*Sheria yawaondolea mamlaka ya kumkamata tena aliyefutiwa kesi
*DPP azuiwa kufungua kesi hadi upelelezi ukamilike, masharti yalegezwa
*Uhujumu uchumi sasa ni kuanzia bilioni 1, awali hata Sh 1 ilihusika
*Mawakili watoa mazito, wapinga kifungu 47A kuwapa polisi meno
DAR ES SALAAM
Na Mwandishi Wetu
Serikali imependekeza mabadiliko makubwa katika sheria mbalimbali nchini ikiwamo kuzuia watu kukamatwa na kushitakiwa kwa makosa yaliyofutwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), JAMHURI linathibitisha.
Tangazo la Serikali lililotolewa katika Gazeti la Serikali Na. 43 Vol. 101 la Oktoba 21, 2021, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Eliezer Feleshi, amependekeza makabadiliko makubwa katika mfumo wa sheria nchini.
Muswada wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali unapendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai Sura ya 20 kwa madhumuni ya kuzuia kukamatwa tena kwa mtuhumiwa aliyeachiwa kutokana na uamuzi wa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuondoa mashtaka kwa ‘nolle prosequi’ kwa mujibu wa kifungu hicho cha 91, isipokuwa kama kuna ushahidi wa kutosha.
Pia, kifungu kipya cha 131A kinaongezwa ili kuweka masharti ya kutofungua mashtaka hadi upelelezi utakapokamilika, isipokuwa kwa makosa makubwa. Madhumuni ya marekebisho hayo ni kupunguza msongamano katika magereza na kuboresha masharti yanayohusiana na mchakato wa makubaliano ya kukiri kosa.
Akizungumza na Gazeti la JAMHURI mwishoni mwa wiki, Wakili wa kujitegemea wa Kampuni ya Haki Kwanza Advocates, Alloyce Komba, amesema hayo ni miongoni mwa marekebisho muhimu kwa sababu awali DPP alikuwa na uwezo kumfutia mashtaka mtuhumiwa, kisha akamkamata tena na kumshitaki kwa makosa yale yale yaliyoondolewa na kuyaanzisha upya bila kujali alishakaa mahabusu kwa muda mrefu.
“Mamlaka hayo ya DPP yalikuwa yanaleta kadhia kubwa kwa washitakiwa na kupingwa na watetezi wa haki za binadamu,” amesema.
Komba amesema muswada huo unamlinda mshitakiwa kutokamatwa tena na kushitakiwa kwa makosa yale yale ya awali isipokuwa kuwe na sababu za kuridhisha kwa mahakama na kesi ianze kusikilizwa mara moja bila kucheleweshwa kwa mujibu wa Kifungu cha 131A (1) cha CPA ambacho nacho ni kipya kinachotaka upelelezi uwe umekamilika ndipo mtuhumiwa ashitakiwe.
“Hii inakomesha kauli zilizozoeleka za waendesha mashitaka kwamba upelelezi bado kukamilika na kutaka kesi kuahirishwa kwa tarehe nyingine za kutajwa na mshitakiwa kurudishwa mahabusu,” amesema.
Komba amesema mapendekezo ya marekebisho hayo yatasaidia DPP kuhakikisha anafungua mashitaka yenye ukamilifu wa upelelezi na mahakama itaweza kukataa mashitaka yanayorudishwa tena na waendesha mashitaka baada ya awali kuyaondoa.
Pia amesema mapendekezo hayo yatasaidia mashitaka kutochelewa kusikilizwa mahakamani kwa sababu ya upelelezi kutokamilika kwa sababu hati ya mashitaka haitapokelewa na mahakama iwapo upelelezi haujakamilika na itapunguza msongamano wa mahabusu magerezani kwa sababu wengi wanasubiria kukamilika kwa upelelezi wa kesi zao.
Vilevile amesema Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) itabidi awe makini katika ukamataji na upelelezi wa watuhumiwa, ikiwamo suala la kubambikia watu kesi ambazo DPP atakosa ushahidi na kumfanya asifungue mashitaka au ayaondoe bila ya kuyarudisha tena.
