Na Mwandishi Wetu Jamhuri
Jeshi la Polisi Mkoani Arusha kupitia mtandao wa Polisi wanawake leo Machi 08, 2023 katika kusherehekea siku ya wanawake duniani wamewakumbuka askari ambao waliumia wakati wakitekeleza majukumu yao ya kazi kwa kwa kuwapa misaada ikiwemo fedha.
Akiongoza zoezi hilo lililofanyika katika Zahanati ya Polisi Arusha Afisa Mnadhimu wa Jeshi hilo Mkoani Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Edith Swebe amesema wameamua kusherehekea siku hiyo kwa kuwakumbuka wateja wa ndani ambao ni Askari ambao waliumia kazini wakati wakitekeleza majukumu mbalimbali ya kazi.
Kamishna Msaidizi Swebe amefafanua kuwa mara nyingi huwa wanatoa misaada sehemu mbalimbali ikiwemo vituo vya yatima lakini kwa mwaka huu wakaona ni vyema kuwakumbuka Askari Polisi wagonjwa ambao wamelazwa hospitalini na wengine kuugulia nyumbani.
ACP Swebe amebainisha kuwa kupitia maadhimisho hayo pamoja na mambo mengine, mtandao huo umetoa elimu ya ukatili maeneo mbalimbali ikiwemo shuleni, hospitalini, stendi za mabasi na makundi mengine katika jamii lengo likiwa ni kukomesha vitendo vya ukatili wa kijinsia katika jamii.
Naye Bi. Mwanaisha Ramadhani kwa niaba ya Askari waliopewa msaada huo ameushukuru mtandao huo wa Polisi kwa moyo huo wa upendo walio uonesha kwa kuwakumbuka wagonjwa.
Kabla ya tukio hilo, mtandao huo wa polisi wanawake uliungana na wanawake wengine Mkoa wa Arusha kusherehekea kilele hicho cha siku ya wanawake duniani kwa kufanya maandamano katika mitaa mbalimbali ya Jiji la Arusha.