishuhudia.
Tunachotaka kusema hapa ni kwamba kuna idadi kubwa mno ya Watanzania wanaouawa au kupata vilema vya kudumu kwa staili hii hii ya Mwangosi. Tatizo la polisi kutumia zaidi maguvu bila akili ni kubwa mno kuliko tunavyodhani. Bado tuna kumbukumbu za Watanzania wenzetu waliouawa katika Msitu wa Pande mkoani Dar es Salaam, lakini mwisho wake ukawa watuhumiwa kuachiwa. Hata yule ambaye ushahidi ulimtaja kwamba ndiye aliyetoa amri ya kuua, aliachiwa. Kwa hakika damu ya watu wasiyo na hatia inapopuuzwa, nchi haiwezi kutulia.
Watu wengi wameuawa katika matukio ambayo polisi wamekuwa wakiyaita ya “kujibizana risasi na majambazi”. Mara kadhaa madai hayo yamekuwa ni ya uongo. Tumefika mahali ambako wananchi wasiyo na hatia wanaogopa kuwakaribia polisi kwa sababu wanajua hawatakuwa salama.
Kwenye maandamano na mikusanyiko ambako watu wameuawa, mara zote wachokozi wamekuwa ni polisi. Ukweli ndiyo huo, ingawa propaganda za kisiasa zinaelekeza lawama kwa Chadema ambao hawana hata bisibisi.
Wiki iliyopita, Waislamu waliandamana jijini Dar es Salaam bila kibali. Polisi walitumia busara kuwasindikiza na kusikiliza kilio chao. Tujiulize, kama polisi wasio na busara wangethubutu kutumia mabomu kuwatawanya, ni maafa kiasi gani yangetokea? Baada ya kuwaacha wawasilishe kilio chao kwa amani, kuna aliyejeruhiwa au kuuawa? Kumbe ni kweli polisi ndiyo wachokozi.
Je, sasa tufanye nini? Tunapendekeza haya. Mosi, Jeshi la Polisi lifumuliwe. Pili, somo la haki za binadamu litolewe vyuoni na kazini ili polisi wajue wajibu wao. Tatu, uchukuaji vijana wanaojiunga Polisi utazamwe upya. Utaratibu wa kupeana kazi kwa sababu ni vijana wa “line” ukomeshwe. Nne, utaratibu wa kufanya “vetting” kwa vijana urejeshwe haraka.
Tano, Polisi wapimwe mara kwa mara ili kutambua wavuta bangi. Sita, kazi ya upolisi ni kazi nyeti na muhimu sana, hivyo isifanywe kuwa ni kazi ya waliokosa kazi. Saba, polisi kumtanguliza Mungu ni jambo la maana. Kumcha Mungu ni chanzo cha maarifa, tena ni jambo lenye thamani, hekima na busara.
Nane, maofisa wa polisi wanaotuhumiwa kuwatuma walio chini yao kufanya uhalifu na kupokea rushwa ili wawapelekee, wachunguzwe na kuchukuliwa hatua.
Tisa, kila polisi anayeua atambue kuwa atakabiliwa na kosa la mauaji hadi hapo Mahakama itakapojiridhisha vinginevyo.
Kumi, polisi warejee kwenye miiko ya kazi inayowataka wawe wanajeruhi watuhumiwa, na si kuwaua kama ilivyo sasa. Matatizo ndani ya Polisi ni suala mtambuka. Sote tushiriki kuyaainisha na kuyashughulikia. Mungu Ibariki Tanzania, Mungu warehemu wote ambao uhai wao umeishia mikononi kwa polisi wasio na huruma.
.