pg 1Mkataba wa utwaaji wa eneo la Kituo cha Polisi Oysterbay, Dar es Salaam uliofanywa na kampuni ya Mara Capital kutoka nchini Uganda, unatajwa kuwa miongoni mwa mikataba hatari iliyotekelezwa wakati wa uongozi wa Awamu ya Nne.

Mwishoni mwa wiki iliyopita mjini Dodoma, akifungua kikao kazi cha makamanda wa polisi wa mikoa, mawakili wafawidhi wa Serikali na wakuu wa upelelezi wa mikoa na vikosi, Rais Magufuli hakusita kueleza hisia zake juu ya mkataba huo ambao ulipoingiwa mwaka 2012 uliibua maswali mengi.

Rais Magufuli alisema: “Oysterbay pale ni eneo lenye soko, kila mmoja anajua, mmeingia kwenye mikataba mnayoijua nyinyi, akapewa mtu anawajengea pale, sifahamu kama majengo hayo yanafaa.

“Palikuwa na ubaya gani eneo la Oysterbay likawa na hati, mkaitumia hiyo hati kwenda kukopa benki na kujenga nyumba hata za ghorofa 20 pale, mkaweka kitegauchumi na polisi wenu wakakaa pale?”

Gazeti la JAMHURI katika toleo lake Na. 120 la mwaka juzi lilikuwa la kwanza kuandika taarifa za ‘kuuzwa’ kwa eneo hilo kwa mwekezaji.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ndiyo iliyofanikisha mpango huo, ikiwa imeingia mkataba na kampuni ya Mara Capital, ambayo ni kampuni tanzu ya Mara Group.

Pamoja na nyumba za polisi, mwekezaji alipanga kuzitwaa pia nyumba za Shirika la Ugavi wa Umeme (Tanesco) zilizopo eneo hilo, lakini akakwaa kisiki kutokana na msimamo wa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospter Muhongo.

Chanzo cha habari kimedokeza kuwa viongozi wakuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi wakati huo walimfuata Profesa Muhongo wakimshawishi akubali majengo ya Tanesco yajumuishwe kwenye ‘uuzwaji’ huo, lakini waziri huyo aliwakatalia.

“Tulimfuata, akakataa. Hoja yake ikawa kwamba hatuwezi kuruhusu kila kilicho cha Serikali kitolewe kwa wageni wakati wananchi wenyewe wana uwezo wa kufanya baadhi ya mambo. Lakini hoja yake nyingine ikawa kwamba kusogeza majengo makubwa eneo hilo kungesababisha ‘ugomvi’ usio wa lazima na ubalozi wa Marekani.

“Profesa akasema yeye angekuwa tayari kuombwa kubadili matumizi ya eneo hilo kama ingekuwa ni mpango wa kujenga mitambo ya kupoza umeme,” kimesema chanzo chetu.

Mkataba huo unaoiwezesha kampuni hiyo kuchukua eneo lote la Polisi Oysterbay kwa kile kinachotajwa kuwa ni ujenzi wa duka kubwa la kisasa (shopping mall), hoteli mbili, hospitali na huduma nyingine za kibiashara.

Nyumba nyingi walizokuwa wakiishi polisi wa vyeo vya chini na vya kati zimeshabomolewa, huku ujenzi wa kinachotajwa kuwa ndicho kituo kipya cha polisi ukiwa umeanza.

Kwa mujibu wa taarifa za mtandao wa Mara Group, ukubwa wa eneo hilo ni futi za mraba milioni 3.5. Thamani ya vitegauchumi vitakavyojengwa hapo ni dola milioni 300 za Marekani kwa wakati huo ambao dola moja ilikuwa Sh 1,590.

Mradi huo unaelezwa kwamba utakuwa na duka kubwa na la kipekee katika ukanda wa Afrika Mashariki, hoteli mbili za nyota tano, kituo cha mikutano, hospitali ya kisasa, makazi na kituo cha kisasa cha polisi.

