MBOGWE
Na Antony Sollo
Polisi mkoani Geita wameanza uchunguzi wa tuhuma zilizotolewa bungeni wiki chache zilizopita kuwa maofisa madini mkoani hapa wamewaua kikatili watu sita.
Tuhuma hizo zilitolewa bungeni jijini Dodoma na Mbunge wa Mbogwe, Nicodemus Maganga, akidai kuwa mmoja wa watu waliouawa ni binamu yake.
Maganga alimuomba Spika Job Ndugai kulielekeza Bunge kujadili alichodai kuwa ni ‘jambo la dharura’ lililotokea jimboni mwake.
Hata hivyo, Spika Ndugai alimuomba Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kulishughulikia jambo hilo.
Na sasa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita (RPC), Henry Mwaibambe, anasema hawajapata taarifa hizo na kumuomba mbunge atoe ushirikiano ili jeshi lifuatilie na haki itendeke.
“Tumepokea kwa masikitiko madai kuwa wananchi sita wa Wilaya ya Mbogwe wameuawa kikatili.
“Nikiwa mjumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, sijapata taarifa hizo. Hata hivyo, tumezichukua kwa uzito na kufungua jalada la upelelezi na kuanza uchunguzi,” anasema Mwaibambe.
Hadi Novemba 16, mwaka huu tayari maelezo ya mashahidi wanane, akiwamo Katibu wa Mbunge, yamechukuliwa na polisi.
JAMHURI limeshuhudia askari wa upelelezi wakiwahoji watu mbalimbali eneo ambalo Mbunge Maganga hufanyia shughuli za uchenjuaji madini.
Ndugu wa Mbunge Maganga ni miongoni mwa watu waliohojiwa katika harakati za Jeshi la Polisi kufahamu ni akina nani hasa waliouawa.
“Uhai wa binadamu una thamani kubwa. Uhai haununuliwi, ndiyo maana ni lazima kuzichukulia tuhuma hizi kwa uzito stahiki.
“Mbunge ni rafiki yangu, tunafahamiana sana. Ninashangaa kwa nini hakuona sababu ya kunishirikisha katika suala zito kama hili, kwa kuwa tunashirikiana naye katika mambo mengi sana,” anasema RPC.
Hata hivyo, tangu kumalizika kwa mkutano uliopita wa Bunge jijini Dodoma, Maganga amekuwa akionekana kwa nadra na kuna madai kuwa afya yake si nzuri.
Ili kujua nini kinamsumbua, JAMHURI limezungumza na watu wa karibu na mbunge huyu na hakuna anayefahamu hasa nini kinamsumbua.
“Huenda amegundua kuwa hatapata ushahidi wa tuhuma nzito alizotoa bungeni, hivyo kujikuta kwenye wakati mgumu.
“Nijuavyo mimi katika maeneo haya hakujawahi kutokea tukio la aina hii (kuuawa watu sita). Nadhani anaweza kuitwa kwenye Kamati ya Maadili ya Bunge kuthibitisha tuhuma hizi,” anasema mmoja wa ndugu wa Maganga (tunahifadhi jina lake).
Kwa muda mrefu mwandishi wa habari hii amejaribu bila mafanikio kumtafuta Mbunge Maganga kwa simu ya mkononi, ambayo imezimwa.
JAMHURI likabisha hodi nyumbani kwake Mtaa wa Shinyanga ‘B’, Masumbwe Sekondari, na kukutana na mke wake, aliyedai kuwa mumewe yupo safarini Mwanza.