Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Arusha
Mrakibu Msaidizi wa Polisi kituo cha polisi Usa wilayani Arumeru mkoani Arusha, F 21639, John Peter Shauri amehukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kukutwa na hatia ya shtaka la uhujumu uchumi la kusafirisha dawa za kulevya aina ya mirungi bunda 264 yenye uzito wa kilo 102.5.
Hukumu hiyo ilitolewa Ijumaa iliyopita katika Mahakama Kuu Babati mkoani Manyara mbele ya Jaji Mfawidhi Mkoa, Jaji John Kahyoza na katika hukumu yake amesema kuwa amemfunga askari huyo baada ya kujiridhisha pasipo na shaka kwa ushahidi wa mashahidi 12 wa Jamhuri walioutoa mahakamani hapo na kupokea vielelezo 11 vilivyowasilishwa na Jamhuri katika mahakama hiyo dhidi ya mshtakiwa
‘’Nina kufunga kifungo cha maisha jela baada kujiridhisha pasipo na shaka yoyote baada ushahidi mashahidi 12 wa Jamhuri na Mahakama kupokea vielelezo 11 vya Jamhuri hivyo vimethibitisha pasipo na shaka yoyote kuwa askari Shauri alitenda kosa hilo hivyo mahakama inamtia hatiani kwa kumfunga kifungo cha maisha jela,” alisema Jaji Kahyoza.
Julai 16, 2023, mtuhumiwa huyo alikamatwa Arusha baada kuwakimbia Polisi wa Babati Julai 13, 2023 akiwa katika sare za Jeshi la Polisi majira ya saa 2.30 asubuhi katika kizuizi cha Polisi Minjingu Manyara akitokea Arusha kwenda Babati akiwa na madasa hayo na alisimamishwa akiwa na gari aina ya Noah Vox rangi nyeusi yenye namba za usajili T465CUS.
Hata hivyo Mahakama ya Mkoa wa Manyara bado ina kesi nyingine inayomhusu askari Polisi kikosi cha usalama barabarani Arusha (Trafic), Sajenti Ismael Kadenya(48) mwenye namba F.3544 ambaye alikamatwa na Polisi Januari 22, mwaka huu, saa 9 usiku katika kijiji cha Silaloda kata ya Silaloda tarafa ya Endagikot Zone ya 17 wilayani Mbulu mkoani Manyara akisafirisha mirungi bunda 340 yenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 50 akitokea mkoani Arusha.
Kesi nyingine ya dawa za kulevya inayowahusu vigogo wengine wa Jeshi la Polisi mkoani Arusha bado haijatolewa maamuzi pamoja na kwa mahakama ya kijeshi ya Jeshi la Polisi kuwatia hatiani wakaguzi waandamizi wanne wa Polisi Arusha kwa makosa matatu ikiwemo kushawishi na kuomba rushwa ya Sh milioni 10 na kuachia madawa ya kulevya aina ya mirungi kilo 1200 yenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 60 katika tukio lililotokea Desemba 5 mwaka jana eneo la Burka kata ya Elerai ndani ya jiji la Arusha majira ya saa 5 asubuhi.
Vigogo wa Polisi waliotiwa hatiani kwa makosa hayo matatu ni pamoja na Mkaguzi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi Arusha ,Mwinyimvua Shomari na Rizki Khatibu ambao wako ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha,Mkaguzi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi ,Yahaya Mokiwa ambaye yuko Kituo cha Polisi Post Soko la Tengeru wilayani Arumeru Mkoani Arusha,Mkaguzi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi na Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Polisi aliyetambuliwa kwa jina moja la Rashid ambaye yuko kituo cha Polisi uwanja mdogo wa Ndege Kisongo Air Polisi Port Arusha.