Polisi waliokuwa wakiishi eneo hilo walipewa hadi Mei, mwaka jana wawe wameondoka ili kupisha ujenzi. Baadhi walilipwa fedha za kuwawezesha kupata nyumba za kupanga wakati mwekezaji akiwa amepewa eneo jingine mbali na Oysterbay kwa ajili ya ujenzi wa nyumba 300 ambazo baadaye zitatumiwa na polisi hao.

Mkataba huo ulitiwa saini katika Makao Makuu ya Polisi jijini Dar es Salaam na kuwahusisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, wa wakati huo, Mbarak Abdulwakil, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) wa wakati huo, Saidi Mwema, na wakurugenzi wawili wa Mara Group – Ashish Thakkar na Prashant Manek.

Eneo linalohusishwa kwenye mradi huu linaanzia Namanga Shopping Centre hadi Morocco. Mwekezaji huyo alishatoa fedha kwa ajili ya kuwalipa polisi waliohamishwa, ingawa kulikuwapo malalamiko kutoka kwa baadhi ya polisi ya kutoridhishwa na kiasi walichopewa.

Kila polisi wa cheo cha chini aliyehamishwa ilikuwa alipwe Sh milioni tatu, ilhali wale wa vyeo vya juu, kila mmoja alipangiwa Sh milioni saba. Fedha hizo ni kwa ajili ya kusafirisha mizigo pamoja na usumbufu.

Ilipangwa kuwa polisi wa vyeo vya juu wangejengewa nyumba za makazi eneo la Mikocheni; na askari wa vyeo vya chini wangejengewa Kunduchi Mtongani.

Oysterbay ndicho Kituo Kikuu cha Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni. Kwa mabadiliko hayo, inapendekezwa kuwa Kituo cha Mkoa huo kitahamishiwa Kijitonyama- Mabatini!

Mara Group inajinasibu kuwa inajishughulisha na masuala mbalimbali yakiwamo ya ujenzi wa vitegauchumi, teknolojia ya mawasiliano, miundombinu, habari na mawasiliano, na kadhalika. Ina matawi katika mataifa 18 barani Afrika ikiwa imeajiri wafanyakazi zaidi ya 4,000.

Wakati wa utiaji saini makubaliano ya kumkabidhi mwekezaji eneo la Oysterbay, Manek alisema mradi huo mkubwa utaifanya Dar es Salaam kuwa ya kisasa na kuitangaza Tanzania duniani kote.

“Ardhi itabaki kuwa mali ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Jeshi la Polisi la Tanzania,” alisema Mkuu wa Ununuzi katika Jeshi la Polisi aliyetajwa kwa jina la Gregory.

Hiyo haikuwa mara ya kwanza kwa Serikali kuchukua uamuzi wa kuhamisha shughuli za kijeshi kwa ajili ya kuwapisha wawekezaji.

Tayari ilishafanya hivyo kwa kuhamisha Kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Buhemba iliyopo Butiama mkoani Mara, ili kuwapisha wachimba dhahabu – Kampuni ya Meremeta kutoka Afrika Kusini. Kampuni hiyo baadaye ilibainika kuliibia Taifa kiasi kikubwa cha fedha zilizotokana na madini, kabla ya kutimka nchini. Kwa sasa eneo la Buhemba ni magofu na mashimo.

Pia kulikuwa na harakati za baadhi ya mawakala wa wawekezaji, kuona wanafanikiwa kuihamisha Kambi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ya Kiabakari, iliyopo wilayani Butiama mkoani humo, ili kutoa fursa ya uchimbaji dhahabu.

Hata hivyo, habari za uhakika kutoka ndani ya vyombo vya ulinzi na usalama zinasema mpango huo ulikumbana na upinzani mkali, ikizingatiwa kambi hiyo ni muhimu mno katika masuala ya ulinzi na usalama kwa Kanda ya Ziwa.

Kiabakari iliyokuwa mgodi wa dhahabu wakati wa serikali ya kikoloni, ilitumiwa kujenga kambi ya jeshi ili kulinda dhahabu hiyo, ikiwa ni utaratibu uliotumiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kulinda rasilimali za nchi.