Baada ya wananchi wa Wilaya za Kilosa na Mvomero mkoani Morogoro kuwataja wabunge wa mkoa huo kuhusika na migogoro kati ya wakulima na wafugaji, Mbunge wa Mvomero, Amos Makalla, amesema chanzo ni udhaifu wa Jeshi la Polisi.
Amos Makalla, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maji, ameieleza JAMHURI mwishoni mwa wiki iliyopita kwamba amesikitishwa na vitendo vya uhasama, mauaji ya watu, uporaji wa mali za wananchi, vitendo vinavyoendelea katika jimbo lake huku Jeshi la Polisi likishindwa kuchukua hatua kwa wahusika.
“Polisi wamekuwa wakipewa taarifa za viashiria vya uvunjifu wa amani na wananchi lakini wanashindwa kuchukua hatua mapema na matokeo yake wanaonekana baada ya tukio huku watu wamekwishauawa ama mali zao kuharibiwa, hapa kuna tatizo,” anasema Makalla.
Anasema chanzo kingine cha mgogoro huo kati ya wakulima na wafugaji uliodumu kwa kipindi kirefu bila kupatiwa ufumbuzi wowote ni Serikali kuchelewa kuweka mipaka inayoeleweka kutenganisha maeneo ya wafugaji na wakulima.
Pamoja na hayo, Naibu Waziri huyo amekana kuhusika na ufadhili wa Jeshi la Jadi (Mwano), lililoundwa na wakulima wanaopambana na wafugaji wa Kimaasai na kueleza kwamba ni hatua ya wananchi wenyewe baada ya kuona Jeshi la Polisi likionesha udhaifu mkubwa wa kukabiliana na matukio ya uvunjifu wa amani hata wanapopewa taarifa mapema.
“Mimi vurugu hizi nimezikuta, zilianza mwaka 1991 nikiwa kidato cha nne waliuawa watu wawili – mkulima na mfugaji – na kujirudia mwaka 2005 kabla sijawa mbunge wa jimbo hili,” anasema.
Anasema mwaka 2010 akiwa mbunge, alianza jitihada za kusuluhisha mgogoro huo alioukuta ukiibuka mara kwa mara na kupoteza maisha ya watu na mali zao kwa kuwaleta mawaziri wa wizara nne tofauti na pia kumwomba Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuonana na wananchi kwa lengo la kuleta ufumbuzi wa haraka.
Hata hivyo, anasema bado anaendelea na jitihada za kulipatia ufumbuzi suala hilo na kusisitiza kwamba Serikali inapaswa kupima upya maeneo hayo na kuweka wazi mipaka, kwa kutafuta maridhiano kati ya jamii za wafugaji na wakulima kwa kudumisha amani na ushirikiano kwani sote ni raia wa Tanzania.
Mbunge huyo amelitaka Jeshi la Polisi kuacha kupuuza taarifa za kiitelijensia, zinazotolewa na wananchi na kuchukua hatua kwa haraka ili kudhibiti matukio ya uvunjifu wa amani badala ya kujitokeza baada ya wananchi kuuana na kupoteza mali zao.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonard Paul, alipotafutwa na gazeti hili ili kuelezea madai hayo ya udhaifu kwa jeshi hilo mkoani humo na kusababisha wananchi kuunda majeshi yao ya jadi (mwano), alipokea simu na kushindwa kuzungumza chochote.
Wiki iliyopita mwandishi wa JAMHURI alitembelea vijiji vya wakulima na wafugaji katika wilaya za Kilosa na Mvomero na kuzungumza na nyakati tofauti na wananchi waishio katika vijiji hivyo walieleza kukatishwa tamaa na mapigano yasiyokoma, huku yakiwanufaisha watu wachache wanaotoka nje ya wilaya hizo.
Wanasema baadhi ya viongozi wa Serikali waliogawana ardhi iliyotengwa kwa ajili ya shughuli za kilimo kwa wananchi waishio katika vijiji hivyo wamekuwa na vitendo vya kuchochea migogoro ili kujenga chuki kati ya jamii za wafugaji na wakulima.
