*Amri yake ya mwaka 2006 yaota mbawa
Jeshi la Polisi limepuuza agizo halali la Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Rais Jakaya Kikwete, lililolitaka lihakikishe linawasomesha watoto watatu wa askari polisi, PC Abdallah Marwa.
PC Abdallah aliuawa wakati akipambana na majambazi katika tukio lililofanyika eneo la Ubungo Mataa jijini Dar es Salaam, Aprili, 2006.
Rais Kikwete, akiwa amemtembelea mmoja wa askari na raia waliojeruhiwa katika tukio hilo waliokuwa wamelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), aliagiza watoto wa PC Abdallah wasomeshwe, na pia polisi waliohusika kwenye mapambano hayo wapandishwe vyeo. Rais alifanya ziara hiyo Aprili 23, 2006.
Katika mapambano hayo, Sh milioni 150 ziliporwa huku polisi wakifanikiwa kuokoa Sh milioni 850. Fedha hizo mali ya Benki ya Makabwela, NMB, zilikuwa zinapelekwa katika Tawi la Wami, Morogoro.
Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Solomon Adam aliyekuwa na cheo cha koplo, alionesha ushujaa wa hali ya juu kwa kuchukua bunduki na kupambana na majambazi hao.
Rais Kikwete akiwa Muhimbili, alisema, “Namuagiza IGP ampandishe cheo trafiki aliyejitoa muhanga kusimama mstari wa mbele kuwasaidia wenzake katika mapambano dhidi ya majambazi, pia awapandishe vyeo askari wote walioshiriki katika mapambano hayo.
“Nampongeza askari polisi aliyeuawa katika mapambano hayo. Amekufa kishujaa, Serikali inachukua jukumu la kuwasomesha watoto wake aliowaacha.”
Tangu Rais Kikwete, atoe maagizo hayo, ni moja tu la kuwapandisha vyeo polisi ndilo lililotekelezwa, huku watoto wa marehemu PC Abdallah wakiendelea kutaabika kwa kukosa ada na matunzo mbalimbali.
Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa watoto watatu wa PC Abdallah walionyimwa msaada ni Ali, Hamidu na Hamisa.
Kwa sasa Ali anasoma kidato cha tatu katika Sekondari ya Kayenze mkoani Morogoro. Hamidu anasoma kidato cha kwanza katika Sekondari ya Kihonda iliyopo Morogoro, ilhali Hamisa akiwa anasoma darasa la tano katika Shule ya Msingi Bungo. Mmoja wa wanafamilia aliyezungumza kwa masharti ya kutotajwa jina, alisema kwa miaka yote wamekuwa wakifuatilia ahadi ya Rais Kikwete ili watoto hao waweze kusomeshwa, lakini hakuna mafanikio yoyote yaliyokwishapatikana.
“Tumefuatilia ofisi ya IGP (Inspekta Jenerali wa Polisi), miaka yote hii kuanzia mwaka 2006, hakuna chochote tulichoambulia. Tumeonana hadi na Gumbo (Ofisa Tawala), hakuna kitu…ni usumbufu tu,” amesema.
Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Senso, alipoulizwa na JAMHURI kuhusu kukwama kutekelezwa kwa ahadi ya Rais Kikwete, alisema hana rekodi sahihi kuhusu suala hilo.
“Ngoja nifuatilie, hili si suala la kutoa jibu mara moja, nawasiliana na ngazi husika, nikifanikiwa nitawaeleza,” alisema Senso. Kwa sasa watoto wa PC Abdallah wanasoma kwa shida, huku mara kadhaa wakiondolewa shuleni kwa kukosa ada.