Na Israel Mwaisaka, JamhuriMedia, Rukwa

Jeshi la Polisi mkoani Rukwa linamshikilia mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina la Anifa Mwanawima (36) mkazi wa Kijiji Cha Mashete wilayani Nkasi Kwa kosa la kumtupa mtoto wake chooni baada ya kujifungua.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi mkoa Rukwa Shadrack Masija ni kuwa tukio hilo limetokea jana baada ya kubainika kuwa mtoto mchanga ametupwa chooni kutokana na harufu kali iliyokuwa ikitokea chooni ambapo mama mwenye nyumba alitoa taarifa kwa majirani na kwa viongozi wa kijiji.

Amesema kuwa kufuatia hofu hiyo walitoa taarifa Polisi ambao walishirikiana na wananchi na kuiopoa maiti ya mtoto mchanga huku akiwa amekufa na kuharibika vibaya.

Kamanda Masija amesema kuwa baada ya uchunguzi wa haraka ilibainika kuwa kulikuwa na mwanamke aliyekua mjamzito na akiishi katika nyumba hiyo lakini na walipomtazama hawakumuona tena na ujauzito na kumtilia mashaka na katika mahojiano alikiri kuhusika katika tukio hilo.

Amesema kuwa mwanamke huyo siku tatu zilizopita akiwa mjamzito alipata uchungu na kujifungua kwa siri bila ya mtu yeyote kujua na ndipo alipomtumbukiza chooni mtoto huyo na kufariki dunia.

Pia amefafanua kuwa kutokana na uchunguzi wa kitabibu umebaini kuwa mtoto huyo alikua ni wa kiume na amekaa chooni kwa muda wa siku tatu toka atupwe.

Kamanda amesema kuwa tukio hilo limetokana na migogoro ya kifamilia ambapo mama huyo mwenye watoto watatu alitengana na mumewe na kwenda kupanga.

Amesema uchunguzi zaidi juu ya hilo unaendelea na baada ya kukamilika atafikishwaa mahakamani kujibu tuhuma hizo.