Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mwanza

Watu wawili wasiofahamika majina yao wamefariki wakati wa majibizano na Polisi baada ya kukutwa na watoto wawili waliowateka na kutaka kupewa mamilioni ya fedha ili waweze kuwaachia watoto hao.

Akizungumzia tukio hio Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Wilbroad Mutafungwa, amesema tukio hilo la utekaji watoto hao lilitokea Februari 5, 2025, majira ya saa 12:10 asubuhi, eneo la Capripoint katika barabara ya Nassa, Wilaya ya Nyamagana wakiwa kwenye gari yenye namba za usajili T. 233 DJC Toyota Hiace, mali ya shule hiyo wakati wakipelekwa shuleni.

Kamanda Mutafungwa amewataja watoto hao kuwa ni Magreth Thobias Juma (8), mwanafunzi wa darasa la pili na mkazi wa Mtaa wa Hesawa, Capripoint na Fortunata Geofrey Mwakalebela (5), mwanafunzi wa darasa la kwanza na mkazi wa Bugando wote wanafunzi wa shule hiyo iliyopo Nyasaka, Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza.

Amesema kuwa baada ya tukio hilo Jeshi la Polisi lilianza doria na msako katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Mwanza, kwa kutumia wataalamu wa Polisi wa matukio makubwa kwa kushirikiana na wananchi.

Kamanda Mutafungwa amesema kuwa katika msako huo walipata taarifa ya watoto kushikiliwa na kufungiwa ndani katika mtaa wa Nyabulogoya, Kata ya Nyegezi Wilaya ya Nyamagana nyumba namba 8 na kupiga simu kwenye uongozi wa shule hiyo wakitaka kupewa fedha ili waweze kuwaacia watoto hao.

“Wasamaria wema walitoa taarifa kwa Jeshi la Polisi kuhusiana na kushikiliwa kwa watoto hivyo kupitia askari wa kupambana na makosa makubwa ya uhalifu, waliokuwa wakiendelea na msako katika maeneo mbalimbali, mara moja walifika eneo hilo na kuizingira nyumba hiyo kwa lengo la kuwaokoa watoto hao na kuwakamata wahalifu.

“Askari wetu waliokuwa na silaha walipojaribu kuingia katika chumba ambaco watoto hao wamefungiwa wakiwa pamoja na watuhumiwa, ndipo watu wawili jinsi ya kiume walitoka wakiwa na panga, jambia na nondo na kutaka kuwashambulia askari.

“Askari walilazimika kuwafyatulia risasi zilizowajeruhi watekaji na kuvuja damu nyingi,ambapo walipoteza maisha wakati wa jitihada za kuwapeleka hospitali kwa matibabu ” amesema Kamanda Mutafungwa.

Amesema kuwa katika tukio hilo watoto waliokuwa wametekwa walipatikana wakiwa salama na kupelekwa Hospitali ya Mkoa ya Sekou -Toure na askari wa Dawati la Jinsia na Watoto pamoja na Ustawi wa Jamii,kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Ha hivyo katika purukushani hizo watuhumiwa wengine wawili walikimbia baada ya kuwaona askari na juhudi za kuwatafuta zinaendelea

Miili ya watu hao wanaokadiriwa kuwa na umri wa miaka 25 hadi 35, imehifadhiwa hospitali ya Sekou -Toure ,kwa ajili ya uchunguzi na utambuzi.

Hata hivyo ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Mwanza ,kuendelea kutoa ushirikiano ili kudhibiti uhalifu na wahalifu, huku akiwatahadharisha watu wanaojiusisha na vitendo vya utekaji na uhalifu mwingine vinavyoleta taharuki kwa wananchi kuacha mara moja.

“Mkoa wa Mwanza sio sehemu salama kwao, tutawasaka popote pale walipo na kuwachukulia hatua za kisheria,” amesema.