Na Mwamvua Mwinyi,JamhuriMedia,Pwani
Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani katika misako iliyofanya kwa kipindi cha mwezi mmoja wamefanikiwa kumkamata mtu mmoja( miaka 53) mwanaume, mkulima mkazi wa kijiji cha Ruvu stesheni,ambae anadaiwa kufanya mauaji, wilayani Kisarawe kisha kutorokea katika kijiji cha Ruvu stesheni.
Pamoja na kukamatwa kwa ajili ya kufanya mauaji pia amekutwa akiwa na silaha aina ya Shortgun Greener yenye namba za usajli 729, maganda sita ya Risasi za Shortgun na unga wa baruti.
Kamanda wa polisi mkoani Pwani,Pius Lutumo alikiri kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo katika msako ulifanyika ndani ya mwezi mmoja ambapo alieleza pia wamekamata silaha aina ya Short Gun moja, silaha aina ya Riffle moja na risasi sita .
“Ni kwamba, huko maeneo ya Msanga sokoni, kata ya Msanga, Tarafa ya Maneromango Wilaya ya Kisarawe Mkoa wa Pwani Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani, wakiwa katika misako na operesheni mbalimbali walimkamata Mtu mmoja, me, miaka 47, mzaramu, mfanyabiashara mkazi wa Msanga sokoni akiwa na Bunduki aina ya Riffle yenye namba za usajili zilizofutika akiwa hana vibali vya umiliki.
Lutumo alieleza,mara baada ya upelelezi kukamilika watuhumiwa hawa watafikishwa mahakamani.
Sanjali na taarifa hizo , Jeshi la Polisi mkoa wa Pwani limefanya misako na operesheni mbalimbali kuanzia tarehe 01/01/2023 hadi tarehe 31/01/2023 kwa lengo la kudhibiti makosa ya uvunjaji, unyang’anyi wa kutumia nguvu, wizi, wizi wa mifugo, utumiaji wa dawa za kulevya na matumizi ya pombe haramu ya moshi (gongo).
Kamanda huyo alifafanua,jumla ya watuhumiwa 19 wanaume wamekamatwa.
Alitaja mali zilizokamatwa kutokana na matukio hayo Kuwa ni Pikipiki mbili, televisheni moja, Speka moja, deki , feni na meza ya Television,Viti 13,Fensi waya rola tatu,Gongo (Pombe ya Moshi) lita 140 na Bhangi gunia 12, Puli 57 na kete 157.
Upelelezi wa matukio hayo utakapokamilika watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowahusu.
Jeshi hilo,linaomba wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa zinazohusiana na uhalifu na wahalifu kwa wakati kwa kuwatumia wakaguzi kata waliopo kwenye maeneo yao yote ndani ya Mkoa wa Pwani.