Kocha wa timu ya Yanga ya Dar es Salaam, Mholanzi Hans van der Pluijm, amewaambia wachezaji kwamba kama wanataka kuendelea kupanda ndege na kucheza mechi za kimataifa, basi hawana budi kutwaa ubingwa wa Bara.
Kocha huyo anasema anaamini wachezaji wa Yanga wana uwezo mkubwa kufanya vizuri kama watakubali kujituma na kupambana kwa hali na mali kufikia mafanikio ya zaidi ya msimu uliopita.


 “Wachezaji wanatakiwa wakaze msuli ili tufanye vizuri zaidi msimu ujao ndiyo maana kila ninapokuwa nao nawakumbusha kujituma zaidi kutokana na kutaka timu yetu ipate mafanikio zaidi na zaidi,” anasema Pluijm ambaye timu yake kwa sasa inaongoza ligi ikiwa na pointi 40.


  Anasema kwamba malengo ni kutwaa ubingwa na mara baada ya kutoka Zimbabwe, msuli utaongezeka huku akiwataka mashabiki wa timu hiyo kuacha visa vya kumzomea kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Simon Msuva, ambaye kwa sasa ana juhudi za kuzifumania nyavu kwenye michezo ya Ligi Kuu Bara inayoendelea.


 Kiungo huyo ambaye kwa sasa ndiye kinara wa kuzifumania nyavu katika Ligi Kuu Bara kwa kuwa na mabao 11, huku akimuacha kwa bao moja mshambuliaji wa Azam, Mrundi Didier Kavumbagu, aliyeongoza kwa muda mrefu.
  Pluijm  anasema, “Tangu niichukue Yanga nimemuona Msuva akifunga mabao mara kwa mara, ni vizuri kwani huwa anafanyia kazi akiwa mazoezini na ndiyo maana akiwa uwanjani hupata ujasiri na kufanya kile kinachotakiwa.”


  Pia katika kuhakikisha wanakuwa na kikosi bora zaidi msimu ujao, Pluijm anapendekeza wasajiliwe wachezaji wanne kwa ajili ya kuongeza nguvu kwenye kikosi chake.
 Yanga imekuwa ikimtumia Amissi Tambwe kama mshambuliaji wa kati ambapo hana msaidizi hadi sasa iwapo atapata majeraha kutokana na Kpah Sherman kutokuwa fiti inaweza ikapelekea Yanga kuyumba katika safu ya ushambuliaji.  


Chanzo kutoka ndani ya Yanga kimeeleza wapo katika mikakati ya kusaka wachezaji wanne kwa ajili ya usajili wa msimu ujao ili kuimarisha kikosi hicho kwa ajili ya ligi na michuano ya kimataifa.
 Nafasi ambazo zinatarajiwa kuzibwa katika usajili wa msimu ujao ni pamoja na walinzi wa pembeni, kiungo, washambuliaji wa kati na viungo wa pembeni ili kuweza kuimarisha kikosi.