Jeshi la Polisi limejipatia sifa kubwa wakati wa kampeni, siku ya upigaji kura na hata wakati wote wa kuhitimishwa kwa shughuli ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Kwa mara ya kwanza, Polisi wa Tanzania walionekana weledi, wavumilivu na wenye staha.
Tumeona namna wagombea urais, hasa wa CCM alivyopambana na wafuasi wa vyama vya upinzani katika miji mikubwa kama Mbeya na Dar es Salaam, lakini polisi walitulia. Wakawapa mwanya wa kuonyesha hisia zao, na mwishowe wakatawanyika kwa amani na utulivu. Matukio hayo na mengine, yaliwapa imani Watanzania kuwa chombo hiki kimeanza kuwa na askari na makamanda wenye weledi.
Lakini kuna matukio ya hivi karibuni yanayolifanya Jeshi la Polisi lianze kupoteza sifa ndogo iliyoanza kuonekana.
Kumetokea mauaji ya kikatili ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Geita, Alphonce Mawazo.
Mwili wake ulipelekwa kuhifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa Bugando jijini Mwanza. Siku hiyo polisi walitumia gesi ya machozi kuwatawanya waombolezaji.
Hiyo ikawa sababu kwa Polisi Mkoa wa Mwanza kuwazuia waombolezaji kuuaga mwili wa marehemu. Hoja yao ni kwamba kama mwili utaagwa, kuna viashiria vya vurugu kutokea.
Sisi JAMHURI hatufungamani na upande wowote. Kwetu sisi usawa na haki bila kujali itikadi za vyama ndiyo msingi wetu mkuu.
Hatuoni mantiki ya kuwazuia waombolezaji kuuaga mwili wa Mawazo. Wajibu wa Polisi ni kuimarisha ulinzi ili wananchi washiriki shughuli halali kwa amani.
Kama ni hofu ya kutokea vurugu kwa sababu wana Chadema wamepata msiba, basi hii ina maana misiba mingi sana katika Tanzania, Afrika na ulimwengu ingeendeshwa kwa utashi kama huu wa Polisi wetu.
Edward Moringe Sokione aliyefariki dunia kwa ajali ya gari, Watanzania walimlilia sana. Hakuna mahali Polisi walisema asiagwe kwa sababu vurugu zingetokea kwa hasira dhidi ya aliyesababisha kifo hicho.
Rais Samora Machel aliyependwa na wananchi wa Msumbiji, alipouawa kwa ndege yake kudunguliwa, hakuna Polisi waliosema waombolezaji wasiage mwili kwa sababu zingetokea vurugu kutokana na hasira za wananchi dhidi ya wauaji, yaani makaburu.
Kuna wana mapinduzi wengi waliouawa na majahili kwa risasi, lakini hakuna Polisi waliosema miili yao isiagwe kwa sababu eti wangeibua chuki dhidi ya waliofanya mauaji hayo.
Kuzuia wananchi kuuaga mwili wa kiongozi wao waliyempenda, Mawazo, si jambo la kiungwana. Ni uonevu ulipindukia ambao kwa nchi inayojali usawa, haiwezi kuuvumilia. Hofu ya Polisi imesimama juu ya nini? Je, wanataka kuficha nini? Wana siri gani? Kazi ya Polisi ni kutoa haki bila upendeleo. Haya wanayofanya kwa Chadema, tuyaone pia wakiyafanya kwa CCM kama kweli ni ya haki.
Uonevu kama huu unawafanya wananchi wazidi kuichukia Serikali ya CCM wakati huu ambao Rais John Magufuli, akijitahidi kurejesha imani ya wananchi. Tunasema huu ni uonevu.