Mchezo wa wanasiasa kutumia kampuni za mfukoni kunyofoa rasilimali za umma bado unaendelea, baada ya JAMHURI kubaini kuwa mmoja wa wabunge wamejipatia zaidi ya Sh bilioni 40 kwa njia ya udanganyifu.

Kibaya zaidi na bila woga, waliokabidhiwa dhamana ya kulinda mali za umma ndiyo waliogeuka ‘mbwa mwitu’ na kutumia nyadhifa zao kunyofoa kila kinachopita mbele yao.

 “Huwezi kuamini. Rais [John] Magufuli anapozungumza wapiga dili si watu wadogo wadogo wa mtaani, bali ni wakubwa. Baadhi ya Polisi wanashirikiana na wabunge ‘kuliibia’ Taifa, wakati wao walipaswa kukamata wabadhirifu,” anasema mtoa habari wa JAMHURI ndani ya Jeshi la Polisi kwa masikitiko.

 Wakati mwaka uliopita nchi ilishuhudia mtikisiko mkubwa kutokana na Kampuni ya Lugumi Enterprises, kujipatia kwa njia ya udanganyifu Sh bilioni 37 kwa ajili ya kufunga vifaa vya kutambua alama za vidole katika wilaya 108 nchini, kampuni hiyo ilifunga vifaa katika wilaya 12 tu na kati ya hizo wilaya nane pekee ndiko vilikokuwa vikifanya kazi na ikalipwa Sh bilioni 34, zamu hii kashfa inayorindima ni ya sare, kofia na makoti ya mvua ndani ya Jeshi la Polisi.

 Katika hali ya kustaajabisha, Kampuni ya Daissy General Traders imepewa zabuni za mabilioni bila kuwasilisha kofia, sare na makoti ya mvua, na sasa uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa inamilikiwa na Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Angela Kizigha.

 Katika nyaraka ambazo JAMHURI imeziona, kwa kipindi cha mwaka mmoja na nusu Daissy General Traders ilipewa zabuni ya sare za Jeshi la Polisi yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 40.

 Mchezo wa kulinyofoa Jeshi la Polisi ulianza Juni 19, 2014 wakati joto la uchaguzi lilipoanza kupanda, ambapo Wizara ya Mambo ya Ndani iliipatia Daissy zabuni namba ME.014/PF/2013/2014/G/34-Lot 11 yenye thamani ya Sh 21,463,750,000. Zabuni hii ilikuwa ni kwa ajili ya sare za polisi na mavazi mengine. 

 Mchezo huu ulienda kwa ‘raketi’ ya hali ya juu, kwani wakati watunza bohari wa polisi wakionesha kuwa nguo na vifaa vinavyotajwa chini ya mikataba mbalimbali vililetwa, uhalisia wakubwa hawa walikuwa wanagonga mihuri makaratasi na kurekodi “bidhaa hewa”. 

 Mei 30, 2015 Wizara ya Mambo ya Ndani ilipoipatia Daissy zabuni namba ME.014/PF/2013/2014/G/3I-Lot 1 yenye thamani ya Sh 716,614. Zabuni hii ilikuwa ya sare na nguo za matukio.

Juni 12, 2015 Jeshi la Polisi lilitoa hati ya mahitaji (Call-Off Order) Na. MOHA/PF/2014/2015/338 zabuni ME.014/PF/2014/2015/G/31-Lot 1 yenye thamani ya Sh 3,524,570,234. Kama zabuni iliyotangulia, hata hii ilitajwa kuwa zabuni ya sare na vifaa visaidizi vya matukio. Zabuni zote zilizofuata zilitajwa kununua vifaa vinavyofanana.

 Juni 15, 2015 Jeshi la Polisi lilitoa hati ya mahitaji (Call-Off Order) Na. MOHA/PF/2014/2015/337 zabuni ME.014/PF/2014/2015/G/31-Lot 1 yenye thamani ya Sh 3,524,570,234.

Novemba 4, 2015 Jeshi la Polisi lilitoa hati ya mahitaji (Call-Off Order) Na. MOHA/PF/2015/2016/108 zabuni ME.014/PF/2015/2016/G/30-Lot 2 yenye thamani ya Sh 22,918,880,600.

Novemba 2, 2015 Wizara ya Mambo ya Ndani iliipatia Daissy zabuni namba ME.014/PF/2015/2016/G/30-Lot 2 yenye thamani ya Sh 716,614.

 Oktoba 1, 2015 Daissy ilipata zabuni namba ME.014/PF/2013/2014/G/30-Lot 2 yenye thamani ya Sh 532,631.

 Katika hali ya kushangaza, Kampuni ya Daissy ilikuwa ikisambaza sare za Jeshi la Polisi kwa mchanganuo kwa gharama ya kutisha;

1.   Kofia Nyeusi (Beret Cap Black) 1 Sh 74,340

2.   Kofia Nyekundu (Beret Cap Red) 1 Sh 77,880

3.   Reflective Jackets 1 Sh 79,060

4.   Koti la mvua (Coat Waterproof R/F) 1 Sh 80,691

5.   Lanyard Single Cord R/F 1 Sh 25,960

6.   Lanyard Double Cord Officers 1 Sh 29,500

7.   Mkanda (Belt Stable Coloured) 1 Sh 64,900

8.   Coat Waterproof White Traffic 1 Sh 100,300

Katika nyaraka hizo, Daissy imebainisha kuwa sare hizo imekuwa ikizichukua China.

