Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linachunguza tukio la mtu mmoja aliyejifanya mganga wa jadi huko maeneo ya Mji mwema, Kigamboni, Dar es Salaam kwa kuwanywesha dawa inayodhaniwa kuwa ni sumu na kuwalewesha watu 16 wa familia moja na baadae kuwaibia simu.
Tukio hilo limetokea Februari 18, 2024 majira ya saa tatu usiku wakati mtu huyo aliyejifanya mganga wa jadi alipofika nyumbani kwa familia ya Mzee Halisi Amani kwa lengo la kumtibia mke wake Fatuma Abdalla (52) aliyekuwa anasumbuliwa na tatizo la miguu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 20, 2024 Kamanda Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema mganga huyo aliwanywesha dawa iliyowalewesha familia nzima, wakapoteza fahamu na akawaibia simu 5 za mkononi na kuondoka.
“Kufuatia tukio hilo Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linamtafuta mganga huyo pia limemkamata kwa mahojiano mtu mmoja anayefamika kwa jina la Jalala Ally Said anayedaiwa kushirikiana na mganga huyo,” amesema Muliro.
Ameeleza kuwa wagojwa walilazwa na kupatiwa matibabu kwenye Hospitali ya Wilaya ya Kigamboni mpaka sasa wagonjwa 13 wamesharuhusiwa na wengine watatu wanaendelea kupatiwa matibabu na hali zao zinaendelea vizuri.
Aidha Muliro amesema tukio lingine limetokea Februari, 9, 2024 huko eneo la Tuangoma, Mbagala ambapo mtu mmoja aliyejifanya mganga wa jadi aliwanywesha dawa zilizowalevya na baadae kupoteza fahamu watu watano na kuwaibia pikipiki namba MC474, simu 3 za mkononi na Tsh 30,000.
“Jeshi la Polisi linawatahadharisha wananchi kuhusiana na kuwepo kwa watu wanaojifanya waganga wa jadi ambao huwalewesha watu na wanafamilia kwa ujumla na baadae kuwaibia,” amesema Muliro.