Askari wa Jeshi la Polisi, mgambo na baadhi ya maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wanatajwa kutumiwa na genge la wafanyabiashara wa mahindi kuwezesha usafirishaji mahindi kwa njia za panya kwenda nchi jirani ya Kenya, uchunguzi wa JAMHURI umebaini.
Magari yote yanayovuka mpaka wa Tanzania kwenda Kenya yamekuwa yakivuka kwa usaidizi wa askari polisi waliopo katika vituo vya polisi vya Himo, Holili, Mkuu, Tarakea, Sanya Juu, Ngarenairobi na Mwanga.
Wakuu wa vituo vya polisi wanatajwa kuwa waratibu wakuu wa biashara hiyo, ambapo wasaidizi wao pamoja na askari wa vyeo vya kati kwenye vituo hivyo kwa kushirikiana na madalali wanaotajwa kuwa na nguvu kubwa kuliko wenye mali.
Mbali na askari hao, baadhi ya maofisa wa TRA ambao usiku kucha wamekuwa wakifanya doria za kukabiliana na wasafirishaji na waingizaji wa bidhaa za magendo kutoka nchini Kenya huku wakiwa na askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), nao wanatajwa kuhusika na biashara hiyo iliyopigwa marufuku na serikali.
Magari 120 aina ya Scania yenye uzito wa tani 15 na magari aina ya Mitsubishi Fuso yanashikiliwa mkoani Kilimanjaro katika Wilaya za Siha, Moshi Vijijini na Rombo yakidaiwa kuvusha mahindi kwenda nchini Kenya.
Kukamatwa kwa magari hayo yaliyosheheni mahindi kunatokana na agizo lililotolewa wiki iliyopita na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kupiga marufuku mahindi, sukari na nafaka nyingine kusafirishwa kwenda nje ya nchi.
Mahindi yanayoingizwa nchini kutokea nchi ya Zambia hupitia mpaka wa Tunduma uliopo Wilaya ya Momba Mkoa mpya wa Songwe na kupakiwa kwenye magari ya Tanzania kabla ya kusafirishwa hadi Mkoani Kilimanjaro tayari kupelekwa nchini Kenya.
Uchunguzi wa JAMHURI umebaini mahindi yanayoingizwa nchini kutoka nchi jirani ya Malawi hupitishwa mpaka wa Kasumulo uliopo Wilaya ya Kyela, Mkoa wa Mbeya kabla ya kusafirishwa hadi Kilimanjaro.
Katika salamu za Baraza la Eid El Fitri ambayo kitaifa ilifanyika mkoani Kilimanjaro, akiwa katika msikiti wa Riadha mjini Moshi, Waziri Mkuu Majaliwa aliagiza kutaifishwa kwa mahindi na magari yote yatakayokamatwa yakisafirisha mahindi kwenda nje ya nchi.
“Naomba mnisikilize vizuri, kuanzia leo (June 26) ni marufuku kwa yeyote kusafirisha chakula kwenda nje ya nchi bila vibali na vibali ni vya kusaga na kusafirisha unga na sio mahindi,” alisema Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu alikiri kuwa na taarifa za baadhi ya maofisa wa polisi kujihusisha na biashara hiyo kwa kushirikiana na genge la wafanyabiashara wanaovusha mahindi kwenda nje ya nchi.
Waziri Mkuu amemwagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hassan Issah kufuatilia nyendo za askari wake na akigundua wapo wanaojihusisha na biashara hiyo achukue hatua za kinidhamu.
Agizo hilo liliwazindua polisi wakakamata magari 103 maeneo ya njia panda eneo lililopo ndani ya Mamlaka ya Mji Mdogo wa Himo.
Eneo hilo la njiapanda ndiyo kitovu cha biashara ya magendo pia hutumika kwa ajili ya kuficha mahindi kabla ya kuyasafrisha usiku kupitia barabara za Himo-Holili, Mwika –Kiracha, Himo-Tarakea, Himo-Makuyuni hadi eneo la Masaini kabla ya kuingia eneo la Kitobo nchini Kenya.

