Jeshi la Polisi mkoani Geita limeshindwa kuwakamata walinzi wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo vya ujambazi wa kutumia silaha.

Watuhumiwa hao — Maneno Nangi na John Magige —  wamekwishaapa mbele ya mlalamikaji kwamba wako tayari kutumia fedha zao zote ili kuhakikisha kuwa wanajinasua kwenye tuhuma hizo.

Alipohojiwa na JAMHURI hivi karibuni, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Geita, Joseph Konyo, alidai kuwa amekwishamkabidhi Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Mkoa (RCO), John Temu, jalada hilo apeleleze na baadaye lifikishwe kwa Mwanasheria wa Serikali kwa hatua zaidi.

Alipotakiwa kutoa ufafanuzi wa jalada hilo kurudishwa upya kwa RCO ilhali lilikwishatoka kwake, na Mwanasheria wa Serikali alikwishatoa maelekezo, Kamanda Konyo alisema, “Ndugu yangu mbona unataka kupeleleza kinachopelelezwa? Nimekwambia jalada linapelelezwa upya.”

Watuhumiwa hao wanaendelea kutamba mitaani kwamba watahakikisha kuwa wanafutiwa shitaka linalowakabili.

Hata hivyo, alipotakiwa kutaja kesi za unyang’anyi zenye dhamana na zisizo na dhamana, Kamanda Konyo alisema, “Niseme tu wazi kuwa ni kweli makosa ya unyang’anyi hayana dhamana.”

Wakati kamanda huyo akisema hayo, uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa Mei 8, mwaka huu watuhumiwa hao wa ujambazi walikuwa na maongezi na kamanda huyo yaliyodumu kwa zaidi ya saa moja.

Watuhumiwa hao wakiwa na mmoja wa viongozi wao wa ulinzi mgodini hapo aliyefahamika kwa jina la Badei, walifika ofisini kwa kamanda huyo asubuhi wakiwa na gari lenye namba T 439 AQW aina ya Toyota Land Cruiser.

Habari zaidi zinaeleza kuwa watuhumiwa hao walifika ofisini kwa Kamanda Konyo kushawishi ili jalada hilo libadilishwe kutoka kwenye unyang’anyi wa kutumia silaha isiyokuwa na dhamana, ili wasije kutupwa rumande iwapo jalada hilo litafikishwa mahakamani.

Iwapo Kamanda Konyo atatekeleza ombi la watuhumiwa hao, atakuwa amejichafua mbele ya umma licha ya kuwa na sifa kuu ya kufanya kazi kwa weledi unaotakiwa.

Kwa upande wake, Ramadhani Mashaka, ambaye ni mlalamikaji katika kesi hiyo, ameeleza kushangazwa kwake kuona ukimya unatawala suala hilo, na amemwomba Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu, kuingilia kati ili jalada hilo lifikishwe mahakamani kutokana na ukweli kuwa tangu awali jalada hilo limekuwa likipigwa danadana.

“Nashangaa, nimeambiwa niende kwa Kamanda wa Polisi eti anataka kunihoji, hivi nihojiwe mara ngapi, nimehojiwa, tume imeshakwenda eneo la tukio kujiridhisha, jalada limekwenda kwa Mwanasheria wa Serikali naye akaagiza lifikishwe mahakamani, sasa nikahojiwe ili iweje kama si kutaka kunitisha? Namuomba IGP Mangu anisaidie ili haki itendeke maana nahisi hawa watu wana mtandao mkubwa kwenye Jeshi la Polisi,” alisema Ramadhani.

Kwa upande wake, Maganga, ambaye ni kaka wa Ramadhani, alisema kwamba iwapo jalada hilo litabadilishwa na kufikishwa mahakamani kwa kosa jingine kinyume na maelekezo ya awali ya Mwanasheria wa Serikali, atalazimika kusafiri hadi ofisini kwa IGP Mangu akiwa na mdogo wake ili kumueleza jinsi baadhi ya askari polisi walivyowekwa mfukoni na watuhumiwa hao.

“Ninaapa, nipo tayari kufa, lakini hawa watu lazima wafikishwe mahakamani na wakijidanganya kulibadilisha jalada hilo, nitasafiri hadi kwa IGP Mangu kumweleza kila kitu jinsi hawa watu wanavyoonekana kuwaweka mfukoni baadhi ya askari polisi. Ninamwomba Mwanasheria wa Serikali asijiingize kwenye mtego huu maana najua hizi pesa wanazokula ili kupindisha ukweli zitawatokea puani mambo yakiharibika,” alisema Maganga.

Februari 22, mwaka huu jioni, walinzi hao waliokuwa na bunduki walidaiwa kumteka Ramadhani (24), mkazi wa Mtaa wa Misheni mjini Geita, kisha kumpora Sh milioni 1.5.

Mashaka alikuwa akitokea mjini Geita kuelekea Kijiji cha Nyakabale kupitia barabara ya Nungwe, kupeleka malipo ya wafanyakazi wa kaka yake wanaochenjua mchanga wa dhahabu kijijini hapo.

Vyanzo vya habari vilisema Mashaka alivamiwa na walinzi watano wakiwa wamevalia sare za kazi za mgodi huo, ambapo wawili kati yao walimweka chini na kumwamuru kulala kifudifudi huku wakimtisha kumuua.

Baadaye walinzi hao ambao wametajwa kwa majina ya Maneno Nangi na John Magige walimpora Mashaka kiasi hicho cha fedha, kisha kumwamuru atoweke.

Watuhumiwa wakamatwa, waachiwa

Hata hivyo, hawakuweza kufungua kesi kwa siku hiyo, badala yake ilifunguliwa Februari 25 baada ya kujiridhisha waliomteka na kumpora ni wafanyakazi wa GGM, ambapo baadaye Jeshi la Polisi liliwakamata watuhumiwa wote wawili na kuwaweka rumande.

