Wiki iliyopita kundi la vijana zaidi ya 20 linalojiita panya road, mbwa mwitu na mtoto wa mbwa, liliibuka upya na kuvamia, kupora mali na kushambulia watu kwa kutumia silaha za jadi zikiwamo panga jijini Dar es Salaam.
Maeneo yaliyokumbwa zaidi na uvamizi huo ni Kariakoo, Jangwani, Karume na Kigogo, ambapo kundi hilo lilijeruhi watu na kupora mali mbalimabli nyakati za jioni na usiku.
Uvamizi wa aina hiyo unaosababisha watu kulazimika kukimbia ovyo kukwepa kushambuliwa, umepata kutokea mara kadhaa katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam tangu mwaka jana.
Mbali ya uhalifu wa kujeruhi watu na kupora mali mbalimbali, kundi hilo limekuwa likisababisha hofu hata kwa wamiliki na madereva wa daladala, hivyo kuwafanya kusitisha huduma za usafiri katika maeneo linayovamia.
Sisi JAMHURI tunasema bila kusita kwamba kundi hilo la panya road linapata mwanya wa kuendeleza uovu huo kutokana na upungufu wa utekelezaji jukumu la kulinda usalama wa raia na mali zao uliopo katika vyombo vyetu vya ulinzi na usalama, hususan Jeshi la Polisi.
Tunasema hivyo kwa sababu ni jambo lisiloingia akilini kwamba kundi la vijana wenye umri wa kati ya miaka 16 na 20 wenye silaha duni za jadi wanapata mwanya wa kuteka usalama na amani katika Jiji la Dar es Salaam lenye Ikulu ya Rais.
Taswira hii ya uhalifu unaotekelezwa na kundi hilo wakati mwingine mchana kweupe, inaweza kutuaminisha kuwa huenda ni mpango maalum wenye mkono wa baadhi ya viongozi wa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama, waliokusudia kufanya unyang’aji wa kutumia nguvu.
Kwa sabau hiyo, tunauhimiza uongozi wa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama utafakari upya na kuanza kuchukua hatua stahiki zitakazotokomeza kundi hilo kabla halijasababisha madhara makubwa zaidi dhidi ya wakazi wa jijini Dar es Salaam.
Jeshi la Polisi liitishe msako maalum dhidi ya kundi la panya road, wahusika wote wakamatwe na kufikishwa mahakamani kwa hatua kali za kisheria ili kurejesha usalama unaoonekana kutoweshwa na kundi hilo.
Tunaamini Jeshi la Polisi likidhamiria kwa dhati ya kweli litafyeka mtandao wa kundi hilo kwa kuwa silaha za jadi zinazotumiwa na vijana hao hazina uwezo wa kukabiliana na silaha za moto zinazotumiwa na jehi hilo.
Lakini kwa upande mwingine, wananchi wema wa maeneo husika wanapaswa kutoa ushirikiano wa dhati kwa Jeshi la Polisi pale linapojitokeza kukabiliana na kundi hilo kwa dhati ya kweli.
Tunawahimiza wananchi kushiriki kwa nguvu kubwa kutoa ushirikiano utakaosaidia kuwafichua na kuwakamata vijana hao wa panya road kutokana na ukweli usiopingika kwamba wanaishi na kula nao katika majumba yao.
Ni aibu kwa nchi yetu ambayo inasifika kwa amani duniani kutoa mwanya wa kundi dogo na lenye silaha dhaifu kiasi hicho kuteka maeneo katikati ya jiji na kutekeleza mashambulizi na uporaji wa mali za wananchi.
Vyombo vya dola, hususan Jeshi la Polisi litekeleze jukumu lake kikamilifu kwa kuhakikisha linatokomeza kundi hilo la panya road, mbwa mwitu na mtoto wa mbwa, haraka iwezekanavyo ili kuwaondolea hofu wakazi wa Jiji la Dar es Salaam na wageni wanalitembelea.
Jiji la Dar es Salaam bila kundi la panya road, mbwa mwitu na mtoto wa mbwa inawezekana.