Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van der Pluijm amesema anakwenda Misri na timu yake vitani kuisambaratisha Al Ahly ambayo itakuwa mwenyeji wao katika mchezo wa mkondo wa pili wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1 katika mchezo wa mkondo wa kwanza uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambao inaiweka Yanga kwenye mazingira magumu kushinda mchezo wa marudiano.
Yanga ina sababu tatu za kutofanya vema baada ya kuruhusu sare na Al Ahly katika mchezo wa mkondi wa kwanza uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wiki iliyopita. Al Ahly inanolewa na Martib Jol.
Pamoja na sababu hizo, Yanga haina rekodi ya kuifunga Al Ahly kwao katika michuano mbalimbali ya kimataifa ambayo klabu hiyo ya Jangwani imekutana na ‘Waarabu’.
Hata hivyo, Pluijm amezungumza na JAMHURI Ijumaa iliyopita jijini Dar es Salaam na kusema: “Tunajua tutakutana na ugumu. Lakini nataka mashabiki wa Yanga wajue kuwa hii ni vita. Tunakwenda kupambana.”
Anasema kwamba katika mchezo wa kwanza Yanga ilifanya makosa kutoshinda, lakini inawezekana ikashinda kwao kwani katika kuiongoza timu hiyo aliwahi kuvunja mwiko kwa kuichapa mwaka juzi kwenye michuano kama hii.
“Wengi wanadhani tutafungwa. Mimi nasema mchezo ni dakika 90. Kwanini tufungwe? Mbona tumewahi kushinda hapa?” alihoji Pluijm na kuongeza: “Kutakuwa na maajabu Misri.”
Chini ya Pluijm, Yanga kwa mara ya kwanza iliwalaza Al Ahly jijini Dar es Salaam mwaka juzi kabla ya kusambaratishwa katika mchezo wa marudiano Ahly.
Katika mchezo uliofanyika jijini Alexandrie, Al Ahly walilipa kisasi kwa ushindi wa 1-0, hivyo mchezo ukahamia dakika za nyongeza kabla ya kuingia kwenye changamoto ya mikwaju ya penalty. Yanga ikafungwa penalti 4-3.
Rekodi zinaonyesho kwamba Yanga huwa inapata matokeo mazuri nyumbani lakini inafungwa Misri katika mazingira ambayo hudai kuwa ni ya hujuma kutoka kwa viongozi wa soka wa Misri na mashabiki wa Kiarabu.
Rekodi inaanza kuchuliwa kuanzia mwaka 1982, mchezo ujao utakuwa ni wa sita kwa Yanga kukipiga na Al Ahly kwani tayari zimekutana mara tano. Kwa mara ya mwisho ni ule uliofanyika Jumamosi ya wiki iliyopita.
Kabla ya mchezo wa Jumamosi iliyopita, mechi nne za zamani, Yanga ilitupwa nje na Waarabu hao katika michezo yote ya kimataifa, lakini iliweka rekodi ya ushindi huo wa mwaka juzi jijini Dar es Salaam.
Mabingwa hao wa Tanzania wanaojaribu kutetea ubingwa wao walishinda mchezo mmoja, kutoa sare mbili na kufungwa mchezo mmoja katika michezo minne iliyocheza Dar es Salaam dhidi ya timu hiyo, lakini ilifungwa michezo yote minne mingine ilipocheza ugenini nchini Misri.
Mwaka huo wa 1982, Yanga na Al Ahly zilikutana katika hatua ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Yanga kulala kwa mabao 5-0 ugenini, lakini ikakomaa Dar es Salaam na kulazimisha sare ya bao 1-1. Hata hivyo ikafungashiwa virago kwa jumla ya mabao 6-1.
Kadhalika zilikutana tena mwaka 1988 na katika mchezo wa kwanza uliofanyika jijini Dar es Salaam, timu hizo zilitoka suluhu ya 0-0 na kisha Yanga kupigwa ugenini kwa mabao 4-0 na hivyo kutolewa raundi ya kwanza katika mashindano hayo.
Miaka saba iliyopita yaani mwaka 2009, Yanga ilikubali kipigo cha nyumbani kwa bao 1-0 kutoka kwa Al Ahly pia ikafungwa ugenini mabao 3-0 katika mchezo wa raundi ya kwanza ya mashindano hayo na hivyo kutolewa kwa jumla ya mabao 4-0.