Na Alex Kazenga
 

Kwa kipindi kirefu yamekuwepo malalamiko kutoka sehemu mbali mbali nchini watu wakilituhumu Jeshi la Polisi kutumia nguvu zilizopitiliza kwa raia wanapotuhumiwa kuwa na makosa.

Hali hiyo kwa mara nyingi imeacha taharuki kwenye jamii huku baadhi ya watuhumiwa wakipata ulemavu, wengine wakipoteza uhai kutokana na kushindwa kuhimili nguvu hiyo.

Uwepo wa tuhuma hizo za muda mrefu umedhihiri karibuni katika Kijiji cha Mang’ula wilayani Kilombero, mkoani Morogoro baada ya askari polisi kulazimisha kumkamata na kumuweka mahabusu mwanamke mjamzito aliyejifungua muda mfupi baadaye.

Inaelezwa kuwa Amina Mbunda ambaye amekutwa na mkasa huo, alifikishwa kituo cha polisi na kuwekwa mahabusu kwa kosa la mume wake kununua kitanda kinachosadikiwa kuwa cha wizi.

Pamoja na mwanamke huyu kujieleza kuwa ni mjamzito, bado alikumbana na unyama wa askari Andrew Songea na wenzake wa kituo hicho ambao kukubaliana kumweka mahabusu huku wakiwa wametaarifiwa juu ya hali ya mjamzito huyo.

Baada ya kukaa mahabusu kwa saa kadhaa,  inaelezwa Amina Mbunda alijifungulia nje ya kituo kama mnyama pori hatua chache kutoka kituo hicho cha polisi, tena bila kusaidiwa na mtu yoyote huku akiwa chini ya ulinzi kutoka kwa askari wa zamu aliyegoma kumwahisha kituo cha afya ajifungue salama.

Tukio hili la kinyama limewafanya baadhi ya askari waonekane hawana tofauti na wanyamapori kwani wao hawana uwezo wa kuyatawala mazingira yao zaidi ya kuendeshwa na hisia na mihemko ya kimwili.

Kimeonyesha ni kwa kiasi gani baadhi ya askari hawatambui msingi wa kazi zao na umhimu wa uhai wa mtu na haki za binadamu kwa ujumla.

Tukio hilo ni ushahidi wa malalamiko ya watu kwa kipindi kirefu kwamba askari polisi wanahusika kuwanyanyasa na kuwatesa raia kwa tuhuma zisizo na msingi huku wakisahau jukumu lao kuu kuwa ni kulinda raia na mali zao.

Katika hali ya kawaida, mtu anayetumia vizuri fikira zake ni rahisi kubaini kuwa mwanamke huyo alihitaji kusikilizwa kabla ya kuchukua uamzi wa kumuweka mahabusu.

 

Hali hiyo imekuwa tofauti kwa askari wetu, wamekuwa wazuri wa kutenda bila kutumia fikra kwa usahihi, wanachojali wao ni kutekeleza maagizo au vifungu vya sheria zinazowaongoza, wakati mwingine bila kuzisoma zinataka nini kifanyike katika kazi, bila kutaja haja ya kuangalia mazingira ya utekelezaji wake.

Kadhia hii ya kutenda bila kufikiri au kutumia ubongo kuchanganua mambo kwa usahihi haiwakumbi askari polisi peke yao, bali ni ugonjwa wa watu wengi waliopo kwenye jamii yetu.

Zipo kesi nyingi zinajitokeza katika jamii yetu ambazo zinapima uwezo wetu binafsi wa kufikiri dhidi ya viwango vya elimu tuliyo nayo katika kuchanganua mambo na kupata suluhisho la changamoto zetu.

Hali hii huenda inatokana  na kukosekana kwa watu wenye uwezo wa kutenda kwa kujiamini katika jamii yetu, hivyo kuishia kufanya kazi kwa woga.

Katika mkanganyiko wa mambo kama huo wanafalsafa wa zamani kama Plato na Socretes walianzisha madarasa kwa ajili ya watu kujifunza namna ya kufikiri na kutumia ubongo kwa ufasaha.

Lakini jambo la kushangaza, katika jamii yetu hali hiyo ni tofauti, watu wameenda shule kukariri maandishi na kuongeza vyeti baadala ya kusoma baadaye elimu yao itumike kuleta matokeo chanya katika maeneo yao ya kazi.

Pengine hatupaswi kulaumu uwepo wa hali kama hii. Huenda ikawa ni njia ya kutukumbusha kuwa mfumo wa elimu tulio nao ni mbovu kwani unazalisha watu wabovu ndiyo maana matukio ya hovyo hayaishi mitaani.

Hivyo, wakati viongozi wakitaka uchunguzi kufanyika kubaini ukweli wa matukio kama la mwanamke huyu, pia wanapaswa kuangalia upya mfumo wa elimu kwani unaonekana kuzalisha watu dhaifu katika mazingira yao.

Kwani huenda msingi mkubwa wa  matukio kama hayo unatokana na kushindwa kutumia fikira kwa usahihi katika kutatua changamoto zetu za kimaisha baadala yake tunategemea maisha ya kukariri. Vyoyove iwavyo, lazima askari aliyefanya umyama huu Mang’ula awajibike kwa matendo yake.