Kampuni ya Daissy General Traders inajieleza kuwa na Ofisi Wilaya ya Ilala Mtaa wa Swahili na Uhuru ambayo ilipatiwa leseni ya biashara Julai 21, 2015 namba 01033836 na namba ya ushuru wa mapato 103-758-122.

Katika nyaraka hizo, maafisa wa ghala kuu la Polisi wamethibitisha kupokea sare kutoka Daissy.

“Vifaa vimekaguliwa na Kamati na kuridhika kuwa vina ubora unaoridhisha na vinafaa kwa matumizi yaliyokusudiwa,” inasema sehemu ya taarifa ya Kamati ya Ukaguzi na Mapokezi ya vifaa Ghala Kuu la Polisi Dar es Salaam.

“Kampuni hii hata risiti zake zimekuwa na utata mkubwa. Kwa kutumia tu akili ya kawaida unabaini ujanja ujanja uliofanyika katika kuzitoa maana ilikuwa shida kutoa risiti za malipo ambayo amekuwa akiyapokea,” anasema mtoa taarifa wetu.

Risiti ya mashine (EFD) yenye namba ya mlipa kodi 103758122 iliyotolewa na kampuni ya Daissy kwa Jeshi la Polisi ya Agosti 14, 2014 saa 10: 56 (16:56) yenye namba 0002/000026 inaonesha alilipwa Sh bilioni 4.

Risiti nyingine ya tarehe hiyo hiyo ilitolewa saa 11:44 (17:44), ikiwa namba 0207/001824 kupitia Namba ya Mlipa Kodi (TIN) 103758122 yenye thamani ya Sh bilioni 3.

“Kampuni hii ikichunguzwa itakutwa na mambo ya ajabu, kwani wapo baadhi ya watu wapo nyuma yake. Pia ni moja ya kampuni ambazo zimekuwa ni pasua kichwa baada ya kupata zabuni, maana malipo yakichelewa inakuwa kazi haswaa. Watu wanasumbuliwa mpaka alipwe kwani simu zinapigwa kutoka kila mahali,” anasema mtoa taarifa mwingine.

Julai mwaka jana, wakati anawaapisha Manaibu Kamishna wa Polisi (DCP) na Makamishna Wasaidizi Waandamizi (SACP) wa Jeshi hilo, Rais Magufuli alisema amepata taarifa za rushwa ndani ya Jeshi la Polisi inayokadiriwa kuwa kati ya Sh bilioni 60 ambazo zililipwa kuwanunulia nguo na vifaa vingine askari polisi tangu mwaka 2015, lakini hazijanunuliwa.

Akizungumza na JAMHURI, Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira, amesema hajui nani mmliki wa kampuni ya Daissy kwani ameanza kazi wizarani hapo Januari, mwaka jana.

Alipoelezwa kuwa mmiliki ni mbunge wa Afrika Mashariki, akasema hawezi kuzungumzia umiliki wa kampuni kwani yeye si Mamlaka ya Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA).

“Kwanza mtu huyo unayemzungumzia simjui. Mimi nimeanza kazi Januari, 2016. Mimi sio BRELA na wizara yangu haina haja ya kuyajua hayo. Hebu niache nipumzike leo ni siku ya mapumziko, na kama unataka kumjua mwenye kampuni hiyo nenda BRELA,” amesema Meja Jenerali Rwegasira.

Katika mahojiano na JAMHURI, Angela Kizigha alikiri kuwa mmiliki wa Kampuni ya Daissy na kwamba hakuna kifungu cha sheria kinachomzuia kuwa na kampuni wala kupata zabuni hizo.

Kiziga ameiambia JAMHURI kuwa yeye ni Mtanzania kama walivyo wengine, hivyo haoni kama ni dhambi kwake kumiliki kampuni hiyo, kwani anazo haki kama wengine.

“Hicho unachokiuliza sioni kama kuna habari yoyote. Kama ni suala la kampuni hakuna mahali nimekiuka sheria na taratibu, hivyo unaweza kuandika unavyotaka,” amesema Kizigha.

 Wiki iliyopita, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Rwegasira, amenukuliwa na gazeti la Nipashe akisema kuwa kampuni ya Daissy ni kampuni hewa na kwamba wameshindwa kubaini zilipo ofisi zake.

 Amesema pamoja na kufuatilia anwani ya kampuni hiyo, wameshindwa kuipata kwani hakukuwa na ofisi hizo katika mtaa wa Swahili, jambo ambalo limewalazimu kukabidhi kazi hiyo kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa uchunguzi zaidi.

 Alinukuliwa akisema kuna uwezekano kwamba kuna watu walipeana zabuni hiyo na kampuni ambayo ni ya mfukoni na kwamba suala hilo lipo mkononi mwa Takukuru.

  Msemaji wa Takukuru, Mussa Msalaba, yeye amesema uchunguzi juu ya suala hilo unaendelea na taarifa itatolewa mara tu utakapokamilika.