Hata hivyo, wamewataja wabunge wanaodaiwa kuchochea migogoro na kupandikiza chuki baina ya jamii za wafugaji na wakulima kwa upande wa vijiji vya Hembeti, Dihombo na Kambala vilivyopo katika Wilaya ya Mvomero kuwa ni Amos Makalla (Mvomero), Ahmed Mabkhut Shabiby (Gairo) na Abdul-Aziz Mohamed Abood (Morogoro Mjini).
Kutokana na madai hayo Amos Makalla amekana kuwa hahusiki na migogoro hiyo wala kufadhili jeshi la jadi la mwano lililoundwa kwa ajili ya kuwasaidia wakulima pale yanapoibuka mapigano na wafugaji.
Kwa upande wake, Abood anasema, “Mvutano unaotokea Morogoro unanisikitisha. Naona watu wengi wamezungumza wakiwamo viongozi wa dini. Bila shaka inatakiwa kutulia na kuzungumza na viongozi wenzangu wa dini na kada nyingine, ili kuiletea Morogoro amani,” anasema Abood.
“Tutakayozungumza bila shaka tutaita waandishi wa habari wafahamu kwa kina namna gani tumetatua matatizo ya wakazi wa Morogoro. Wakazi hawa ni waelewa, nikiwa na imani kwamba tutayazungumza na kumaliza.
“Nayasema haya nina maana kuu. Kwamba mimi ni mbunge wao. Kisemeo cha wanyonge, nawatetea wote. Katu siwezi kuwahujumu watu wangu ambao siku zote wanaamini nawatumikia. Matatizo yako tangu miaka ya nyuma, naamini yatatatuliwa na yatakwisha,” anasema Abood.
Wananchi hao wamelieleza JAMHURI kuwa wabunge hao kwa nyakati tofauti wamekuwa wakiwaleta watu kutoka Morogoro Mjini na nje ya mkoa huo kwa mabasi na kuwapeleka kwenye maeneo ya vijiji hivyo na kuwapa maeneo ya kulima bila kufuata utaratibu uliowekwa na vijiji husika.
Kwa upande wake Ibrahim Rijua anasema miaka iliyopita kabla na baada ya Operesheni Vijiji ya mwaka 1972 waliishi katika kijiji hicho cha Kambala bila kuwa na mgogoro na mtu yoyote, wakiheshimiana na kuthaminiana kama wananchi wa Tanzania tofauti na sasa ambapo viongozi wa kisiasa wamegeuka kuwa wachochezi na wavuga amani nchini.
“Nilizaliwa katika kijiji hiki cha Kambala mwaka 1957 na hii ilikuwa kabla ya Operesheni Vijiji na mwaka 1958 kilifanyika kikao cha kwanza kilichowajumuisha wa sita na kumchagua Lekake Machanja kuwa mjumbe,” anasema Rijua.
Anasema kabla hata uhuru kijiji cha Kambala kilikuwako, na mwaka 1968 Serikali ilianzisha miradi ya maji na kujenga majosho kwa ajili ya mifugo wakati huo Mvomero ikiwa tarafa na Hembeti ikiwa kata.
“Hapa tumechanganyikana na Wapare, Wasukuma, Wahaya, Wabena, Waluguru, Wakagulu wakijihusisha na ufugaji na kilimo, na kabila kuu ni Wamaasai ambao ni wafugaji kwa asilimia 75 lakini kwa miaka yote hatupigani wala hatuna sababu ya kufanya hivyo,” anasema.
Rijua anasema Shule ya Msingi ya Kambala na zahanati ya kijiji hicho zilijengwa mwaka 1977 sambamba na ujenzi wa Masijala.
Hata hivyo, anasema Mei 11, 1984 kilifanyika kikao cha pamoja cha viongozi wa vijiji vya Kambala, Hembeti, Dihombo na Mkindo kuhusu mipaka ya kijiji cha Kambala na vijiji vinavyopakana na kijiji hicho.