Jeshi la polisi limeingia lawamani baada ya kituo kidogo cha polisi Kova – Bwaloni, jijini Dar es Salaam kudaiwa kuchangia kifo cha mtoto wa miezi sita aliyefia rumande baada ya mama yake kuwekwa ndani.

Tukio hilo limetokea Jumatano usiku wa kuamkia Alhamisi ya wiki iliyopita katika kituo hicho kilichofunguliwa mwaka 2010 na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, abacho kilipewa jina lake. Kipo Mbezi kwa Msuguri, Dar es Salaam.

Mbali na kifo kilichotokea, kituo hicho kinalalamikiwa na wakazi wa eneo hilo kwa unyanyasaji na udhalilishaji wa wazi kwa wananchi.

Akizungumza na JAMHURI kwenye msiba wa mtoto huyo (Tony), Mama wa Tony, Mirabi Meshack  alisema: “Sababu ya mtoto wangu kufia mikononi mwa polisi ni askari kukataa kutoa dhamana. Tuliwaomba turudi kesho yake kuendelea na shauri wakakataa.

“Tukawaomba tupelekwe Kituo Kikuu cha Polisi Mbezi Luis, wakakataa. Tuliomba mtoto akae nje ya ‘lokapu’, pale itakapohitajika huduma ya mama basi niruhusiwe nimpatie, nalo likakataliwa.”

Akielezea chanzo cha kufikishwa polisi, Mirabi anasema, “Kisa ni mchezo wa upatu. Tulikuwa tukicheza upatu. Katika mchezo tupo 20. Nimeshachangia watu 19 na ikawadia zamu yangu. Nikaona sipewi pesa zangu na siku zikawa zinayoyoma. Kila nikimwendea Nuru Ramadhani ambaye anafahamika kama Mama Naa kutokana na ufupisho wa jina la mtoto wake Najima akawa ananizungusha.

“Yeye ndiye ‘Kijumbe’(Mkusanya fedha) katika mchezo huu. Nikahoji kuhusiana na pesa zangu. Mama Naa hakunijibu vizuri. Tulipishana kauli hadi tukavutana. Mama Naa aliwaendea viongozi wa Serikali ya Mtaa,” anasema Mirabi.

Viongozi hawa walituweka chini wakayazungumza. Wakaelezwa waume zao wakirudi wayazungumze yaishe. Waliporudi waliyazungumza hata hivyo suluhu haikupatikana.

Baada ya muda walisikia askari wa ulinzi shirikishi wakigonga mlango kwa fujo huku mmoja wao akisema; “Tupe mkeo, tupe mkeo tuondoke naye” na matusi mengine mengi ya nguoni (yamehifadhiwa).

“Tukawaomba tufike kituoni kesho asubuhi. Kwa kuwa usiku ulikwisha ingia na nina mtoto mchanga ambaye pia ni mgonjwa, walikataa. Wakatutoa pale kwa nguvu hadi kituoni. Mume wangu aliomba nipewe dhamana wakakataa. Wakazozana, askari wale wakaamua kumshushia kipigo. Akafanikiwa kuwaponyoka na kukimbia.

“Akaja shangazi yangu ambaye taarifa zilimfikia. Akawaomba askari wanipe dhamana, wakamkatalia. Akajaribu kuwaeleza kuwa hali ya afya ya mtoto si nzuri-anaumwa. Na hapo alipo yupo kwenye matibabu na humo ‘lokapu’ si salama kwa mtoto. Hata hivyo hakuna aliyejali. Shangazi akarudi nyumbani.

“Usiku nikiwa ‘lokapu’ mtoto alizidiwa. Nikawaita, hakuna aliyejibu. Ilipokaribia kupambazuka nikaona mwanangu hapumui na nikasikia ana ubaridi usio wa kawaida. Nikawaita wale askari, awamu hii wakaitika nikawaambia hali ya mtoto, wakamgusa. Wakaitana pembeni. Baadae walirudi wakaniruhusu niondoke hapo kituoni.

“Nikiwa njiani nikakutana na Mzee Rashid Mussa, almaarufu Mzee Mpare, akanijulia hali kwa kuwa alikuwa anajua yaliyonisibu jana yake. Wakati anamjulia hali mtoto akashangaa na kuniuliza mbona mtoto hayuko hai? Alinishauri turudi kituoni.

“Tuliporudi tukakuta kituo kimefungwa na wale askari hawapo. Wakati huo palikuwa pamepambazuka. Watu walijaa hapo kituoni kwani taarifa zilikuwa zimeshazagaa.  Shangazi na Mume wangu nao wakafika kituoni. Niliona Mzee Mpare akizungumza na baadhi ya watu  baadae walipiga simu kwa viongozi wa jeshi la Polisi.

“Askari walifika mara moja. Wakati huo Mkuu wa Kituo hicho,  alikuwa hajafika. Alipofika, alihojiwa na kuwekwa chini ya ulinzi. Sote tukapelekwa kituo cha polisi Mbezi Luis, huko tuliandika maelezo. Mwili wa marehemu ulipelekwa hospitali ya Tumbi, Kibaha. Mkuu wa Kituo cha Polisi Kova -Bwaloni na Mama Naa walibaki kituoni hapo,” anasema Mirabi.

Bibi wa marehemu, Esther Chibakuli anasema, “Kama alivyoeleza Mirabi. Marehemu mjukuu wangu alikuwa ni mgonjwa kabla ya kifo chake. Kwa kweli tukio hili limenisikitisha. Mbali ya jitihada zilizofanyika za kuokoa maisha yake lakini polisi walikwamisha.

