DAR ES SALAAM
NA MWANDISHI WETU
Polisi kadhaa wanalalamikiwa kuwa wanashirikiana na mtandao wa biashara ya magari kufanya dhuluma.
Mkazi mmoja wa Dar es Salaam, Michael Onduru, amekumbwa na kadhia hiyo. Analalamika kuwa licha ya kuwapo vielelezo vya namna alivyonunua gari na kulipa kodi zote kisheria, polisi hawajafikisha shauri hilo mahakamani.
“Kisingizio ni kile kile kilichozoeleka kwa miaka mingi – upelelezi haujakamilika,” amesema Onduru.
Amesema kachero wa polisi aliyedai alitoka Arusha alimwandikia hati ya ‘seizure notice’ na kuondoka na gari lake.
“Walitaka kuchukua pia kadi halisi ya gari, lakini hilo niliwakatalia na kuwashinda kwa hoja,” amesema.
Mambo yalivyokuwa
Onduru ambaye ni mzee anayesumbuliwa na kisukari, amesema mtandao huo wa dhuluma huhusisha makubaliano ya watu wawili wenye uhusiano kibiashara. Makubaliano hayo ni mmoja kumuagizia mwenzake gari.
“Gari linaingia nchini likiwa limeingizwa na mtu kwa niaba ya mwingine (aliyeagiza). Mgogoro unatengenezwa baada ya mwagizaji kushindwa kulipa gharama stahiki kama za bandari na ushuru wa forodha (Bandari [TPA] na Mamlaka ya Mapato Tanznaia [TRA]).
“Sasa kwenye suala langu, aliyeingiza gari akaenda kukopa fedha katika kampuni ya mikopo (Pro-Share Capital Limited) kisha akaenda kulipa gharama (TPA na TRA) akimshirikisha jamaa yake aliyemwomba amuagizie gari,” amesema.
Amesema masharti hapo ni kwamba mkopo usiporejeshwa kwa wakati basi, gari huuzwa na kampuni iliyotoa mkopo likiwa mikononi mwa mkopaji.
Onduru anamtaja aliyemwelekeza kuwa Pro–Share Capital wanauza magari kuwa ni mkazi wa Arusha aliyekuwa Dar es Salaam wakati huo.
“Julai 22, 2020 nikaenda kwao na kupokewa na Meneja wa Fedha wa Pro-Share Capital aliyejitambulisha kwa jina la Dickson Bukeye.
“Kama mnunuzi halali nisiyejua lolote, nikalipa fedha kununua gari na vielelezo vyote ninavyo. Baadaye nikawa mmiliki halali wa kisheria wa gari hilo Nissan X-Trail lenye usajili namba T 764 DRE.
“Wala sikufahamu kuwapo kwa mgogoro wa aina yoyote wa umiliki ndiyo maana ninajiuliza iweje mimi nionekane mwizi? Mwizi anaweza akalipia mali anayoiba? Kwanini nitengenezewe kesi ya wizi kwa gari nililolinunua wakati aliyeniuzia yupo na hajakataa?” amehoji Onduru.
JAMHURI linazo nakala za mauziano hayo na nyaraka nyingine.
Onduru anaendelea: “Tukakubaliana na Bukeye (Meneja wa Fedha Pro-Share Capital) ninunue gari hilo kwa Sh 10,500,000. Siku hiyo hiyo nikalipa Sh 5,000,000.
“Wiki moja baadaye (Julai 28, 2020) nikalipa Sh 2,500,000 kisha Agosti 4 nikawalipa Sh 400,000; na tena Sh 2,600,000 hivyo kufanya malipo ya jumla kuwa Sh 10,500,000,” amesema.
Kati ya fedha hizo, Sh 7,900,000 ziliwekwa Benki ya CRDB akaunti namba 01J1098157200 inayomilikiwa na Pro-Share Capital Limited.
Taarifa zilizopo BoT zinaonyesha kuwa Pro – Share Capital Limited ni kampuni ya kutoa huduma za mikopo ya fedha.
Taarifa zinaonyesha kuwa gari lililonunuliwa na Onduru lenye chassis namba T30025370 lilikuwa likimilikiwa na wamiliki wawili; Kampuni ya Pro-Share Capital kwa upande mmoja, na Dino Chambago kwa upande mwingine.
