Polisi Kata ya Mlangali Wilaya ya Mbozi Mkoa wa Songwe, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Robert Asumile Kasunga amekemea kitendo cha wananchi wa kijiji hicho kuuza na kunywa Pombe za kienyeji muda wa kazi na badala yake watumie muda huo kujishughulisha na shughuli mbalimbali za kiuchumi zitakazo waingizia kipato kwa manufaa ya Taifa na familia zao.

Mkaguzi Kasunga ameyasema hayo Januari 02, 2025 wakati akitoa elimu katika Kilabu cha Ukiwaona kama watu kilichopo Kijiji cha Mlangali ambapo amewataka kuacha kuuza na kutumia Pombe muda ambao wanatakiwa kuwa katika shughuli za maendeleo jambo ambalo ni kinyume cha sheria na kuwasisitiza kuuza vilevi wakiwa wanafuata sheria za nchi ikiwa ni pamoja na kuwa na kibali cha vilevi.

Sambamba na hilo, Mkaguzi Kasunga amewataka wazazi kuwalinda watoto wadogo katika kipindi hiki cha mvua nyingi, kujiepusha na ugomvi unaotokana na ulevi na kuacha unywaji wa pombe uliokithiri ikiwa ni pamoja na kuacha tabia ya visasi ambayo inapelekea mauaji katika jamii.

Kwa upande wao, wafanyabiashara na viongozi wa vilabu hivyo wameahidi kwa pamoja kukemea vitendo vya uuzwaji na unywaji wa Pombe muda wa kazi kwa kutoa taarifa Polisi ili watumiaji na wauzaji wachukuliwe hatua za kisheria ili kukomesha tabia hiyo Kijijini hapo.