Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibaha
Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani kupitia kikosi cha Afya, Leo Juni, 23 wametoa huduma ya matibabu kwa watoto yatima wa kituo cha Buloma Foundation kilichopo Picha ya ndege, Wilaya ya Kibaha, mkoani Pwani.
Watoto hao walipatiwa huduma za kupimwa magonjwa mbalimbali, kupewa dawa na ushauri wa kitabibu kukabiliana na magonjwa yanayoweza kuepukika kwa kufanya mazoezi na kuzingatia usafi binafsi na mazingira.
Wakitoa huduma hizo kituoni hapo, Daktari wa Polisi, Koplo Hamdani Mwinchande aliwasihi watoto watoe taarifa kwa walezi wao mara wanapoona dalili za ugonjwa wowote ili wapatiwe matibabu kwa haraka kabla ugonjwa husika haujaleta madhara makubwa.
Mlezi wa watoto kituoni hapo Bi. Simfu Njogoro kwa niaba ya Mkurugenzi alishukuru Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani kwa namna wanavyotoa ushirikiano kwa jamii ikiwemo kituo hicho. Pamoja na misaada mingi wanayoipata kutoka kwa wadau mbalimbali huduma ya kiafya iliyotolewa na wataalamu hao imekua ya
kipekee sana kituoni hapo.
Huduma hizo zimetolewa baada ya Mtandao wa Polisi wanawake Tanzania (TPFNet) Wilaya ya Kibaha kutembelea kituo hicho katika maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika, Juni 16 na kubaini kuwa kuna baadhi ya watoto wana changamoto za kiafya hivyo walihitaji msaada zaidi wa kitabibu.