Njia nyingine zinazotumika kusafirisha mahindi kwenda nchini Kenya ni kutoka Moshi hadi Mji wa Bomang’ombe uliopo Wilaya ya Hai kabla ya kuelekea Wilaya ya Siha ambapo husafirishwa kupitia West Kilimanjaro kabla ya kuingia nchini Kenya kupitia eneo la Kamwanga.
Wafanyabiashara wanaotumia njia hiyo ya West Kilimanjaro, wamekuwa wakidanganya kuwa mahindi hayo yanasafirishwa kwenda Arusha hivyo kukwepa kukamatwa na polisi, lakini wanapofika katika Mji wa Bomang’ombe huelekea Sanya Juu Wilaya ya Siha kabla ya kuyavusha kwenda nchini Kenya.
Meneja wa TRA, Mkoa wa Kilimanjaro, Philip Kimune amesema tatizo linaloukabili Mkoa wa Kilimanjaro ni kuwa kuna njia za panya nyingi na ni vigumu kuzidhibiti.
Afisa wa Forodha wa TRA katika mpaka wa Holili aliyefahamika kwa jina moja la Obeid, amesema wafanyabiashara wanatumia teknolojia kukikwepa kikosi kazi.
“Teknolojia ya mawasiliano inafanya ugumu wa kuwadhibiti hao jamaa kwani wanawasiliana kwa njia ya simu na kutukwepa sisi wa TRA,” amesema na kuongeza kuwa bado Mamlaka inafanya kazi kwa nguvu kudhibiti hali hiyo.
Mkurugenzi wa Idara ya Elimu na Huduma kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo ameliambia JAMHURI kwamba ofisi yake haijapata taarifa hizo kwa sababu wafanyabiashara wanaosafirisha mazao kwenda nchi hiyo hawalipi kodi hivyo ni vigumu kupata taarifa za aina hiyo.
Kayombo amesema iwapo watapewa taarifa kamili ikiwa ni pamoja na wahusika halisi anaweza kuzungumzia hilo, lakini kwa sasa hawezi kusema lolote kutokana na jambo lenyewe kuwa geni.
“Labda tupewe taarifa kiundani tuzifanyie kazi,” amesema Kayombo.

Polisi, Mgambo wanavyopiga pesa
Polisi katika vituo vya Himo, Holili, Tarakea, Mkuu, Sanya Juu na Mwanga, na mgambo waliopo katika Kata ya Makuyuni na Kileo Wilaya ya Mwanga wamekuwa wakiingiza mamilioni ya fedha kutokana na kuruhusu mahindi kwenda nchini Kenya.
JAMHURI limebaini kuwa, kila gari moja aina ya Mitsubishi Fuso lililosheheni mahindi hutozwa kiasi cha sh 200,000 na zaidi kabla ya kuruhusiwa kuvuka mpaka na mgao wa fedha hizo hutolewa kwa maofisa hao kulingana na ushiriki wao.
Wastani wa magari 20 hadi 50 aina ya Mitsubishi Fuso huvuka mpaka kila siku kwenda nchini Kenya baada ya kupewa ‘line’ na polisi walioko katika vituo husika pamoja na askari wa doria walioko mipakani.
Baada ya askari hao kutoa maelekezo ya njia za kupita kwa wafanyabiashara. Askari hao huondoka kwenye maeneo waliyoweka doria na kuhamia maeneo mengine kwa lengo la kufanikisha biashara hiyo haramu.
Ushiriki wa askari na mgambo waliopo maeneo ya Himo, Makuyuni, Kileo na Mnoa, Wilaya ya Mwanga katika biashara hiyo unatajwa kuwawezesha kuwa na ukwasi wa kutisha ambao hauendani na kipato chao.
JAMHURI limefanya mahojiano na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Kamishna Msaidizi wa Polisi, (ACP) Hamisi Issah ambaye amesema ni vigumu kwake kukataa kwamba mambo hayo hayafanyiki wakati magari yanapita na kuvuka mpaka wa nchi.
Amesema yeye binafsi ni mgeni katika mkoa huo, lakini ofisi yake tayari imeanza uchunguzi kuhusiana na tuhuma hizo kubaini askari wanaohusika na mtandao huo wa uhalifu.
“Hapa inabidi kuangalia uhalifu wa mtu mmoja mmoja. Na kwa kuanzia ili kuondoa hiki kinachoendelea tunabanana wakubwa wenye vyeo ambao wanasimamia. Tunataka kuliweka hili suala sawa na endapo kama kuna mtu atabainika wa aina hiyo hatua zitachukuliwa dhidi yake.

