Mamlaka huru inayosimamia Jeshi la Polisi nchini Kenya IPOA imesema inachunguza polisi waliohusika kwa njia yoyote kufuatia ugunduzi wa miili iliyokatwakatwa na kutupwa kwenye shimo la jalala mjini Nairobi.

Awali polisi walisema miili kadhaa iliyokatwakatwa ya wanawake sita iliyofungwa kwenye mifuko ya plastiki ilipatikana siku ya Ijumaa ikiwa imetupwa kwenye jalala la taka katika timbo isiyotumika huko Mukuru, kusini mwa mji mkuu, Nairobi.

Mamlaka ya IPOA ilisema katika taarifa baadaye kwamba mabaki ya watu wapatao tisa ilikuwa imegunduliwa, saba ya wanawake, na kuitisha uchunguzi wa haraka ufanyike kuitambua.

“Miili iliyofungwa kwenye mifuko na kamba za nailoni, ilikuwa na alama za wazi za mateso ya kukatwakatwa,” ilisema mamlaka hiyo, ikidokeza kwamba jalala hilo lilikuwa chini ya mita 100 kutoka kituo cha polisi.

Polisi ya Kenya wanakabiliwa na ukosoaji na shinikizo baada ya watu kadhaa kuuliwa wakati wa maandamano ya mwezi uliopita, huku mashirika ya kutetea haki za binadamu yakiwatuhumu maafisa wa polisi kwa kutumia nguvu kupita kiasi.

Kamanda wa jeshi la polisi Japhet Koome, aliyelengwa sana katika ghadhabu ya umma kuhusiana na vifo hivyo, amejiuzulu chini ya miaka miwili tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo, afisi ya rais ilitangaza Ijumaa.

Ni kiongozi wa hivi karibuni wa cheo cha juu kuachia ngazi huku rais William Ruto akijitahidi kudhibiti mgogoro mbaya kabisa wa utawala wake, uliosababishwa na mapendekezo ya kuongeza kodi uliokosolewa sana.

Kamanda Mkuu wa jeshi la polisi Kenya aliyejiuzulu, Japhet KoomePicha: AP Photo/picture alliance
Umati wa watu waliokusanyika Ijumaa katika eneo kulikopatikana miili walikuwa wakipiga kelele wakisema “Ruto lazima aende”, kauli mbiu ya wimbi la maandamano yaliyoongozwa na vijana Wakenya wenye umri mdogo wa vuguvugu la Gen-Z.

Polisi ya Kenya wanaogopwa na hukabiliwa na madai ya mara kwa mara ya mauaji kinyume cha sheria lakini ni nadra kushtakiwa na kuhukumiwa.