“Hapa maana yake Pro-Share Capital ni mdhamini wa mkopo unaodaiwa kuchukuliwa na Dino Chambago kwa dhamana ya gari nililouziwa,” anasema.
Baada ya malipo Onduru akakabidhiwa gari na kuondoka nalo (nakala ya ‘gate pass’ tunayo) na kukabidhiwa kadi ya gari namba 8155366 yenye majina Pro-Share Capital na Chambago.
Amesema: “Pro-Share Capital wakaandika barua TRA Ilala kuomba kuondolewa jina katika umiliki wa kuchangia, libaki jina la Chambago pekee ili umiliki ubadilishwe na kuandikwa jina langu.
“TRA wakanikadiria tozo ya Sh 150,000 kisha wakaidhinisha umiliki mpya wa gari. Mimi nikawa mmiliki hadi sasa.”
Madai ya wizi wa gari
Onduru amesema Oktoba 23, 2021 aliitwa Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam ambako alikutana na kachero Koplo Cosmas, kutoka Arusha.
“Bila kunionyesha nyaraka zozote za kipolisi, akaniambia amekuja kumkamata mmiliki wa gari T 764 DRE lililoibwa Arusha, kwamba mtuhumiwa (Onduru) ataitwa mahakamani Arusha baada ya upelelezi kukamilika,” amesema.
Onduru aliachiwa kwa dhamana huku gari likidaiwa kupelekwa Arusha baada ya kuandikiwa ‘seizure notice’ ya kesi ya wizi yenye Kumb MRT/IR/1300/21.
Baada ya kadhia hiyo Onduru na wakili wake walikwenda Pro-Share Capital kukutana na Bukeye; ofisa aliyeuza gari ambalo sasa linashikiliwa polisi.
Anadaiwa kuwa Bukeye hakuonyesha ushirikiano, na akakana kuuza gari la wizi.
Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa gari hilo lilisajiliwa kwa mara ya kwanza Julai 29, 2019 ofisi za TRA Ilala kabla ya kununuliwa Agosti 4, 2020 katika ‘showroom’ ya Pro- Share lilikokuwa kama dhamana ya mkopo na kuandikishwa kwa mmiliki mpya (Onduru) Oktoba 6, 2020 kabla ya kukamatwa Oktoba 2021.
Kwa nini askari wa Arusha?
Bado hajafahamika kwanini gari lililosajiliwa Ilala, Dar es Salaam na kutumika kama dhamana ya mkopo; likauzwa na kununuliwa Dar es Salaam; likamatwe na askari kutoka Arusha na kesi ifunguliwe Arusha.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Muliro Muliro, amesema: “Jeshi la Polisi linafanya kazi kwa weledi na kufuata misingi ya haki na sheria ndiyo maana mtuhumiwa alipewa dhamana. Upelelezi ukikamilika atapelekwa Arusha jalada lilikofunguliwa.
“Ni sawa jalada kufunguliwa Arusha kwa sababu hapa hatuwezi kuwa na jalada la kesi ya Arusha.”
Ofisa wa Pro-Share Capital, Bukeye, alipopigiwa simu na mwandishi wa habari hii hakutaka kuzungumzia undani wa sakata hili. Akasema: “Hili suala lipo polisi, hivyo mimi sina uwezo wa kulizungumzia. Polisi bado wanaendelea na upelelezi.”
Hata alipoambiwa kwamba masuala ambayo hapaswi kuyazungumzia ni yaliyopo mahakamani, Bukeye hakutoa ushirikiano.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo, ameliambia JAMHURI: “Mimi siwezi kujua kila kesi. Nina vituo karibu 100 na kitu, siwezi kujua kila jambo. Huyu mlalamikaji aende akamuulize mkuu wa upelelezi wa wilaya au mkuu wa kituo cha polisi alikokwenda gari lilipokamatwa.”
Kuhusu hatua ambayo upelelezi umefikia, RPC hakuwa tayari kulizungumzia hilo akisema:
“Hatuwezi kusema upelelezi umefikia wapi kwa kuwa kuna kesi moja huko nyuma tuliwahi kuzungumza na mtu kwenye simu kumbe ndiye mhusika mwenyewe.”