Katika mazingira yanayodaiwa kutawaliwa na rushwa, watuhumiwa hao waliachiwa muda mfupi baadaye na kutoka wakitamba kuwaweka mfukoni baadhi ya askari polisi wasio waaminifu.

“Yaani hawakukaa sana kituoni hapo, baada ya muda walitoka huku wakitamba kwamba hawakuanzia kwetu, ni wengi wamekwisha wafanyizia na hakuna walichofanywa, na kumtaka jamaa waliyempora awe mpole, vinginevyo yeye ndiye atakayewekwa rumande,” kilisema chanzo chetu.

Mlalamikaji abambikiwa kesi, akamatwa

Katika hali inayothibitisha tambo hizo za watuhumiwa hao, Februari 27, ikiwa ni siku mbili baada ya watuhumiwa hao kuachiwa, mlalamikaji [Ramadhani] alikamatwa na askari polisi mmoja (jina limehifadhiwa) na kubambikiwa kesi ya wizi wa pikipiki, tukio lililotokea katika Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, na kuwekwa mahabusu ya polisi akisubiri kusafirishwa kwenda Kahama kujibu tuhuma hizo.

Akiwa mahabusu ya polisi, kaka yake, Maganga, alipata taarifa na kuamua kwenda kulalamika kwa aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Geita, Leonard Paul, na baadaye aliruhusiwa kumdhamini baada ya kukaa mahabusu kwa zaidi ya saa nne.

Kutokana na tukio hilo la mlalamikaji kubambikiwa kesi, Kamanda Paul alimwamuru Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) ya Geita, Busee Bwire, kuchunguza tukio hilo, ambapo inadaiwa upelelezi ulibaini kuwa Ramadhani hakufanya wizi wa pikipiki wilayani Kahama na kwamba alibambikiwa kesi hiyo kumtisha asifuatilie kesi yake ya kutekwa na kuporwa mali.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana kutoka ndani ya Jeshi la Polisi, tayari askari aliyehusika kumkamata Ramadhani na kumbambikia kesi amekwishafunguliwa jalada la uchunguzi.

Habari zinadai kuwa baada ya kumalizika kwa kesi aliyobambikiwa, jalada la kesi ya awali liliwasilishwa kwa Mwanasheria wa Serikali, ambaye pia alilipitia na kulirudisha polisi kwa maelekezo kwamba watuhumiwa ambao ni walinzi wa GGM wafikishwe mahakamani kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha chini ya jalada namba GE/IR/856/2014.

Machi 8, mwaka huu saa sita mchana, OCD wa Geita, aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Mkoa (RCO) wa Geita, Saimon Pasua, watuhumiwa, viongozi wa ulinzi wa GGM na mlalamikaji walizuru eneo la tukio na kubaini kuwa unyang’anyi huo ulifanyika nje ya mgodi na si ndani ya mgodi kama ilivyodaiwa na watuhumiwa hao.

Uchunguzi zaidi umebaini kuwa Machi 14, mwaka huu watuhumiwa walifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Geita.

Watuhumiwa watoroshwa mahakamani

Hata hivyo, wakiwa mahakamani hapo wakisubiri kusomewa shitaka linalowakabili, ghafla watuhumiwa hao waliondolewa na askari polisi wakarudishwa Ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Geita.

Walipokwenda kuuliza sababu ya walalamikiwa wao kuondolewa mahakamani kabla ya kusomewa shitaka, hawakupata msaada wowote zaidi ya kurudishwa kwa RCO Pasua, ambaye naye aliwarudisha kwa RPC.

Kutokana na maelekezo ya RCO Pasua, Machi 17, Ramadhani na kaka yake, Maganga, walifika ofisini kwa Kamanda Paul, lakini hawakumkuta na walipompigia simu alidai yuko mkoani Mwanza kikazi na hadi anahamishiwa mkoani Morogoro hivi karibuni, hakuna hatua zozote zilizokwisha kuchukuliwa dhidi ya watuhumiwa hao.

Kijana aliyetekwa azungumza

Kijana Ramadhani alipohojiwa na JAMHURI alikiri kutekwa na kuporwa mali na walinzi hao wa GGM, na kwamba umaskini wake ndiyo umesababisha haki kutotendeka kutokana na walalamikaji wake kutuhumiwa kutumia fedha kujinasua kwenye tuhuma hizo.

“Nikwambie tu kwamba hawa watu wametumia fedha nyingi kujinasua. Huyu aliyekuwa RCO alitaka haki itendeke, lakini kila alipokuwa akijaribu alishindwa maana wale watu walikuwa karibu na bosi wake.

“Unavyoniona nimeamua kukaa kwa wasiwasi, sijui hatima yangu maana hawa watu wameshaniahidi nikiendelea kuwafuatafuata nitakiona cha moto, hivyo naogopa, naomba mamlaka za juu zinisaidie nipate haki yangu,” amesisitiza Ramadhani.

Afisa habari GGM akwepa mwandishi

Kwa upande wake, Afisa Habari wa GGM, Tenga Bill Tenga, alipotafutwa ili atoe ufafanuzi wa tuhuma zinazoelekezwa kwa walinzi wa mgodi huo, simu yake iliita bila kupokewa na hata alipotumiwa ujumbe wa maandishi (SMS) hakujibu.

Naye Mwanasheria wa Serikali, Kiria, alipotafutwa ili kutoa ufafanuzi iwapo jalada hilo liliwasilishwa ofisini kwake na kulitolea ufafanuzi wa kisheria, hakupatikana kwa kile kilichodaiwa ametingwa na majukumu ya kiofisi.