Leo imepita karibu wiki moja tangu lilipotokea tetemeko la ardhi mkoani Kagera, hasa Wilaya ya Bukoba. Tetemeko hili limeacha majonzi makubwa.
Taarifa nilizosoma kwenye mtandao zinaonesha kuwa watu wapatao 17 wamepoteza maisha, zaidi ya 200 wamejeruhiwa na nyumba zaidi ya 5,000 zimeathirika ama kwa kubomoka au kupata nyufa kubwa.
Nitangulie kusema bayana hapa kuwa hata mimi nimekuwa mhanga wa tetemeko. Nyumba ya mama yangu mzazi, mzazi pekee niliyesalia naye, Ma Angelina, iliyopo pale Bukoba Mjini kijiji cha Nyanga, nayo imekumbwa na tetemeko. Kama wananchi wengine, mama amepata msukosuko wa aina yake, ikiwamo kulala nje migombani kwa siku kadhaa kwa kuhofia kuingia kwenye nyumba ambayo baadhi ya kuta zimedondoka au zina nyufa kubwa.
Kwa shemeji zangu, nako huko nyumba mpya kabisa, kuta zote za ndani zimemwagika. Kimsingi, tetemeko hili lililotajwa kuwa na kipimo cha richa cha 5.7 na kwamba limepita chini usawa wa kilomita 10, limeacha madhara makubwa. Barabara zimekatika, kuna hofu kuwa huenda yamezuka mashimo tumbukizi ambayo baada ya muda au ikinyesha mvua kubwa baadhi ya maeneo yanaweza kutitia.
Sitanii, lilipotokea tetemeko yapo mambo yaliyonigusa. Naona ujumbe unaosambazwa kwenye mitandao, baadhi ya watu wakiwahurumia Wahaya kuwa mwaka huu ni zamu yao kuomba misaada tofauti na miaka yote ambayo wao hujinadi kuwa vinara wa kutoa misaada. Nimeshuhudia ujumbe mwingine unaoashiria kuwa katika msafara wa mamba kenge hawakosekani.
Kwa mujibu wa taarifa ya Sensa na Makazi ya Mwaka 2012, Mkoa wa Kagera una wakazi 2,500,000. Wakazi hao, katika nyumba moja wanaishi wastani wa watu sita. Kwa mantiki hiyo, Mkoa wa Kagera wote una nyumba zipatazo 400,000 hivi. Pamoja na ukweli huo, wapo watu tayari wanasambaza ujumbe kuwa nyumba 1,200,000 zimebomoka na hivyo wanatafuta misaada.
Ni katika hatua hiyo, naomba kutahadharisha kuwa Serikali iwe makini na wachumia tumbo. Wapo watu watalitumia tukio hili kujinufaisha kimapato. Ni vyema ukawapo utaratibu wa kutambua waathirika halisi, wenye kuhitaji misaada kweli na ikiwezekana majina yao yachapishwe kwenye vyombo vya habari kwa nia ya kuongeza uwazi.
Sitanii, tetemeko hili limetia msumari wa moto kwenye kidonda. Juni 9, mwaka huu, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, alilitangazia Taifa mikoa mitano iliyokithiri kwa umaskini. Waziri Mpango alisema Mkoa wa Kigoma unaongoza kwa kuwa na umaskini mkubwa wa 48.9% ukifuatiwa na Geita (43.7%), Kagera (39.3%), Singida (38.2%) na Mwanza (35.3%).
Kwa Mkoa wa Kagera, nasema bahati mbaya ni kubwa zaidi. Yapo matukio yenye kuhuzunisha kwa mkoa huu. Vita ya Kagera ya mwaka 1979, iliacha mkoa huu ukiwa hoi kiuchumi. Mwaka 1980, ukaingia ugonjwa uliofahamika kama Juliana (Ukimwi), ukaua nguvu kazi kwa kiwango kikubwa. Mei 21, 1996, Meli ya mv Bukoba ikazama na kuua zaidi ya watu zaidi ya 1,000. Kwa sasa hata meli ya mv Victoria iliyokuwa inategemewa haifanyi kazi.
Mkoa huo ulikuwa na Chama cha Ushirika cha BCU. Chama hiki kilikuwa na nguvu kubwa kifedha. Watawala wa nchi hii kwa hofu za kisiasa wakakifilisi chama hiki. BCU ilikuwa inalipia watoto ada shule. Mkulima alikuwa akiuza kahawa asilimia ndogo inakatwa na kupelekwa kwenye BCU. Baadaye ililetwa KCU. KCU nayo ikanyofolewa nguvu kwa kuanzisha vyama vingine vya ushirika vipatavyo 30.
Kiwanda cha kusindika kahawa cha TANICA kilichokuwa kinaajiri watu wengi kiasi, kwa sasa utendaji wake si wa kujivunia. Kiwanda pekee kinachofanya kazi ni kile cha sukari cha Kagera. Migomba imepata mnyauko, biashara kati ya Mwanza na Bukoba imekufa, gongo imeharamishwa, kokoto tulizokuwa tunauza ujenzi umesimama… ni shida.
Sitanii, kwa hali halisi ya umaskini uliopo Kagera, tetemeko hili linaweza kuzirejesha baadhi ya familia katika ujima zisipopata msaada wa dhati wa kuwajengea nyumba zao zilizobomoka. Lakini tetemeko hili sasa liwe kengele ya kutuamsha. Serikali iangalie uwezekano wa kuwezesha wawekezaji wazawa kuanzisha angalau kiwanda kimoja kikubwa mkoani Kagera kisaidie kuongeza mzunguko wa pesa.
Kimsingi kwa Mkoa wa Kagera ikiwa hakuna kitakachofanyika kuuwezesha mkoa huu kiuchumi, basi tujue miaka si mingi umaskini utaongezeka hadi asilimia 90.
Nahitimisha kwa kuwaomba walimwengu kutusaidia sisi wakazi wa Mkoa wa Kagera tuweze kurejea katika hali ya kawaida baada ya tetemeko hili, ila misaada itakayotolewa iwekewe utaratibu wa wazi jinsi ya kuwafikia walengwa.
Poleni sana wana-Kagera.