“Walimweka ‘lokapu’ mpaka akapoteza maisha ndipo wakamwachia. Mazingira ya ‘lokapu’ yanaeleweka. ‘Lokapu’ kwa mtoto mchanga si salama. ‘Lokapu’ hakuna hewa safi na ya kutosha. Kuna kiza, kuna baridi kali ambayo ni hatari kwa afya ya mtoto hususani kwa mtoto mchanga. Mbu nao ni wengi mule lokapu.”

Mzee Mpare anasema, katika kituo hicho askari wamekuwa na kawaida ya kuendesha mambo kienyeji. “Sisi baada ya kuthibitisha kuwa mtoto amepoteza maisha, tulishauriana na baadhi ya watu na kuwapigia simu kwa viongozi wa jeshi la polisi. Wao waliagiza askari kutoka vituo vikuu vya polisi waliofika kwa hatua zaidi.”

Ofisa Mtendaji wa Mtaa huo, Shah Suleiman alikiri kufahamu kutokea kwa tukio hilo. “Sikufikishiwa taarifa yoyote kabla ya kifo cha mtoto. Kama wanasema viongozi wa mtaa walijaribu kusuluhisha basi si rasmi kwani mimi ndiye Mtendaji Mkuu wa Mtaa na sikuwa na taarifa hizo za mzozo. Hata taarifa niliyonayo si kwamba nimeletewa ofisini bali nimeshuhudia  kutokana na ofisi zetu za serikali ya mtaa kuwa karibu na kituo hiki kidogo cha polisi.”

Baba wa Marehemu, Paskari Matonya amesema, Tukio hilo limewafedhehesha na kuwasikitisha. Wanaomba serikali isiliache suala hilo liishie hewani. “Serikali iwachukulie hatua wote waliohusika katika kusababisha kifo cha mwanangu.” anasema. Anaomba utendaji wa jeshi la polisi uangaliwe upya vitendo kama hivi visiendelee kutokea.

JAMHURI lilifika nyumbani kwa Mama Naa, wapangaji wenzake waliomba kutotajwa majina, wamesema tangu tukio lilipotokea Mama Na ameshikiliwa Kituo cha Polisi Mbezi Luis. Mumewe ametoweka na haijulikani aliko.

Wanasema, hata wao ni wanachama katika mchezo huo, lakini tatizo ni kuwa Mama Naa anapokusanya pesa huwa anazitumia ikifika wakati wa kukabidhi inakuwa mzozo.” Tatizo hili si kwa Mirabi pekee, kuna wanachama wengine watano wamepewa pesa nusu wakati pesa zote za mchezo tumeshachanga. Kuna wengine wawili ambao zamu zao za kupokea pesa zilikuwa kabla ya Mirabi hawajapewa pesa zao hadi leo,” amesema mmoja wa wapangaji.

Mirabi ndiye alikuwa mtu wa mwisho kupokea pesa na inaelezwa kuwa alizihitaji fedha zake akamtibie mwanaye.

Taarifa nyingine zinasema kuwa, Kituo cha Polisi Kova Bwaloni kimekuwa kikikiuka agizo la Kamanda Kova  lililoagiza vituo vyote vidogo vya polisi vifunguliwe asubuhi na inapofika saa moja jioni vifungwe. Kituo hicho kimekuwa kikiendesha shughuli kwa masaa 24.

Watoa taarifa wanaeleza kuwa, kituoni hapo askari polisi  ni mmoja ambaye ndiye Mkuu wa Kituo. Wengine waliobaki ni askari wa polisi jamii ambao wanafanya kazi kienyeji. Imedaiwa kuwa shughuli zao zinaendeshwa kwa unyanyasaji bila kufuata haki na taratibu.

Rosena Mapunda anasema: “Ni kawaida kwa askari shirikishi wa kituo hicho kunyanyasa watu. Wanawalaza watu katika kituo hicho kwa siku moja hadi tatu bila dhamana wala kuwafikisha katika kituo kikuu cha polisi Mbezi Luis. Tatizo linalowatawala ni rushwa.

“Anayeleta malalamiko na anayelalamikiwa wote hulazimishwa kutoa chochote ili wawe huru. Tofauti ya hivyo watakaa kituoni hapo mpaka ‘kieleweke’. Kuna nyakati huwa wanawabambikizia watu kesi. Katika hili nina shaka huenda hata mkuu wa kituo naye anashiriki.

“Tabia chafu zinafanyika kituoni ikiwemo unywaji wa pombe tena kwenye kaunta ya kituo. Kwa ujumla wanalichafua jeshi la polisi hata jina la Kamanda Kova nalo linachafuka. Kazi yao kubwa ni kunyanyasa, kudhalilisha na kukamata watu kwa tuhuma za uzururaji,” anasema Rosena.

Lucy Simbaliama anasema, “Siku hiyo ya tukio kituoni walikuwepo askari shiriki wawili. Majina yao ni: Saidia Kayuka na Fredy almaarufu Baba Koku. Mkuu wa Kituo yeye jina lake ni Adiel Zakaria Ayo ambaye wakati wa tukio hakuwepo.”

Mwanasheria na wakili wa kujitegemea, Buruhani Mussa akizungumza na JAMHURI kuhusiana na dhamana anasema, “Sheria inasema dhamana ni haki ya mtuhumiwa mwenye tuhuma zinazoruhusu kupewa dhamana. Kwa mujibu wa maelezo, hiyo ni kesi ya jinai. Kifo cha mtoto kinaonekana kimetokana na uzembe wa askari.”

Katika kituo cha Polisi Mbezi Luis, Mkuu wa Kituo, Joseph Kajange amekiri kutokea kwa tukio hilo na kushikiliwa kwa Mama Na na Adieli Zakaria Ayo katika kituo hicho.

Kamanda Kova aliliambia JAMHURI kuwasiliana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kiondoni, Cammilius Wambura aliyedai yuko kikaoni.