Polisi Mkoa wa Katavi inamsaka mtu mmoja ambaye bado hajafahamika kwa tuhuma za kumlawiti mtoto mwenye umri wa miaka 12.

Tukio hilo limetokea Julai 17, 2023 katika Kijiji cha Dilifu, Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi ambapo mtuhumiwa alimvizia mtoto huyo na kisha kutekeleza kitendo hicho wakati akiwa katika eneo la vichaka.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Kaster Ngonyani alisema mtoto huyo ni mwanafunzi wa darasa la tatu na sasa anaendelea vizuri baada ya kupatiwa matibabu.

Akisimulia tukio hilo mtoto huyo alisema siku ya tukio alitaka kwenda kwenye sherehe na kulikuwa na mkesha wa muziki na rafiki zake, walipofika njiani yeye pekee aliahirisha kuendelea na safari kwa kuwa ilikuwa usiku.

Akiwa peke yake kurudi nyumbani alikutana na mtuhumiwa aliyemtishia kutaka kumchoma kisu, alimziba mdomo na kumkaba shingoni ili asiweze kupiga kelele na kisha kumburuza hadi kichakani na kutekeleza azma yake.

Mama mlezi wa mtoto huyo ambaye alisema alimuokota akiwa ametelekezwa katika umri wa miaka miwili na kisha kumlea kama mtoto wake, alisema siku ya tukio alikwenda kwenye mkesha wa sherehe hiyo ya mjukuu wake na baada ya muda alirudi nyumbani kwake, ambapo alipofika hakuweza kumkuta mtoto wake.

“Mimi niliporudi sikumkuta, nilifikiri alikuwa kwenye sherehe na muda huo atakuwa kwa mama yake mdogo amelala. Baada ya muda alikuja Mwenyekiti akiwa ameambatana na watu wengine wanamrudisha mtoto wangu na baada ya kufika wakaniambia ‘huyo hapo mtoto’ kisha wakaondoka, nilipo muuliza alikuwa wapi alinijibu kuwa amebakwa.

“Huwa nasumbuliwa na maradhi ya figo, kwa muda huo nilikuwa nasikia maumivu makali sikuweza kutoka, lakini pia nilikuwa naogopa kwa sababu huwa wanatuambia kuna matukio ya watu kuchinja chinja hasa usiku. Tulilala hadi asubuhi bila kuchukua hatua yoyote hadi kulipopambazuka tulikwenda na mtoto kwa mwenyekiti kutoa maelezo, alichukua maelezo yangu na ya mtoto lakini hatukwenda polisi,” alisema.

Mama huyo ameliomba jeshi la polisi pamoja na serikali kumsaka mtuhumiwa huyo na kumkamata ili haki ya mtoto wake ipatikane.