Ninahuzunika juu yako kaka yangu Absalom Kibanda. Moyo wangu umejaa uchungu. Kibanda wamekutenda vibaya, wamekuteka, wamekushambulia na kukujeruhi vibaya! Wamekusababishia kilema.

Ama kweli hujafa hujaumbika. Inavyoelezwa, watesaji wako huenda walitumwa, sijui nani kinyago na mbwa mwitu huyo aliyewatuma kukufanyia uharamia huu. Ninahuzunika juu yako Kibanda.


Matukio ya kihalifu yanaonekana kushamiri hapa nchini, sasa yanaanza kuirarua Tanzania katika suala la mhimili wa amani na upendo.Upendo na amani tulioachiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, haupo tena! Makundi ya watu wanaojihusisha na uhalifu yanaongezeka kila kukicha.


Hii ni picha mbaya kwa Serikali yetu iliyoundwa na CCM. Huu ni unyama na kutaka ‘kubaka’ uhuru wa raia na vyombo vya habari. Taarifa zinazotolewa na baadhi ya watu zinaonesha Kibanda umetekwa na watu wenye mafunzo ya ujasusi.


Ingawa bado vyombo vya usalama vinaendelea na uchunguzi juu ya tukio hilo, lakini ukweli ni kwamba Tanzania ya sasa imeanza kupoteza sifa nzuri ya amani. Ninajiuliza, hivi ni nani aliyeudharau uongozi wa Rais Jakaya Kikwete kiasi hiki?


Je, kuna watu wanaomiliki kundi la ujasusi kwa ajili ya kutesa raia nchini? Usalama wa Taifa, Jeshi la Polisi na idara nyingine zinafanya kazi gani hadi hali hii izidi kujionesha?

 

Kwa jinsi watesi wa hawa walivyoonekana kujipanga na kumfuatilia hadi siku ya tukio, hapana shaka walilenga kumuua kabisa kaka yangu Kibanda. Namshukuru Mungu hawakutimiza kusudio lao la kishenzi, kiwendawazimu na kifedhuli.

 

Tukio hili la Kibanda, huwezi kulitofautisha na lile alilofanyiwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk. Steven Ulimboka.


Huwezi kulitofautisha sana na lile alilotendewa Mhariri Mtendaji wa Gazeti la MwanaHALISI, Saed Kubenea, mwandishi mkongwe wa tasnia ya habari ambaye pia ni mshauri wa masuala ya habari nchini, Ndimara Tegambwage, na aliyekuwa Mkurugenzi wa Gazeti la Kasi Mpya la jijini Mwanza, Richard Masatu, aliyekufa katika mazingira tatanishi.


Ninalaani kwa nguvu zangu zote. Pale utawala wa nchi husika unaposhindwa kudhibiti uharamia kama huu aliofanyiwa Kibanda, unajijengea mazingira mabaya kwa wananchi wake. Kwa maana hiyo, siku zote dalili ya mvua ni mawingu, na dalili ya moto ni moshi. Hali inaweza kuwa mbaya zaidi.


JAMHURI inachotaka kujua ni kwamba, hivi ni kwa nini matukio ya utekaji, utesaji na mauaji ya kinyama dhidi ya raia yanaonekana kuongezeka wakati Tanzania ina vyombo vya usalama?

Je, vyombo hivi vimeelemewa na kazi? Au Serikali yenyewe imeshindwa kusimamia usalama na amani? Nakuhuzunikia kaka yangu Absalom Kibanda. Pole sana!

+255 (0) 777 068270