Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Moshi (MUWSA) imezitangaza rasmi taasisi tatu za Serikali mkoani Kilimanjaro kuwa ni wadaiwa sugu.
Taasisi hizo ni Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC) wa Kilimanjaro, Chuo cha Taaluma ya Polisi (MPA), na Gereza Kuu la Mkoa wa Kilimanjaro, Karanga.
Kutokana na hali hiyo, MUWSA imetoa hati ya siku 14 ya kusudio za kukata huduma ya maji kutokana na malimbikizo ya ankara za huduma hiyo ya Sh bilioni 1.1 katika kipindi cha miaka saba.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mtendaji wa MUWSA, Joyce Msiru, amesema Ofisi ya RPC inadaiwa malimbikizo ya ankara ya maji ya Sh milioni 528.6, MPA Sh milioni 401.9 na Gereza la Karanga linadaiwa Sh milioni 203.7.
Msiru anasema changamoto kubwa aliyonayo ni kwa Mamlaka yake kutolipwa madeni inayozidai taasisi za Serikali; hali aliyosema imeathiri utekelezaji wa mipango mbalimbali ya kuhakikisha watu wengi zaidi wanapata maji safi na salama.
Anasema pamoja na juhudi kubwa zilizofanywa na MUWSA kufuatilia madeni hayo, Serikali imeshindwa kulipa, na pale inapolipa imekuwa ikilipa kidogo.
Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka hiyo inayoongozwa na Shally Raymond, imezuru baadhi ya taasisi zinazodaiwa, lakini haikupata uhakika wa kulipwa karibuni.
Desemba 28, mwaka jana, Bodi, kwa kauli moja iliagiza taasisi hizo zipewe notisi ya siku 14 kulipa malimbikizo hayo, kama zitashindwa, basi zikatiwe huduma ya maji.
MUWSA inasema ina miradi mingi inayohitaji fedha ili itekelezwe na hivyo kuwahakikishia wananchi huduma ya maji.
Baadhi ya miradi hiyo ni upanuzi wa mtandao wa maji katika vitongoji vitano vilivyopo katika Kijiji cha Mabogini ambavyo ni Shule, Mpirani, Rau-Msufini, Sanyaline ‘A’ na Kitongiji cha Mjohoroni.
“Wasipolipa madeni yao, maji tutayaelekeza kwenye maeneo mengine,” amesema Msiru.
Mamlaka hiyo inahitaji Sh milioni 459.081 kwa ajili ya ukarabati wa chemichemi ya Njoro ya Goa na ukarabati wa tangi lililotelekezwa na Halmashauri ya Wilaya ya Moshi Vijijini.
Ameiomba Serikali kusaidia upatikanaji wa fedha ambazo Mamlaka hiyo inazidai taasisi hizo ili ziweze kutumika kuboresha huduma.
Mkuu wa MPA, Matanga Mbushi, amekaririwa akisema kama kusudio hilo la MUWSA litalekelezwa, chuo hicho kitalazima kufungwa.
Anasema chuo hicho hakiwajibiki kulipa ankara za maji kwani wenye wajibu huo ni Hazina.
Taasisi nyingine zinazodaiwa ni Shule ya Sekondari Ufundi ya Moshi (Moshi Tech) wanaodaiwa Sh milioni 34, na Shule ya Sekondari ya Moshi (Old Moshi Sec) wanaodaiwa Sh milioni 17.
Wakati taasisi hizo zikitangazwa kuwa ni wadaiwa sugu, Mamlaka imewapongeza wananchi wa kawaida kwa kulipa vizuri ankara za maji.