“Tatizo kuna watu ambao wamekaa huku miaka mingi wanajuana, lakini kama kuna mtu amewekwa sehemu halafu sehemu hiyo ina tatizo naye atakuwa miongoni mwa tatizo.”
“Kama kuna watu walizoea kufanya kazi kwa mazoea sio sasa, askari wetu ni walinzi wa mipaka hivyo ni lazima watimize wajibu wao ipasavyo. Kuna watu ambao wana jukumu la kuzuia pale. Kwa sasa tuko katika jukumu la kuchunguza ni akina nani ambao wanajihusisha na kushirikiana na hawa watu wengine kufanya hivyo,” amesema ACP Issah.
Amesema ni jukumu la wakuu wa vituo na askari kujitafakari kama eneo lake linatuhumiwa na tangu tamko litolewe na serikali kazi iliyofanyika hakuna mtu aliyejaribu kuruhusu kufanyika magendo.
“Tatizo hili suala watu wanajuana kwani wapo huku miaka mingi na matukio haya miaka mingi yanatokea, lakini kwa vile tamko limetolewa hivyo ni lazima kuhakikisha linazingatiwa na kuacha kufanyakazi kwa mazoea yaliyokuwepo,” amesema ACP Issah.

Tamko la Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro
Wiki iliyopita, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwila, aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kutoa msimamo wa Serikali juu ya usafirishaji wa mahindi, mchele, mpunga, sukari na unga kwenda nje ya nchi.
Katika mkutano huo, mkuu huyo wa mkoa alisema ni marufuku wafanyabiashara wa sukari na mazao ya nafaka kusafirisha bidhaa hizo kwenda nje ya nchi bila kibali cha Serikali.
Alisema watakaofanya hivyo watakuwa wametenda kosa la jinai linaoangukia kwenye makosa ya uhujumu uchumi na pia kukiuka agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kupitia waraka wake wa Mei 30 mwaka huu na maelekezo yake ya Juni 26 mwaka huu.
“Ofisi yangu imejiridhisha kuwa baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakisafrisha sukari na nafaka hizo nyakati za usiku kupitia njia ambazo si rasmi kwa kushirikiana na baadhi ya askari polisi ambao siyo waaminifu,” anasema Mkuu wa Mkoa.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa, wafanyabiashara hao wamekuwa wakitoa taarifa kuwa wanayo maghala ya chakula katika maeneo yanayopakana na nchi jirani ya Kenya taarifa ambazo si za kweli.
Amehoji shehena ya mahindi iliyokamatwa Wilaya ya Siha kusafirishwa nyakati za usiku kwa kupitia njia ya vumbi kutoka Moshi kwenda Tarakea kupitia West Kilimanjaro badala ya kupitia Himo, Mkuu hadi Tarakea ambayo ni njia fupi na yenye lami.

Hali ya chakula Mkoa wa Kilimanjaro
Akitoa taarifa ya hali ya chakula katika Mkoa wa Kilimanjaro na bei ya mahindi Wilaya za Rombo na Siha ambako shehena hizo za mahindi zimekuwa zikipitishwa amesema ni ya kuridhisha.
Amesema kwamba Mkoa wa Kilimanjaro hauna uhaba wa chakula bali una ziada ya tani 62,468 za wanga na tani 4,522, za protini huku Wilaya ya Rombo ikiwa na ziada ya chakula tani 14,648 za wanga na tani 8,000 za protini.
Taarifa hiyo inafafanua kuwa, bei ya gunia la mahindi katika Wilaya ya Rombo linauzwa kati ya Sh 75,000 hadi Sh 80,000 ikilinganishwa na Wilaya ya Siha ambako gunia moja la mahindi linauzwa kati ya Sh 105,000 hadi Sh 120,000.
“Ni matarajio yetu kuwa wafanyabiashara halali wanatarajiwa kusafirisha mahindi kwenda Siha na Moshi kuliko Rombo ambako bei ya mahindi iko chini, hata hivyo yapo maeneo ndani ya nchi yenye uhitaji mkubwa wa mazao ya nafaka,” inaeleza taarifa hiyo.