Kuhusu hilo, Wakili Bashir Yakub, amesema: “Pengine mtu atawaza au atasema, kama wamekatazwa kukupeleka mahakamani bila upelelezi kukamilika sasa si watakuweka tu huko polisi selo muda wanaotaka mpaka upelelezi ukamilike ndipo wakupeleke mahakamani?
“Jibu ni hapana, mabadiliko hayo hayo kifungu cha 131A(2) kinaongeza kuwa ikiwa upelelezi haujakamilika hivyo kutomwezesha mtu kupelekwa mahakamani, basi hata hapo polisi aliposhikiliwa asikae, bali apewe dhamana wakati polisi au mamlaka inayokushikilia ikiendelea kukamilisha upelelezi.”
Muswada unarekebisha kifungu cha tatu kwa kupandisha kiwango cha makosa ya uhujumu uchumi hadi Sh bilioni 1. Awali hakukuwapo kiwango halisi kwani hata Sh 1, ilitosha mtu kushitakiwa kwa makosa ya uhujumu uchumi.
Kuanzia sasa makosa ya uhujumu uchumi yatakuwa na thamani ya kiwango kisichopungua Sh bilioni 1 ambayo Divisheni ya Mahakama Kuu ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi itakuwa na mamlaka ya kusikiliza.
“Kifungu cha 29 kinarekebishwa kuzipa uwezo mahakama za chini kutoa dhamana kwa makosa yenye thamani isiyopungua Sh milioni 300. Lengo la marekebisho hayo ni kupunguza mrundikano wa mashauri,” anasema Jaji Feleshi.
Dhana ya kurahisisha masharti ya dhamana kwa watuhumiwa imepokewa vizuri na wanasheria hapa nchini.
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga, ameonyesha kufurahishwa na hatua hiyo kwa kusema:
“Hili jambo (kuwapo kwa dhamana) kwa kipindi kirefu tumekuwa tukipambana liwepo kwenye vipengele vya sheria. Ninashukuru jitihada zinaelekea kuzaa matunda,” amesema.
Amesema kukosekana dhamana kwa watuhumiwa wa utakatishaji fedha kilikuwa kitendo cha ukandamizaji haki za binadamu kwa kuwa dhamana ni haki ya kila mtu.
Anna amesema ilivyo kwa sasa mtu akishitakiwa kwa utakatishaji fedha anaanza kutumikia kifungo kwa kukaa rumande muda mrefu kabla ya hukumu.
“Hii ni sawa na kuwahukumu kabla ya hukumu halisi kutolewa,” amesema. Anna anataka makosa yote yawe wazi kwa dhamana sawa na zilivyo sheria katika viwango vya kimataifa.
Wakili wa Kitengo cha Sheria Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, Martine Sabini, amesema dhamana kwa watuhumiwa ni hatua nzuri katika utekelezaji wa haki za binadamu kwa vitendo.
“Kumuweka mahabusu mtu kwa tuhuma tu si jambo zuri, huko ni kumhukumu kabla ya uchunguzi kufanyika na makosa yake kubainika.
“Mtu akikaa mahabusu miaka mitano hadi sita bila dhamana, kisha akakutwa hana hatia, anakuwa hajatendewa haki kisheria,” amesema Martine.
Ameongeza kuwa kwa mujibu wa sheria, mtuhumiwa hana makosa hadi mahakama itakapothibitisha makosa yake.
Ibara ya 13(6)(b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) inapiga marufuku kumtia hatiani mtuhumiwa kabla ya kuthibitishwa na Mahakama kwa kusema:
“(b) ni marufuku kwa mtu aliyeshitakiwa kwa kosa la jinai kutendewa kama mtu mwenye kosa hilo mpaka itakapothibitika kuwa anayo hatia ya kutenda kosa hilo.” Kumnyima dhamana mtu ni kumtia hatiani kabla ya kusikilizwa.
Wakili wa kujitegemea, Everist Mnyele, amesema hakukuwa na haja ya kuwanyima watu dhamana kwa makosa yoyote, hata utakatishaji fedha.
“Ilikuwa ni sheria ya kiwivuwivu tu iliyotumika kukandamiza haki za watu. Ni sheria ya kijamaa zaidi iliyokuwa ikitumika Tanzania pekee. Wenzetu wa Kenya hakuna kitu kama hiki,” amesema Mnyele. Kwa Kenya kila kosa linaruhusiwa kupewa dhamana.
