Na Isri Mohamed
Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa limethibitisha kifo cha cha katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Kilolo, Christian Nimrod Nindi (56), kilichotokea usiku wa kuamkia leo baada ya kupigwa na risasi akiwa nyumbani kwake kitongoji cha Banawanu, Kijiji cha Ugwachanya Kata ya Mseke.
Akizungumza na wanahabari, Kamanda wa Polisi mkoani humo, SACP Allan Bukumbi
amesema marehemu alivamiwa na watu watatu wasiofahamika akiwa nyumbani kwake na mabinti zake wawili, ambapo walimpiga risasi yeye, kumshambulia binti yake mmoja aliyekuwa akijaribu kumtetea mama yake na kumuumiza maeneo ya usoni na kumjeruhi jirani sehemu ya ubavu aliyekimbilia kwenda kutoa msaada baada ya kusikia kelele.
Baada ya watu hao kutekeleza tukio hilo walikimbia bila kuchukua wala kuacha chochote, ambapo Christina alikimbizwa katika Hospitali ya Tosamaganga na kufariki dunia akiwa anapatiwa matibabu.
Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi ili kuwabaini watuhumiwa ambapo limetoa wito kwa wananchi kwa yeyote mwenye taarifa inayohusiana na tukio hilo kuziwasilisha kituoni.