Jeshi la Polisi mkoani Arusha limesema kuwa limefanikiwa kuwakamata wanafunzi wawili wa chuo cha Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru kwa tuhuma za unyanyasaji wa kijinsia kwa mwanafunzi wa chuo hicho kwa njia ya mtandao na wanafunzi wenzake.
Akitoa taarifa hiyo leo Januari 29,2023 Kamanda wa Polisi mkoani Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Justine Masejo amewataja waliokamtwa kuwa ni EFRON ISAYA (32) na COSMAS ROBERT (26) wote wakiwa ni wanafunzi wa mwaka wa tatu katika chuo cha Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru.
Kamanda Masejo amesema kuwa Januari 21 mwaka huu muda wa saa 11:00 jioni huko katika Chuo cha Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru (CDTI) kilichopo wilaya ya Arumeru na Mkoa wa Arusha kuliripotiwa tukio la unyanyasaji wa kijinsia mwanafunzi wa chuo hicho (jina tumelihifadhiwa) kwa njia ya mtandao na wanafunzi wenzake.
ACP Masejo amesema baada ya kupata taarifa hiyo jeshi hilo lilianza uchunguzi kuhusiana na tukio hilo na kufanikiwa kuwakamata wanafunzi hao wawili.
Masejo amesema bado Jeshi hilo linaendelea na upelelezi wa tukio hilo na mara utakapokamilika jalada litapelekwa ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa hatua zaidi za kisheria.
Sambamba na hilo Polisi mkoani humo wametoa onyo kwa watu wachache ambao wana matumizi mabaya ya mitandao inayodhalilisha utu na heshima ya jamii yetu ya Kitanzania ambapo amewataka kuacha mara moja tabia hiyo kwani Jeshi hilo litawachukuliwa hatua kali za kisheria.