Mnyele amesema wakati watu wakisumbuliwa kwa madai ya kuhujumu uchumi, utakatishaji fedha una faida na hasara zake katika uchumi wa taifa husika.
Kauli yake inaungwa mkono na ofisa mmoja wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) aliyeliambia JAMHURI kuwa kuna asilimia fulani ya utakatishaji fedha inayovumilika kiuchumi.
“Fedha haramu za dawa za kulevya, ugaidi na mambo kama haya hazikubaliki. Lakini kuna fedha watu wanajenga hoteli na viwanda na kuajili wananchi, hizi zinavumilika,” amesema ofisa huyo.
Kwa upande wake Wakili Komba, amesema muswada huo umependekeza marekebisho ya vifungu vingi vilivyokandamiza na kutesa watu waliotuhumiwa.
“Ni vizuri sheria hiyo ingefutwa na kutungwa nyingine mpya yenye kulinda haki za binadamu na kulinda uchumi wa nchi. Au itumike tu Sheria ya Uhujumu Uchumi, Sura ya 200 kushughulikia pia masuala ya utakatishaji fedha,” amesema Komba.
Kamati ya Bunge ya Bajeti, Jumamosi iliyopita ilikutana na wadau kutoa maoni yao juu ya muswada huo.
Marekebisho mengine unapendekeza vifungu vya 174, 265 na 285 vinavyoweka masharti ya kuwapo kwa wazee wa baraza kwenye mashauri katika Mahakama Kuu kurekebishwa au kufutwa kwa lengo la kufanya uwepo wao katika usikilizaji wa mashauri Mahakama Kuu kuwa suala la hiari.
Katika sehemu ya nne ya muswada huo wa marekebisho ya sheria mbalimbali unapendekeza marekebisho katika Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Sura ya 20.
Marekebisho yanapendekeza kuongeza kifungu kipya cha 47A kwa lengo la kutoa mamlaka kwa polisi kufanya operesheni za kificho kwa madhumuni ya kuzuia utendaji wa makosa.
Wadau wamepinga kifungu hiki: “Polisi wetu tunawafahamu. Kifungu hiki kinafanana na kifungu kilichokuwa kinapendekezwa katika sheria ya uchunguzi ya nchini Botswana lakini kikakataliwa. Polisi wetu tunawafahamu. Hivi tu wanaua watu hadi Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan anaelekeza wachunguzwe, wakipata kifungu hiki itakuwaje?
“Hapa serikali inataka kuteketeza watu wake. Kifungu hiki ni hatari kuliko ukoma, kwani Polisi wamekuwa wakitumia vibaya madaraka yao, hivyo kuwaruhusu wafanye uchunguzi wa siri, watu wataonewa kama nini. Hii ilikuwa inafanyika wakati wa mkoloni. Ilipenyezwa kwenye Sheria ya Makosa ya Mtandao mwaka 2016, lakini sasa imeongezewa mabega.
“Hivi kuna shida gani kama uchunguzi unaendelea anayechunguzwa akajulishwa? Sheria hii sasa inaandaa uonevu rasmi kupitia vyombo ya dola. Tusiliruhusu wala kukubali hili kutokea. Litatuumiza, hatutakaa tusahau.
“Nawaomba wabunge wakikatae hiki kifungu cha 47A. Kifungu hiki kitatumiwa kisiasa, kinakwenda kuua demokrasi nchini. Kitaandaa majalada ya fitina za kutisha. Hata kama bungeni wamo wabunge wa CCM pekee, waangalie yanayomkuta Ole Sabaya, alikuwa mwana-CCM na ofisa wa Serikali, ila hivi sasa ni mfungwa.
“Zimetumika sheria hizo hizo kabla ya kutungwa. Hivi kweli ofisa wa kampuni ya simu anafika na kusema alikuwa anashiriki kukuchunguza bila wewe kutaarifiwa, hii si ni jinai na ni kinyume cha Katiba ya Tanzania? Kifungu hiki ni hatari. Kikataliwe ndugu zangu,” anasema kiongozi mmoja mstaafu aliyeomba asitajwe gazetini.