Agizo la Waziri Mkuu
Katika kutekekeza agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro ametoa maagizo sita ikiwamo kupiga marufuku usafirishaji wa sukari, mahindi, mchele, mpunga na unga wa mahindi nyakati za usiku.
Mwananchi yeyote au mfanyabiashara yeyote atakayekamatwa akisafirisha mazao hayo pamoja na sukari atachukuliwa hatua kulingana na sheria ya uhujumu uchumi huku mazao na magari yakitaifishwa.
Amewaonya askari polisi wanaojihusisha na shughuli za usindikizaji pamoja na kupanga njia za kusafirisha mazao hayo kuwa wanatakiwa kuacha tabia hiyo mara moja au kuondoka ndani ya Jeshi la Polisi kabla hawajachukuliwa hatua za kisheria.
Amewaomba wananchi wenye taarifa juu ya biashara hiyo aliyoiita haramu kutoa ushirikiano kwa vyombo vya ulinzi na usalama na kuagiza idara ya uhamiaji kuwasaka wageni wanaonunua mazao ya wananchi yakiwa mashambani.
Pia ametoa tahadhari kwa wakulima kuacha kuuza mazao yao yakiwa shambani na kuwaomba wawe na subira na kuuza mazao yao kwa bei nzuri na kwa vipimo vilivyodhibitishwa.

Maficho ya mahindi
Mkuu wa Mkoa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wameshuhudia shehena ya mahindi iliyokuwa imefichwa kwenye vituo vya mafuta eneo la njiapanda ya Himo kabla ya kusafirihwa kwenda nchi jirani ya Kenya kwa njia za panya.
Mahindi hayo yalifichwa nyuma ya vituo vya mafuta vya ORYX, Oil Alliance, MT Meru na kituo cha mafuta cha Munio. Pia Kamati hiyo ikashuhudia magari manane aina ya Scania yenye uzito wa tani 15 kila moja yakiwa yamefichwa vichakani na kwenye nyumba ya kulala wageni ya Safari Park.
Wafanyabiashara wamegeuza nyumba za kulala wageni na nyumba za makazi kuwa ni maficho ya mahindi katika Mji wa Himo, Njiapanda, Tarakea, Sanya Juu na Kileo kabla ya kuyasafrisha usiku wa manane kwenda nchini Kenya.
Wafanyabiashara hao wamekuwa wakitumia kigezo cha kupeleka mahindi katika Soko la Kimataifa la Nafaka katika Mji wa Himo, lakini JAMHURI limebaini kuwa hakuna magari makubwa yanayofika katika soko hilo yakiwa na mahindi zaidi ya magari madogo aina ya Toyota Pick-Up kutoka kwa wafanyabiashara wa kawaida na wakulima wadogo.

KENYA
Wakati wafanyabiashara hao wakimdanganya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira kuwa Kenya haina uhaba wa chakula, imebainika kuwa serikali ya Zambia imekubali kuiuzia Kenya tani 55,000 za mahindi.
Kenya inakabiliwa na uhaba mkubwa wa unga na kwa muda mrefu imekuwa ikinunua mahindi kutoka Tanzania na nchi za Uganda, Malawi na Mexco japo kwa hapa nchini mahindi hayo yamekuwa yakivushwa kwa njia za panya.
Kwa sasa Serikali ya Kenya ipo katika mazunguzo na Serikali ya Tanzania ikiomba ifungue mipaka yake kuruhusu mahindi yapitie nchini. Hii inatokana na msimamo wa serikali kuzuia mahindi kusafirishwa kwenda Kenya.
Mkurugenzi wa Mazao katika Wizara ya Kilimo nchini Kenya, Johnson Irungu amekaririwa na gazeti la The East African akidai kuwa ikiwa mwafaka hautafikiwa mahindi hayo yanaweza kusafirishwa kupitia nchi za Rwanda na Uganda ambako ni mbali ikilinganishwa na Tanzania.
Pamoja na Zambia kukubali kuiuzia Kenya mahindi hayo, changamoto kubwa ni namna ya kuyafikishwa nchini humo kutokana na msimamo wa Serikali ya Tanzania kuzuia mahindi kwenda nchini Kenya.
Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majliwa amesema hatua ya kuzuia mahindi kusafirishwa kwenda nje ya nchi ni hatua muhimu ya serikali katika kuwalinda wananchi na tishio la baa la njaa siku za usoni.

NA CHARLES NDAGULLA