Bundi ameanza kulia ndani ya klabu ya Tottenham ya London baada ya kujikuta ikisukumwa nje ya timu nne za juu (top 4) hadi kuangukia nafasi ya sita.
Baada ya kupata ushindi dhidi ya klabu ya Real Madrid na ushindi wa ugenini dhidi ya Borussia Dortmund katika mashindano ya klabu bingwa barani Ulaya (UEFA) Tottenham imeendelea kupoteza mwelekeo kila kukicha.
Takwimu za hivi karibuni zinaonesha tangu kuanza kwa ligi timu hiyo imepoteza alama 13 kati ya 18 ambazo ilipaswa kushinda ili kuendedeleza ushindani kama ilivyozoeleka.
Akizungumzia hali hiyo Kocha wa klabu hiyo Mauricio Pochettino amesema hali kama hiyo mara nyigi hutokea kwa timu iliyokaa katika kiwango cha juu kwa mda mrefu.
Amesema klabu hiyo kwa mda mrefu imekuwa ikikabiliwa na majeruhi hasa katika idara ya ulinzi na idara zingine.
“Mwanzoni tulianza vizuri kwa kupata matokeo mazuri katika mashindano mbalimbali lakini gafla hali imebadilika” amenukuliwa Pochettino.
Amesema wachezaji wanatakiwa kutulia na kuanza kurudisha ari ya ushindi waliyokuwa nayo mwanzoni mwa ligi.
Amesema mwanzoni mwa ligi timu ilikuwa na safu imara ya ulinzi tofauti na sasa ambapo wamebaki na wachezaji kama Jan Vertonghen, Eric Dier na Juan Foyth huku wengine wakiwa majeruhi.
Wakati hali ikiwa hivyo ndani ya klabu hivyo wachambuzi wa soka nchini humo wamesema tatizo lingine linalosababisha kufanya bibaya kwa timu hiyo ni kushuka kwa kiwango cha mchezaji kama Dele Alli siku za karibuni.
Wamesema tangu msimu uanze mchezaji huyo alionesha kiwango bora kwenye ligi ya klabu bingwa barani Ulaya dhidi ya Real Madrid baada ya hapo amekuwa mchezaji wa kawaida.
Wametolea mfano katika mechi iliyopita dhidi ya Watford alitoka uwanjani huku akitikisa kichwa kuonyesha ishara kuwa hayuko katika kiwango kilichomfanya kutambulika duniani.
Kama hiyo haitoshi mapema mwezi Agosti mwaka huu mchezaji Danny Rose aliponda mfumo wa ulipaji mishahara ya wachezaji klabuni hapo.
“Hii ni klabu kubwa inayopaswa kuwa thamini wachezaji wake tofauti na ilivyo sasa ambapo hakuna usawa”amesema Rose.
Matokeo ya Spurs katika michezo 8 iliyopita.
Oktoba 28
Tottenham 0-1 Man United
Novemba 1
Tottenham 3-1Real Madrid
Novemba 5
Tottenham 1-0 Crystal Palace
Novemba 18
Tottenham 0-2 Arsenal
Novemba 21
Tottenham 2-1 Dortmund
Novemba 25
Tottenham 1-1 West Brom
Novemba 28
Tottenham 1-2 Leicester City
Desemba2
Tottenham 1-1 Watford.
Kwa vyovyote vile haya ni matokeo yanayoendelea kumuweka kocha wa klabu hii kubwa katika wakati mgumu tangia msimu huu uanze.